Kama tulikuwa pamoja wiki iliyopita, utakuwa umejionea jinsi Jane alivyokosa ‘breki’ akawa anazungumza mambo ambayo yalimkera Raja ambaye baadaye alikosa subira, akamsema vibaya mwenzi wake, kisha wakagombana na kuachana.
TAFSIRI YA KWELI
Kuna falsafa mbili ambazo zinatoa tafsiri ya kweli ya kuvunjika kwa uhusiano wa Raja na Jane. Hata hivyo, zote hizo zipo chini ya mwavuli mmoja ambao ni ulimi. Pande zote mbili walishindwa kuhifadhi ndimi zao, matokeo yake, wakajikuta wanatamka mambo mazito yaliyosababisha kuachana kwao.
Falsafa ya kwanza ni busara ndogo za Jane, kutoweka kwenye mzani maneno yake kabla ya kuyatamka. Huwezi kuwa mwanamke ambaye unataka uitwe mchumba na baadaye mke bora halafu ukawa unabwabwaja maneno ya kijinga ambayo siyo tu ni kero kwa mwenzako bali pia yanashusha thamani.
Maneno ya Jane, yalimfanya Raja amshushe thamani ndiyo maana alimtamkia maneno: “Wewe ni malaya sana” na “nenda, ondoka malaya mkubwa wewe.” Unapoona mwenzi wako ambaye amezoea kukutamkia kauli nzuri, tamu zenye kubembeleza, anageuka mchungu mwenye matamshi makali, jiulize mara mbili kuhusu uhusika wako kwenye mapenzi yenu.
Alipaswa kuchunga ulimi wake, kujua ni maneno yapi ya kuzungumza na yale ambayo anatakiwa kuyahifadhi. Pengine yale maelezo ya Jane kwamba anaifahamu ile hospitali ni hodari kwa utoaji wa mimba, yasingeleta athari kubwa kama yasingetanguliwa na majisifu yake kuwa zamani alikuwa mzinzi sana na akipata mimba anaflash.
Kadhalika, inawezekana mgogoro usingefika hatua ile endapo Jane angezingatia majibu yake, kwamba angeacha kauli za mkato na dharau, badala yake angelainisha ulimi na kujibu vizuri, kitendo cha kuendelea na majibu yake ya ovyo ni sababu ya hasira za Raja kuongezeka hadi kufikia uamuzi wa kuachana.
Falsafa ya pili ni makosa ya Raja. Siku zote kama unataka kujenga uhusiano bora ni vizuri kuamini katika kufundisha. Hasira za haraka na kutoa maneno machafu, ni mambo ambayo yalimwingiza Raja katika gharama kubwa kiasi cha kumfanya auache uhusiano wake uende na maji.
Vilevile, kasoro ya Raja ni kulimbikiza mambo. Alipaswa kushughulikia kila jambo kwa wakati wake. Mfano; siku Jane alipojieleza kuwa yeye alikuwa ni mzinzi, alitakiwa ‘kudili’ naye palepale, vivyo hivyo, suala la kutoa mimba lilipojitokeza, ilitakiwa lipatiwe tiba kwa wakati wake.
Tatizo la Raja ni kuhifadhi vitu viwili vinavyomtesa, akaishi navyo. Baada ya kuongeza na kitu cha tatu, akapandwa na jazba, mwisho wakagombana wodini na kuachana kwa taadhira. Kama ulimi ungedhibitiwa, mgogoro usingefika pale ulipofikia.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment