THE CIVIC UNITED FRONT- (CUF – Chama Cha
Wananchi)
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 24/05/2013
GHASIA ZA MTWARA
The Civic United Front (CUF – Chama Cha
Wananchi) kimesikitishwa sana na vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei 2013
na uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu uliofanywa na polisi tarehe 23 Mei 2013.
Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa
serikali ya CCM kutekeleza ahadi zaka za miradi ya kutumia gesi ya Msimbati na
Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo cha kufua umeme wa MW 300 na
kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi ya taifa.
CUF inalaani vikali vitendo vya kihalifu vya
kuchomea nyumba ya mwandishi wa habari wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),
Kassim Mikongolo, na nyumba za baadhi ya viongozi wa CCM. Vile vile tunalaani
vikali vitendo vya kuhujumu miundombinu muhimu likiwemo daraja la Mikindani
linalounganisha Mkoa Mtwara na Mikoa ya Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
CUF imesikitishwa sana na taarifa za vifo vya
askari wanne wa JWTZ kwa ajali ya gari iliyotokea Kilimahewa wakati askari hao
wakisafirishwa toka Nachingwea kwenda Mtwara kusaidia kudhibiti
vurugu.Tumepeleka salamu za pole kwa CDF Jenerali Mwamunyange na kupitia kwake
kwa familia za marehemu. Tunawapa pole askari wote waliojeruhiwa na kuwaombea
kwa Mwenyezi Mungu wapone haraka na waweze kurejea katika ulinzi wa taifa letu.
Vilevile tumesikitishwa na kifo cha raia
wawili kwa kupigwa risasi akiwemo mama mjamzito na raia wengi kujeruhiwa.
Tunawapa pole familia za marehemu na kuwaombea wote waloumia wapone haraka na
waendelee na shughuli zao.
Taarifa za vyombo vya habari vinaeleza kuwa
ghasia hizi zilianza baada ya hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati na Madini
iliyosomwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza ujenzi
wa bomba la kusafirisha gesi toka Mtwara kwenda Dar es Salaam.
Taarifa tulizozipata toka Mtwara zinaeleza
kuwa jana kuanzia asubuhi, wakati Waziri Nchimbi akisoma tamko la serikali
bungeni kwa niaba ya Waziri Mkuu kuwa hali ya Mtwara sasa ni shwari askari wa
Jeshi la Polisi walifanya vitendo vya kinyama kwa raia wasio na hatia. Polisi
walipita katika nyumba za wananchi na kuwachomoa vijana, kuwapiga na kuwachukua
kuwapeleka kituo cha Polisi. Mabomu ya machozi na risasi za moto zilipigwa hovyo
hovyo. Aidha katika maeneo ambayo vijana hawakuwepo waliwapiga wake zao, watoto
wadogo na hata wazee kwa madai kwamba vijana wao wanasumbua. Binti mjamzito
aitwae Fatuma alipigwa risasi na kufariki. Katika eneo la Mkana Read, Polisi
walichoma moto soko la wananchi, nyumba nyingi za raia zimechomwa moto na
polisi wamepora mali za watu zikiwemo za maduka ya wafanyabiashara. Wananchi
wengi wakiwemo wanawake wamelazimika kukimbia nyumba zao. Taarifa tulizopata
zinaeleza vitendo vya kinyama vya polisi vilisita baada ya maafisa wa juu wa
Jeshi la Polisi kufika Mtwara.
Vurugu zilizotokea Mtwara tarehe 22 Mei
hazihalalishi Jeshi la Polisi kupiga watu, kuua, kuchoma moto nyumba na vibanda
vya biashara na kupora mali za watu wasio na hatia. Vitendo hivi vya polisi kupora
mali na kuchoma vibanda vilitokea Tandahimba mwaka jana. Weledi ndani ya Jeshi
la Polisi uko chini sana. Tunalaani vikali vitendo vya Jeshi la Polisi la
kupiga watu, kuchoma nyumba na kupora. Uongozi wa Jeshi la Polisi uchukue hatua
za kinidhamu na kisheria dhidi ya polisi waliohusika na vitendo hivyo. Tunatoa
wito kwa asasi za haki za binadamu na wanaotoa misaada ya kisheria kuwasaidia
wahanga wa Mtwara kudai haki zao.
Pamoja na kulaani vitendo hivi vya kihalifu
na kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wale waliohusika na vitendo hivyo,
Serikali itafanya makosa makubwa na kuingiza nchi katika mgogoro wa muda mrefu
na wananchi wa mikoa ya kusini ikiwa itafumbia macho chimbuko la mgogoro huu na
kushikilia hoja nyepesi kuwa mgogoro huu ni matokeo ya uchochezi wa wanasiasa
wachache wanaojitafutia umaarufu. Narudia Chimbuko la mgogoro wa gesi wa mikoa
ya Lindi na Mtwara ni kushindwa kwa serikali ya CCM kutekeleza ahadi za miradi
ya kutumia gesi ya Msimbati na Mnazi Bay mkoani Mtwara na hasa ujenzi wa kituo
cha kufua umeme wa MW 300 na kuiunganisha Mtwara, Lindi na Ruvuma katika gridi
ya taifa. Mradi mwingine ni kuanzisha kiwanda cha mbolea kitakachotumia gesi
kama malighafi kama ilivyopendekezwa na Wentworth resources wanaomiliki visima
vya gesi ya Mnazi Bay na Msimbati. Kama miradi hii ingeanza kutekelezwa nina
uhakika wananchi wengi wa mikoa ya kusini hawatapinga gesi ya ziada
kusafirishwa Dar es Salaam.
Kauli ya Waziri Nchimbi Bungeni kuwa serikali
itawasaka waasisi wa vurugu hizi ndani na nje ya Mtwara ni juhudi za kutafuta
mchawi badala ya kutathmini kwa nini wananchi wa Mtwara hawaiamini kabisa
serikali ya CCM. Tumepata taarifa kuwa pana mpango kabambe wa kuwakamata
viongozi mbalimbali wa CUF na kuuaminisha umma kuwa wanaohusika na kuchochea,
kupanga na kutekeleza vurugu za Mtwara ni viongozi na wafuasi wa CUF. Serikali
ya CCM imekubuu katika kubambikia kesi nzito watu wasiokuwa na hatia. CUF
inafanya siasa kwa kujenga hoja. Katika suala la gesi tumejenga hoja za
kiuchumi na maendeleo na uwajibikaji wa kisiasa kuhusu utekelezaji wa miradi
ambayo CCM na serikali yake iliahidi kuitekeleza. Viongozi wa CUF hawajachochea
vurugu wametumia majukwaa ya mikutano ya hadhara na maandamano ya amani kujenga
hoja za kimsingi.
Mimi binafsi nilienda Mtwara mwaka jana
nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara Mtwara mjini kwa madai kuwa hali siyo
shwari wilaya ya Tandahimba. Wananchi wa Mtwara walitaka nifanye mkutano huo pamoja
na kuwa umezuwiwa na polisi, nikawasihi tusifanye hivyo na wakakubali. Tarehe
14 Aprili 2013 nilikuwa Mtwara nikazuwiwa kufanya mkutano wa hadhara sikukaidi
nikafanya mkutano wa ndani. Maalim Seif, Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza
wa Rais wa Zanzibar alitaka kufanya ziara ya mkoa wa Mtwara akaambiwa hana
ruhusa ya kufanya mikutano ya hadhara mkoa wa Mtwara na hivyo akasitisha ziara
yake.
Kuwakamata viongozi wa CUF wa wilaya za
Mtwara na Lindi na wa kitaifa hakutamaliza mgogoro kati ya serikali na wananchi
wa Mtwara ikiwa serikali itaendelea kuwabeza, kuwadharau na kutowasikiliza.
Badala yake itaongeza chuki dhidi ya serikali.
Wakati wananchi wa Mtwara wamepoteza imani
kwa uongozi wa CCM na serikali yake, Serikali imezuia vyama vingine vya siasa
na asasi za kiraia kufanya shughuli za kuwasiliana na wananchi wa Mtwara na kwa
hiyo kuunyima umma miongozo ya kisiasa za demokrasia. Umma uliokata tamaa na
unaoamini unabezwa, kudharauliwa na kudanganywa na watawala unaweza kuchukua
hatua zenye madhara hata kwa maslahi yao wenyewe.
Serikali imekuwa inapotosha kwa makusudi
madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara ambayo ni kuwa serikali itekeleze miradi
ya gesi iliyoahidi wananchi wa Mtwara. Badala yake wananchi wa mikoa mingine
wanalishwa sumu kuwa Wananchi wa Mtwara hawataki raslimali ya gesi iwanufaishe
Watanzania wengine. Umeme ukifuliwa Mtwara na kuunganishwa katika gridi ya
taifa utatumiwa na wote waliounganishwa na gridi ya taifa. Kiwanda cha mbolea
cha Mtwara kitazalisha mbolea itakayotumiwa nchi nzima. Wananchi wa Mtwara
hawajasema Watanzania wengine hawana haki ya kwenda Mtwara kupata ajira au
kufanya shughuli za kibiashara. Wanaobomoa umoja na mshikamano wa kitaifa ni
wale wanaowabeza, kuwadharau na kuendelea kuwadanganya wananchi wa Mtwara na kupandikiza
sumu kwa Watanzania wengine kwa kupotosha madai ya msingi ya wananchi wa Mtwara
na kushindwa kwa serikali kuwajibika kisiasa kwa ahadi ambazo viongozi akiwemo
Rais alizitoa kwa wananchi wa Mtwara.
Wananchi wa Mtwara zaidi ya elfu 24 wameweka
sahihi na kupeleka ombi (petition) kupitia Mhe. Habibu Mnyaa, Mbunge wa
Mkanyageni kujadili kutekelezwa kwa miradi ya gesi ya Mtwara. Spika Anna
Makinda kazuwia ombi hilo kujadiliwa.
Bunge limeshindwa kuisimamia serikali na
kuhoji kwa nini mradi wa kufua umeme MW 300 ambao katika mwaka wa bajeti wa
2011/12 ulitengewa na kutumia shilingi 540 milioni umesitishwa. Mpaka hivi sasa
hakuna kamati ya Bunge iliyoenda kusikiliza kilio cha Wananchi wa Mtwara badala
yake Spika amekuwa mstari wa mbele kuunga mkono vitendo vya serikali badala ya
kuhakikisha kuwa Bunge linaisisimamia serikali.
Katika hotuba ya bajeti ya mwaka huu, Waziri
kaeleza serikali kupitia TANESCO kwa kwa kushirikiana na kampuni ya Symbion
itajenga kituo cha kufua umeme cha MW 400 na kuunganisha Mtwara na gridi ya
taifa kupitia Songea. Hata hivyo bajeti ya maendeleo haijautaja mradi huu wala
kutenga hata shilingi 1 kwenye mradi. Wananchi wa Mtwara wanaona wanaendelea
kudanganywa na serikali ya CCM. Mikogo, majigambo na kauli za kejeli za Waziri
wa Nishati kuhusu uelewa mdogo wa wananchi wa Mtwara katika masuala ya gesi
zinazidi kuongeza chuki na jazba za wananchi. Mpaka hivi sasa serikali imekataa
kuweka wazi mkataba wa ujenzi wa bomba na upembuzi yakinifu wa mradi huu.
Hotuba ya bajeti ya Waziri wa Nishati haielezi kama Wentworth Resources
wanaoendesha visima vya gesi wataweza kuzalisha gesi kukidhi ukubwa wa bomba la
kusafirisha gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam na ahadi mpya za miradi ya
kutumia gesi mkoani Mtwara.
Linalonistusha na kunitisha ni kwa nini
viongozi wa juu wa serikali hawataki kuwa wawazi kuhusu mradi huu na wako
tayari kupotosha, kuwagawa wananchi na kudanganya alimuradi mradi huu
utekelezwe na usihojiwe?
Gesi ya Mnazi Bay, Mtwara iligunduliwa toka
mwaka 1982 lakini mpaka hivi sasa haijatumiwa kikamilifu. Kampuni ya Artumas
ilianza utaratibu wa kuichimba gesi mwaka 2006 na kuitumia kufua umeme wa
Megawati 18. Tarehe 17 Oktoba 2007 kampuni ya Artumas ilitoa taarifa ya mpango
wake wa kujenga kituo cha kufua umeme wa MW 300. Mpango huu ulitarajiwa
kugharamiwa toka Mfuko wa Maendeleo wa Uholanzi - Netherlands Development
Finance Company. Gharama za mradi wa kufua umeme zilikadiriwa kuwa dola za
Marekani 225. Kampuni maalum ya kuendesha mradi huu ya Tanzania Generation
Company Ltd (TANGEN) ilisajiliwa ili kujenga na kuendesha mradi huu. Kampuni
hii ingekopa dola milioni 160 na dola milioni 65 zingechangiwa kama hisa na
kampuni nyingine zikiwemo mifuko ya pensheni ya Tanzania na kampuni ya madini
ya Barrick International.
Kampuni nyingine maalum ilitarajiwa
kuanzishwa ili ijenge msongo wa umeme (nguzo za nyaya za kusambaza umeme) na
kuunganisha umeme wa Mnazi Bay kwenye gridi ya taifa. Mradi huu ungegharimu
dola milioni 400. Mradi huu ulitarajiwa kugharamiwa na mifuko ya pensheni ya Tanzania
na wawekezaji kutoka Mashariki ya Kati. Mpango huu ulikubaliwa na serikali na
ukaingizwa katika Mpango Kabambe wa Taifa wa kufua na kusambaza umeme (National
Power Development Master Plan). Mradi huu wa kufua umeme MW 300 Mtwara
ulipangwa uwe umekamilika mwaka wa 2012. Tovuti ya Tanesco inaueleza mpango huu
kuwa ni wa muda wa kati. Bila shaka serikali iliukabali mradi huu baada ya
kuufanyia utafiti na upembuzi yakinifu.
Mtikisiko wa sekta ya fedha na uchumi wa
dunia wa mwaka 2008 uliathiri kampuni ya Artumas. Thamani ya hisa moja ya
Artumas iliporomoka toka dola za Marekani 10.80 mwezi wa Aprili 2008 na kufikia
dola 0.12 mwezi wa Machi 2009. Kampuni ilipata matatizo makubwa ya ukata na
ilibidi serikali iisaidie dola milioni 7 ili iweze kuendelea na ufuaji wa umeme
wa MW 18 Mtwara. Barrick International ilijitoa katika mradi wa TANGEN. Katika
kujiunda upya Kampuni ya Artumas Group Inc. iliamua kubadilisha jina lake na
kuwa Wentworth Resources Limited na kuteua menejimenti mpya.
Tarehe 10 Juni 2009 Rais Kikwete alipokuwa
anawahutubia Wabunge na Wananchi katika Ukumbi wa Kilimani Dodoma kuhusu athari
za mtikisiko wa uchumi duniani alieleza “Kwa sababu ya matatizo ya uchumi
uwekezaji wa vitega uchumi kutoka nje umepungua. Wawekezaji wamekuwa wanakosa
fedha kutoka mabenki na masoko ya mitaji. Matokeo yake ni kuchelewa au kukosa
kabisa au kuahirishwa miradi mikubwa ambayo ingetoa mchango muhimu kwa ukuaji
wa uchumi wetu na ajira. Kwa mfano: Mradi wa umeme wa MW 300 kule Mtwara kwa sababu
ya Barrick Gold Ltd. kujitoa na Artumas peke yake haina uwezo wa kifedha; mradi
wa nickel Kabanga, mradi wa aluminium smelter, Mtwara; mradi wa usambazaji
umeme mkoani Mtwara, miradi ya viwanda vya saruji na mbolea Mtwara.” Kwa kauli
ya Rais ambayo wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla waliisikia kwani
hotuba hii ilirushwa live na Shirika la Utangazaji la Tanzania – Radio na
Televisheni na vyombo vingine vya habari. Miradi ya kutumia gesi ni pamoja na
kufua umeme MW 300, kutengeneza mbolea inayotumia gesi kama malighafi,
aluminium smelter inayohitaji umeme mwingi, na kiwanda cha saruji ambacho
kinatumia umeme na kinu chake kinaweza kutumia gesi. Wananchi wakamuamini Rais
wetu na wakaelewa kuwa miradi hii imekwama kwa sababu ya mtikisiko wa uchumi na
kwamba serikali inajitahidi kutafuta njia mbadala ya kujikwamua ili miradi hiyo
iendelee.
Wakati wa kampeni ya uchaguzi wa 2010, Rais
Kikwete aliwaeleza wananchi wa Mtwara akichaguliwa ataendeleza miradi ya Mtwara
itakayotumia gesi ya Mnazi Bay. Maelezo ya Ilani ya CCM ya Uchaguzi wa 2010,
ibara ya 63 kifungu (j) Kuzalisha umeme (300MW) kutokana na gesi asili ya Mnazi
Bay (k) Kupanua mitambo ya kusafisha gesi na bomba la kusafirisha gesi kutoka
Songo Songo hadi Dar es Salaam. Mitambo ya kufua umeme ya Dar es Salaam
ilitegemewa itumie gesi ya Songosongo kwani bomba la kutoka Songosongo hadi
Somanga mpaka Dar es Salaam lingepanuliwa. Toka mwaka 2010 kampuni ya Globeleq-
Songas ilijiandaa kutekeleza mradi wa kuongeza uwezo wa bomba la gesi kutoka
Songosongo – Somanga – Dar es Salaam ili likidhi mahitaji ya gesi ya vituo vya
kufua umeme Dar es Salaam kikiwemo kituo cha Kinyerezi. Serikali iliisitisha
kampuni hiyo isiendelee na mradi huo ambao hivi sasa ungekuwa umekamilika na
kuongeza uwezo wa kufua umeme kwa kutumia gesi kwa alau MW 200.
Rais Kikwete alipoenda Mtwara kuhudhuria
sherehe ya Mashujaa tarehe 25 Julai 2011 alizungumza na wananchi wa Mtwara na
kueleza miradi ya maendeleo itakayotekelezwa kwa kutumia gesi ya Mnazi Bay
ikiwemo ufuaji wa umeme wa MW 300 na kupanua bandari ya Mtwara.
Tarehe 12 Oktoba 2011, Ikulu ilitoa taarifa
kwa vyombo vya habari kuwa “Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Oktoba 12, 2011, amepokea ripoti kutoka
makampuni mawili ya kimataifa kuhusu Mpango Kabambe ya mradi mkubwa wa umeme
ambao utaunganisha kwenye Gridi ya Taifa mikoa yote sita ambayo kwa sasa haiko
kwenye gridi hiyo. Rais Kikwete amepokea ripoti hiyo kutoka makampuni ya China
National Machinery&Equipment Import&Export Corporation (CMEC) ya China
na Siemens ya Ujerumani ambayo kwa pamoja yanatarajia kujenga kituo kikubwa cha
kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara na pia
kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida.
Mradi huo mkubwa wa umeme wa megawati 300 utakaogharimu karibu dola za Marekani
milioni 684 na utakaozalisha umeme wa moja kwa moja na wenye nguvu kubwa ya 300
kV (300 kV High Voltage Direct Current – HVDC) utagharimiwa kwa pamoja na mkopo
kutoka Benki ya Exim ya China na Serikali ya Tanzania.”
Mikoa sita ambayo bado haijaunganishwa na
gridi ya taifa ni Lindi, Mtwara, Ruvuma, Rukwa, Kigoma na Kagera. Mradi huu
pamoja na kufua umeme wa MW 300 Mtwara ungekamilisha kuunganisha mikoa yote ya
Tanzania kwenye gridi ya taifa. Taarifa iliendelea kueleza “Kuunganisha mikoa
yote ya Tanzania kwenye Gridi ya Taifa ilikuwa moja ya ahadi kubwa zilizotolewa
na Serikali ya Rais Kikwete wakati anaingia maradakani na kwa kuuunganisha
mikoa hiyo sita kwenye Gridi hiyo, Serikali hiyo itakuwa imetimimiza ahadi
hiyo.”
Maelezo haya yametolewa na Ikulu na vyombo
vya habari vikayatangaza na wananchi wa Mtwara wakasikia. Kutekeleza mradi wa
kufua umeme kutaifanya Mtwara iwe na umeme wa kutosha kushawishi kampuni
kuanzisha viwanda hasa ukizingatia ahadi ya Rais Kikwete ya kupanua bandari ya
Mtwara. Mwaka wa fedha wa 2011/12 serikali ilitenga na kutumia shilingi 540
milioni fedha za maendeleo za mradi wa Mnazi Bay 300MW Development Project.
Baada ya hapo mradi huu haukutengewa fedha tena. Badala ya mradi huu
kuendelezwa kama Rais alivyowaahidi wananchi wa Mtwara na Watanzania kwa ujumla
badala yake wanasikia serikali imezindua mradi wa kujenga bomba la kusafirisha
gesi toka Mtwara kuja Dar es Salaam.
Kwa taarifa ya Ikulu gharama za mradi wa
kufua umeme wa MW 300 Mtwara na kuiunganisha mikoa sita katika gridi ya taifa
gharama yake ni dola milioni 684. Mradi wa kutandaza bomba la gesi unagharimiwa
na mkopo wa dola milioni 1220 kutoka Benki ya Export Import Bank ya China. Ni wazi
gharama za kufua umeme Mtwara na kuunganisha mikoa sita kwenye gridi ya taifa
ni ndogo zaidi kuliko gharama za kutandaza bomba la gesi.
Msongo wa umeme za kV 400 unajengwa
kuunganisha Iringa – Dodoma – Singida na Shinyanga. Mradi huu unatekelezwa na
Benki ya Maendeleo ya Afrika. Nyaraka ya mradi unaonyesha gharama za kujenga
umeme za kV 400 ni dola za Marekani 600,000 kwa kilomita 1. Gharama za
kujenga bomba la gesi lenye kipenyo (upana wa nchi 36) ni dola 1,309,636 kwa
kilomita 1. Kwa madhumuni ya kufua umeme, gharama ya kujenga bomba la gesi ni
zaidi ya mara mbili ya gharama za kunganisha Mtwara na Dar es Salaam. Isitoshe
unaweza kuongeza ufuaji wa umeme Mtwara na kusambaza kwa msongo huo huo.
Ujenzi wa bomba la Dar es Salaam Mtwara
umeanza bila kuwa na mipango ya kuhakikisha kuwa kutakuwepo na gesi ya kutosha
kuisafirisha hadi Dar es Salaam. Bomba hili litakuwa na uwezo wa kusafirisha
futi za ujazo bilioni 200. Uwezo wa gesi ya Mnazi Bay na Msimbati kwa hivi sasa
ni futi za ujazo bilioni 80. Hakuna mpango unaoeleweka wa kupata futi za ujazo
bilioni 120 ili bomba la gesi liweze kutumiwa kikamilifu.
Mpaka hivi sasa gesi kiasi cha futi za ujazo
trilioni 33.7 imegunduliwa katika bahari yenye kina kirefu. Uchimbaji wa gesi
hii bado haujaanza. Inaweza kuchukukua miaka 7 – 10 kabla ya shughuli ya
uchimbaji wa gesi kukamilika. Kampuni zilizogundua gesi bahari kuu bado
hazijafanya uamuzi wa utaratibu wa kuichimba na kuisafirisha gesi hadi nchi
kavu. Kwa kuwa gharama za kujenga bomba la gesi chini ya bahari ni za juu sana,
kampuni hizi zitapendelea kutandaza bomba kwenda nchi kavu kwenye eneo lililo
fupi kuliko yote. Statoil imegundua gesi nyingi eneo la Zafarani bahari kuu
eneo la mkoa wa Lindi. Hivi sasa wanatazama maeneo ya Kilwa kuweza kuweka kituo
cha nchi kavu. Bandari ya Lushungu kata ya Limalyao, wilaya ya Kilwa ambayo ina
kina kirefu cha bahari yaelekea kuwavutia. Kwa hivi sasa hakuna uhakika gesi
iliyogunduliwa bahari kuu itapelekwa Mtwara. Uamuzi wa kujenga bomba kubwa
umefanywa haraka haraka bila kutathmini kikamilifu faida zake kiuchumi. Jambo
la kujiuliza kwa nini uamuzi huu umechukuliwa na kuacha kutekeleza mradi wa
kufua umeme Mtwara wenye mantiki kiuchumi, kijamii na uwajibikaji wa kisiasa?
Wentworth Resources wamefanya upembuzi
yakinifu (feasibility study) na kubaini kwamba njia nzuri ya kibiashara na
kiuchumi ya kutumia gas wanayoweza kuzalisha Mnazi bay hivi sasa ni kuanzisha
kiwanda cha kutengeneza mbolea na kemikali nyingine Mtwara. Kiwanda cha mbolea
chenye faida kubwa kinaweza kuanzishwa na kuendeshwa hata kama akiba ya gesi
iliyogunduliwa siyo kubwa sana kama ilivyo Mnazi Bay. Mradi wa kujenga kiwanda
unaweza kukamilishwa kwa muda mfupi. Pamoja na mbolea kiwanda kitazalisha
methanol yenye soko kubwa duniani. Kiwanda kitatumia hewa ukaa (carbondioxide)
na kwa hiyo kuweza kupata fidia ya kuboresha mazingira. Uongozi wa Wentworth
Resources una uzoefu wa miaka mingi katika miradi ya kutumia gesi. Wanajua
wanalolieleza. Hata hivyo serikali imewamrisha kupeleka gesi watakayozalisha
kwenye bomba la gesi la kwenda Dar es Salaam.
Serikali imeanzisha mgogoro wa gesi kwa
kuanza kutekeleza mradi mkubwa wa kutandaza bomba la mafuta na kuacha miradi
yenye manufaa makubwa kiuchumi na kijamii kwa taifa letu. Uchunguzi huru na wa
kina ufanyike kubaini sababu za serikali kuacha miradi ya kutumia gesi Mtwara
na kukumbatia mradi wa kutandaza bomba. Ripoti aliyopewa Rais ya mradi wa kufua
umeme Mtwara na kuunganisha mikoa 6 katika gridi ya taifa itolewe ili
Watanzania waweze kuelewa mantiki ya mradi huu. Mkataba wa mkopo na utekelezaji
wa mradi wa kutandaza bomba la gesi uwekwe wazi. Serikali iruhusu kampuni ya
Wentworth resources kuendelea na mradi wa kiwanda cha mbolea. Rais aende Mtwara
kuwaeleza wananchi kuwa ahadi alizoeleza za kutumia gesi Mtwara zitatekelezwa.
Vyama vya siasa na asasi za kiraia viruhusiwe
kufanya mikutano ya hadhara kueleza njia za kidemokrasia za kudai haki za
kiuchumi za wananchi wa Mtwara. Bunge liunde kamati teule ya kuchunguza kwa
nini Mradi wa Kufua umeme MW 300 umesitishwa na serikali, upembuzi yakinifu wa
mradi wa bomba la gesi na mikataba yote inayohusiana na mradi huu.
Sakata hili la gesi ya Mtwara linaonyesha
wazi kuwa hatuna sera muafaka na mkakati wa kuendeleza sekta ya gesi kwa
manufaa ya taifa letu na Wananchi wa kawaida. Badala ya gesi kuwa neema
inaelekea kuwa itakuwa balaa na laana. Sera ya gesi inapaswa kuweka taratibu
zitakazohakikisha kuwepo kwa uwekezaji wa kutosha katika sekta hii na
utakaolinufaisha taifa letu bila kuathiri motisha kwa wawekezaji wenye
teknolojia ya kutafuta na kuchimba gesi. Wananchi wa Mtwara wanahitaji
kushirikishwa. Serikali iwe wazi na kutoa taarifa sahihi kuhusu miradi ya gesi.
Prof. Ibrahim Haruna
Lipumba,
Mwenyekiti wa Taifa, Mei 24 2013.
No comments:
Post a Comment