ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 31, 2013

Serikali yaomba uraia wa nchi mbili kwenye Katiba

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, imeomba suala la uraia wa nchi mbili liwekwe kwenye Katiba mpya ili kuwawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuchangia maendeleo ya nchi yao.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Wizara hiyo, Benard Membe, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara yake.

Membe alisema Watanzania wanaoishi nchi za nje wanaathirika sana na suala la uraia wa nchini mbili kwa kuwa kutokuwa na uraia wa nchi mbili kunawafanya wakose ajira za kueleweka, huduma za afya, elimu na kushindwa kuchukua mikopo katika taasisi za fedha kama wenzao wa nchi mbalimbali.


Alisema Rais Jakaya Kikwete hivi karibuni alikutana na Watanzania wanaoishi Ufaransa na Uholanzi na kuwahakikishia kuwa serikali yake inatambua na kuthamini michango yao hivyo kuwahimiza wakumbuke nyumbani.

Membe alisema katika mkutano huo, Rais Kikwete aliwahamasisha Watanzania hao wawekeze kadri ya uwezo wao na wavutie washirika wao kuja kuwekeza hapa nchini.

Kuhusu changamoto kwenye balozi zake, Membe alisema ni za kiutawala na zingine ni za kibajeti kama ilivyoelezwa hivi karibuni katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),.

Alisema ubalozi wa Tanzania nchini Abu Dhabi na Muscat zilipata hati zenye shaka kufuatia matumizi mabaya ya fedha zilizotokana na makusanyo ya maduhuli.

Membe alisema kwa upande wa Abu Dhabi, hati hiyo yenye shaka ilisababishwa na Mhasisbu wa Ubalozi mdogo Dubai kupeleka kiwango pungufu benki kwa kiasi cha Dola za Marekani 20,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 33.

Kwa upande wa Muscat, Waziri Membe alisema maduhuli ya kiasi cha fedha za Oman 20,965 hazikupelekwa benki ndani ya wakati uliostahili kama kanuni za fedha zinavyoelekeza.

Alisema katika kukabiliana na changamoto hizo, hatua za kinidhamu zimechukuliwa kwa mujibu wa sheria za UAE  za kukata mshahara wa mhasibu huyo kila mwezi ili kulipa fedha zilizopotea.
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

Ni kweli bwana wengine tumeolewa na wazungu watoto wangu Je ? USA tanzania wanatakiwa Kuwa .U cannot wait

Anonymous said...

I have heard this before. It is all talk, talk, talk and more talk with no action.