Saturday, May 4, 2013

MARAFIKI, ULIMI WAKO, KABURI LA MAPENZI YAKO-5

Kwa kuanzia pale tulipoishia wiki iliyopita, tukiwa katikati ya mfano wa uhusiano wa kimapenzi kati ya Raja na Jane, tulishaona jinsi ambavyo Raja alishangazwa na majibu ya Jane akimjibu rafiki yake: “Nikipata mimba ‘naflash’ wala hakuna mgogoro kabisa.”
Siku zilivyokwenda mbele, Raja alimzoea Jane. Sasa akawa na ujasiri wa kuhoji baadhi ya vitu. Siku moja Raja aliumwa na kulazwa kwenye hospitali moja iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam. Jane alipokwenda kumwona, akamwambia: “Baby hii hospitali wanatoa sana mimba.”
Raja akashtuka kusikia kauli hiyo kutoka kwa mwenzi wake, akaiunganisha na ya siku ile alipokuwa anataniana na rafiki yake: “Nikipata mimba ‘naflash’, mbona kitu rahisi!” Vilevile Raja akayakumbuka maneno ya yule rafiki wa Jane: “Umezoea eeh, shauri yako!”
Hapohapo, Raja akamwuliza Jane: “Wewe umejuaje kama hapa wanatoa mimba?”
Jane akajibu: “Najua tu, si unajua mimi ni mwanamke?”
Raja: “Ukiwa mwanamke ndiyo ujue sehemu za kutoa mimba?”
Jane: “Je, nikisema nimeshatoa mimba hapa?”
Raja: “Hapo unamaanisha wewe ni mzoeafu wa kuchoropoa mimba siyo?”
Jane: “Unamaanisha nini kuniita mzoefu?”
Raja: “Kauli zako zinatoa picha. Siku ile ulisema ukipata mimba unaflash, leo umefika hapa hata hatujaongea kuhusu ugonjwa wangu, wewe unasema hapa wanatoa mimba. Nakuuliza umejuaje, unajibu wewe ni mwanamke, eti je, ukisema umeshatoa mimba? Asimuliaye mvua imemnyeshea.”
Jane: “Labda kama una yako, nisikwambie kitu ninachokijua? Wewe siku hizi una wivu sana.”
Raja: “Jane naanza kupata picha mbaya sana kwako. Huko nyuma ulishanitamkia kuwa wewe unapenda sana ngono, tena ulikuwa mzinzi sana. Na sasa hili la utoaji mimba. Maneno yako yanaonesha wewe ni mwanamke malaya sana.”
Maneno “wewe ni malaya sana”, yalitamkwa na Raja akiwa mbali sana kwa hisia zilizomjengea hasira. Alimwamini sana Jane na alimchukulia kwamba ni mkewe mtarajiwa. Tatizo ni Jane mwenyewe hakuwa na nidhamu ya kuzungumza. Hakujua kuchuja maneno mbele ya mwenzi wake.
Upande wa pili, Jane aliyapokea yale maneno “wewe malaya sana” kama yenye sura ya udhalilishaji. Aliona ametukanwa sana. Matokeo yake, Jane alisusa kuendelea kuwa pale hospitali, moja kwa moja akaondoka zake. Raja wala hakujali, akamwambia: “Nenda, ondoka malaya mkubwa wewe.”
Uhusiano ulivunjika hapohapo. Walipoachana, kila mtu alibaki na lake. Jane aliwaambia watu wake kwamba alishindwa kuelewana na Raja kwa sababu ni mwanamme mwenye gubu kwa kuwa ni mtu mwenye kupenda manenomaneno na hata jambo lililopita yeye hulikumbushia.
Upande wa Raja, japo hakuwa msimuliaji sana kwa watu ila pale alipoona ulazima wa kueleza, alisema Jane ni mwanamke malaya na asiyejiheshimu. Kwamba hata kama vitendo vyake vya kihuni alivifanya kwa siri au zamani, huona fahari kusimulia waziwazi kitu ambacho ni kibaya sana.

Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers

No comments: