ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 11, 2013

Ubingwa waipa Yanga Sh70 mil

Wachezaji wa Yanga wakishangilia bao katika moja ya mechi za Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga.

Dar es Salaam. Yanga itavuna Sh70 milioni kama Bingwa Ligi Kuu Bara msimu huu, ikiwa ni nyongeza ya Sh20 milioni zaidi ya walizopata mahasimu wao wakubwa na mabingwa wa msimu uliopita, Simba ya Dar es Salaam.
Hii ni mara ya kwanza kwa bingwa wa Ligi Kuu Bara inayofikia tamati Jumamosi ijayo kwenye viwanja mbalimbali, kupewa zawadi kubwa ya pesa kiasi hicho kutoka kwa wadhamini.
Kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya Sh200 milioni, ambazo wadhamini wakuu wa Ligi Kuu, Kampuni ya Huduma za Simu ya Vodacom walitangaza kutumika kama zawadi.
Tofauti na misimu mingine, ambapo mshindi wa kwanza na pili ndiyo waliokuwa wakipewa zawadi, safari hii timu zote zitakazoshika nafasi nne za juu zitapewa zawadi ya pesa.
“Mwaka huu tutatumia kiasi cha Sh200 milioni kwa ajili ya zawadi za fedha taslimu kwa washindi wa Ligi Kuu ya Vodacom. Bingwa atanyakua Sh70 milioni.” alisema Ofisa Uhusiano wa Nje wa Vodacom, Salum Mwalimu.
Mwalimu alisema kuwa lengo la kuongeza kiwango cha fedha za zawadi ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya wadhamini wa ligi na wadau wengine wa soka.
“Dhamira yetu kubwa ni kuhakikisha ushindani unakuwepo kwenye michuano ya ligi na pia kuzipa fursa timu kufaidi matunda ya ushiriki wao kwa kuroa zawadi nono,” alisema bosi huyo.
Yanga ilitwaa ubingwa kabla hata ya msimu kumalizika, huku Azam ikiambulia nafasi ya pili. Zote zitacheza michuano ya Klabu Afrika mwakani.
Mbali ya kitita hicho atakacholamba bingwa, Vodacom pia ilitangaza zawadi ya mshindi wa pili kuwa ni Sh35 milioni, ikiwa ni nyongeza ya Sh5 milioni.
Mshindi wa tatu ataondoka na Sh25 milioni, huku mshindi wa nne akiingiza mfukoni Sh20 milioni, walisema wadhamini Kampuni ya Vodacom.
Simba inakamata nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45 na Kagera Sugar iko nafasi ya nne ikiwa na pointi pointi 40.
Aidha, katika mfumo mpya wa zawadi, Mwalimu alisema mchezaji bora wa mwaka, kipa bora na mfugaji bora, kila mmoja ataondoka na kiasi cha Sh5 milioni.
Vilevile, safari hii mwamuzi bora wa Ligi Kuu atapata Sh7.5 milioni, kiasi ambacho pia atazawadiwa kocha bora wa mwaka, huku timu itakayoonyesha nidhamu nzuri kwenye michuano hiyo itazawadiwa Sh15 milioni.
Mwananchi

No comments: