Monday, May 27, 2013

Mbunge Mtwara atoa msimamo

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda (Kushoto), akiongozana na Mbunge wa Mtwara Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hasnein Murji baada ya sherehe za kusimikwa kwa askofu mpya na wa kwanza wa Kanisa 
  Waziri Mkuu Pinda awasilisha maombi kwa Maaskofu
  Kuzindua ujenzi kiwanda cha sementi leo
Mbunge wa Mtwara Mjini, Hasnain Mohamed Murji, amesema wananchi wa Mtwara hawazuii gesi asilia kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, bali wanachotaka ni kuwapo kwa mchanganuo wa jinsi watakavyonufaika na mradi huo.

Mbunge huyo alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kujua msimamo wake juu ya suala hilo, ambalo awali aliwahi kulizungumzia.


Mahojiano hayo yalifanyika baada ya kumalizika kwa ibada ya kumsimika Askofu wa kwanza Dayosisi ya Kusini Mashariki wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Lucas Mbedule na Msaidizi wake, Yeriko Ngwema.

“Kimsingi, hakuna anayekataa gesi asilia ya Mtwara kutoka, kinachogombaniwa ni manufaa, serikali iweke wazi sera, mrabaha na uhakika wa ajira kwa vijana ndipo iendelee kutandaza bomba la kutoa gesi,” alisema.

Alisema viashiria vibaya vinaonekana kwa kampuni ambazo zimeanza kazi katika kijiji cha Madimba eneo la Msimbati, ambako patajengwa mtambo wa kuchakata gesi asilia.

Alisema kwenye eneo hilo ajira za udereva na ulinzi ambazo hazihitaji wasomi waliobobea zimepewa watu wa maeneo mengine huku wana Mtwara wakiwa na sifa na tatizo kubwa la ajira.

Murji alibainisha kuwa wananchi wa Mtwara wanajifunza kutoka mkoa wa Lindi, ambako inapatikana gesi ya Songosongo inayosafirishwa kwenda Dar es Salaam kwamba imepita miaka tisa, lakini wananchi wa eneo hilo na mkoa hawanufaiki kwa kiwango kilichotarajiwa.

Alisema tatizo kubwa lililopo kwa sasa ni elimu kwa wananchi ambao wanaamini ujio wa gesi hiyo ndiyo mwisho wa matatizo yao bila kujua kuna changamoto kubwa ambazo wanapaswa kukabiliana nazo.

Hata hivyo, aliishukuru serikali kwa kuonyesha jitihada katika kuwasikiliza wananchi na Bunge kuunda kamati ya wabunge kwenda Mtwara kusikiliza madai ya wananchi na kujionea hali halisi.

Katika ibada hiyo ambayo iliongozwa na Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Alex Malasusa, mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, na ilihudhuriwa na maaskofu wa Dayosisi nyingine za KKKT, viongozi wa serikali na siasa na wengine kutoka ndani na nje.

PINDA: GESI ITAKWENDA DAR
Pinda akitoa salamu za serikali katika ibada hiyo, alisema msimamo wa serikali wa kutoa gesi hiyo kwenda Dar es Salaam ili itumike kwenye viwanda mbalimbali uko pale pale.

Alisema pamoja na usafirishaji wa gesi hiyo kwa bomba serikali itajenga viwanda mbalimbali, mtambo wa kuchakata gesi na kituo cha Liquid Refine Gas (LRG), ambavyo vitatoa ajira kwa wingi kwa wananchi wa Mtwara na wananchi wengine.

Pinda alisema leo anatarajia kuweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha saruji ambacho baada ya kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni tatu kwa mwaka na kuajiri wafanyakazi takribani 1,000 kiwandani na 9,000 wataajiriwa kwenye sekta binafsi kutokana na saruji itakayozalishwa.

Alisema Mei 22, mwaka huu, ilikuwa ni siku ya kuweka jiwe la msingi katika eneo litakalojengwa mtambo wa kuchakata gesi, lakini kutokana na vurugu,wataalamu waliokuwa wakijenga walikimbia na kwamba watarudi kuendelea na kazi.

KAMPUNI 45 KUWEKEZA MTWARA
Aidha, alisema hadi sasa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kina maombi takribani 45 ya kampuni zinazotaka kuwekeza mkoani humo kikiwamo kiwanda cha mbolea na bidhaa za plastiki.

“Kugundulika kwa gesi asilia kuna faida nyingi zitakazopatikana kama kuboreshwa kwa huduma za jamii kutokana na kodi ya huduma, kuwapo kwa umeme na maji safi,” alifafanua na kuongeza kuwa kampuni zitakazojihusisha na utafutaji wa gesi asilia zinashiriki kikamilifu katika kujenga miundombinu ikiwamo barabara, viwanda na kufadhili miradi ya elimu, afya na mafunzo
CHANZO: NIPASHE

No comments: