ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, May 11, 2013

Watoto waangalia filamu za ngono mitaani

Kamanda Suleiman Kova 
Dar es Salaam. Kuwepo kwa mabanda mengi ya kuonyesha filamu yasiyo na usimamizi nchini, kumewapa watoto wadogo nafasi ya kuangalia picha za ngono, huku Serikali ikishindwa kuchukua hatua stahiki ikiwamo kuyafunga mabanda hayo.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumamosi katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwepo kwa idadi kubwa ya mabanda ya kuonyesha filamu katika makazi ya watu, hivyo kuwapa watoto nafasi ya kutazama picha zisizofaa kimaadili.
Uchunguzi huo uliofanyika mchana na usiku, umebaini kuwa baadhi ya wazazi huwapa watoto wao fedha kwenda katika mabanda hayo bila kujua aina ya filamu wanazokwenda kuangalia, huku wazazi wengine wakiwa hawana taarifa kuwa watoto wao huingia katika mabanda hayo.
Katika mitaa ya Kigogo na Mburahati, baadhi ya wanawake walikutwa saa tatu usiku wakiangalia filamu kutoka barani Asia huku wakiwa wamebeba watoto wadogo. Sehemu kubwa ya filamu hiyo ilikuwa ikionyesha watu wakishiriki tendo la ndoa.
Msimamizi wa banda hilo (jina tunalo) alipoulizwa alisema: “Hilo ni picha la Amitabh Bachchan.”
Hata hivyo, baada ya kuiangalia video hiyo kwa muda wa zaidi ya dakika 20, ilibainika kuwa filamu hiyo ilikuwa imechanganywa na filamu nyingine tofauti na ile iliyotajwa.
Katika banda moja lililojengwa kwa mifuko ya plastiki katika Mtaa wa Kabojonga, Mtoni Kijichi walionekana wanawake wanne wakiwa wamekaa sakafuni saa tatu usiku, huku wamewapakata watoto wadogo waliokuwa wamelala.
Chumba hicho kilikuwa kimejaa watoto wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka mitano hadi 17. Walikuwa wamekaa kimya, wakifuatilia filamu iliyotafsiriwa kwa Kiswahili
Kama ilivyokuwa katika mabanda mengine, watoto hao walikuwa wakiangalia filamu kutoka barani Asia iliyofahamika kwa jina la Train.
Msimamizi wa banda hilo, muda wote alionekana kushika ‘remote control’ kwa ajili ya kusogeza mbele baadhi ya sehemu katika filamu hiyo, ambazo zinaonyesha utupu kitendo kilichowafanya watazamaji kulalamika.
“Ina scratches nyinyi, hamuoni?” alijibu msimamizi wa banda hilo, lakini ukweli ni kwamba alikuwa akitaka kusogeza mbele sehemu inaonyesha watu wakifanya ngono.
Saa nne usiku, katika banda jingine eneo la Mbagala Charambe, watoto wawili walikutwa wakiangalia filamu kupitia tundu lililopo kwenye moja ya kona ya banda hilo lililojengwa kwa turubai kuukuu. Ndani ya banda watu walikuwa wakiangali filamu ya ngono.
Kwa mujibu wa watoto hao, wanafunzi wa shule ya Msingi Majimatitu (majina tunayo) walifukuzwa kutoka ndani ya banda hilo baada ya kukosa fedha za kulipia ‘picha’ ya pili baada ya ile ya mwanzo waliyokuwa wakiangalia kumalizika.
“Mwanzo tulikuwa tunaangalia filamu ya Sarafina, lakini naona sasa wamebadilisha wameweka picha ya kizungu,” alisema mtoto mmoja.
Mbinu zinazotumika
Ilibainika kuwa wenye mabanda ya kuonyesha filamu hubandika ukutani matangazo ya filamu zitakazoonyeshwa siku hiyo, lakini huzibadilisha baadaye na kuweka filamu za ngono.
Katika baadhi ya mabanda ilibainika kuwa huanza kuonyesha mikanda ya ngono kuanzia saa tatu na saa sita usiku wakati watu wengi wamekwenda kulala.
Wenye mabanda hayo ya filamu wamebainika pia kutumia majina tofauti yanayotaja mikanda ya ngono.
Baadhi ya majina hayo ni ‘Pilau’, ‘Blue’, ‘Kuchikuchi Hotae’, ‘Yale mambo yetu’ na ‘Picha la ukweli’.
Katika banda moja huko Tandika, haruhusiwi mtu asiyefahamika kuingia ndani ya banda hilo. Jitihada za kujua nini kilichokuwa kikiendelea katika banda hilo zilifanikiwa baada ya kumtumia binti mmoja (jina tunalo) mwenyeji wa eneo hilo, aliyetuthibitishia kuwa filamu iliyokuwa ikitazamwa ndani ilikuwa ni ya ngono.
Uchunguzi ulibaini pia kwamba mabanda mengi yanayoonyeshsa filamu mitaani hayana leseni, huku baadhi yao leseni zake zikiwa zimeisha muda wake.
Kilichobainika kuhusu watoto
Baadhi ya watoto waliohojiwa, wengi wakiwa ni wanafunzi wa shule za msingi, walisema wameshaona zaidi ya mara moja filamu za watu wakifanya ngono katika mabanda ya kuonyesha filamu hizo.
“Tuliona kwa (analitaja banda la kuonyesha filamu) watu walikuwa wakifanya ngono bafuni, baadaye wakaenda chumbani,” alisema mtoto (jina tunalihifadhi) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mabibo, Kinondoni.
Mtoto mwingine wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Tumaini, Ilala, alisema aliwahi kufukuzwa kutoka kwenye banda ambalo watu walikuwa wakiangalia filamu za ngono.
“Mwanzo tulikuwa tunaangalia ‘muvi’ ya Kanumba, ilipoisha wakaweka ya kizungu…wakati inaanza niliona watu hawana nguo nikaanza kucheka wakanifukuza wakasema nitoke mimi bado mdogo,” alisema mtoto huyo wa miaka 13.
Maoni ya wazazi
Wazazi walioonyesha kukerwa na tatizo hilo, waliilalamikia Serikali kwa kushindwa kuyafunga mabanda ya filamu na kusema ni vyema kama litatumika Jeshi la Polisi kuyafunga na ikibidi kuyabomoa kabisa.
“Siku hizi watoto nyumbani wanafanya mambo ya ajabu, ukiwauliza mmejifunza wapi wanakwambia tulikuwa tunaangalia mkanda wa video, …tumechoka, bora wayavunje kabisa mabanda hayo,” alisema Voida Sanga mkazi wa Sinza Kijiweni.
Mchungaji wa Kanisa la Assemblies of God (TAG) Kimara, Festo Segesela alisema kuwa hali imekuwa mbaya katika baadhi ya mitaa kwa kuwa kuna wasichana wadogo wanaokwenda kuangalia mikanda ya ngono, huku wakiwa wamebeba watoto mgongoni.
“Kwa kweli hali ni mbaya…, kizazi chetu kinaangimia, wengine ni mabinti wadogo kabisa wanakwenda kuangalia hiyo mikanda ya ngono wakiwa na watoto mgongoni,” alisema Segesela.
Akifafanua, Segesela alisema kuwa hali imefika ilipo sasa kutokana na viongozi wa Serikali kuingiza siasa katika mambo yanayohitaji kuchukuliwa hatua za haraka.
“Kuna baadhi ya viongozi wanashindwa kuchukua hatua kwa sababu tu wanaogopa kunyimwa kura, hii ni hatari kwa kweli,” alisema Segesela
Hata hivyo, baadhi ya wazazi waliunga mkono kuwepo kwa mabanda ya kuonyesha filamu kwa kile walichosema kuwa watoto wao hutumia muda wa jioni kuangalia video badala ya kwenda mitaani kuzurura.
“Ni bora nikampa mwanangu shilingi mia, aende kuangalia video kuliko aende kucheza mitaani ambako hata sielewi atakutana na nani,” alisema Vicky Tarimo mkazi wa Mwananyamala Kisiwani
Wazazi wengine waliwarushia lawama wazazi wenzao kwa kushindwa kuwaangalia watoto wao, kwa madai kuwa baadhi ya watoto wamekuwa wakitumia siku nzima katika mabanda ya filamu hizo, huku wazazi wao wakiwa hawana taarifa ya kitu kinachoendelea
“Mzazi hajui mtoto wake yuko wapi siku nzima, amepata fedha wapi ya kuangalia hiyo mikanda? Hata kama ni shilingi mia kila mkanda, lazima ujue amepata wapi,” alisema Elias Naftari mkazi wa Kigogo Mburahati.
Mwenyekiti wa Bazara Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mtaa wa Twangoma Temeke, Darwesh Kinicha alisema iwapo hali itaachwa iendelee ilivyo sasa maadili ya jamii yatavurugika na kubaki na kizazi kisicho na mwelekeo.
Akitoa mfano, Kinicha alisema mtoto wake ambaye ana miaka saba tayari ameshaanza kuonyesha dalili zinazoashiria kuwa ameshajifunza mambo yasiyofaa.
“Mimi mwenyewe mtoto wangu yupo darasa la saba anazungumza mambo hayo hayo; …kutokana na vitendo anavyofanya na wenzake, nimeamua kumpeleka madrasa, akitoka huko namfungia ndani sitaki aende kucheza kokote,” alisema Kinicha.
Aliongeza: “Nimeamua kununua TV awe anaangalia channel ya Baby TV, lakini ni wazazi wangapi wanaoweza kufanya hivi?,” alihoji Chinicha.
Kwa mujibu wa Chinicha, vitendo vya watoto kuangalia filamu za ngono vimezidi zaidi katika maeneo ya ‘uswahilini’ ambako filamu hizo huonyeshwa kwenye mabanda yaliyosehemu za wazi na yanayofahamika na viongozi wa eneo husika.
“Hili jambo halihitaji uchunguzi wala kuundwa tume, huku kwetu uswahilini hali ni mbaya kuliko maeneo ya Mikocheni na Mbezi Beach,” alisema Chinicha.
Maoni ya Ofisa Habari wa Wilaya ya Temeke
Kwa kujibu wa Ofisa Habari wa Wilaya ya Temeke, Joyce Nsumba, wanazo taarifa za watoto kuangalia filamu za ngono kwenye mabanda mitaani kwa muda mrefu na kwamba watendaji wa mitaa ndiyo waliopewa jukumu la kusimamia mabanda hayo na kuhakikisha yanafungwa.
Nsumba alisema kuwa madiwani walilijadili tatizo hilo kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka na kukubaliana kuwa kila kiongozi wa mtaa ahakikishe mabanda hayo yanafungwa.
“Hiyo ni kero ambayo inafahamika hata madiwani walijadili, tatizo ni nguvu ya soda inatumika, tuna mpango tuwashirikishe polisi watusaidie kuwakamata wote wanaoendelea na vitendo hivyo,” alisema Nsumba.
Hata hivyo, baadhi ya watendaji katika halmashauri, ambao hawakutaka majina yao kuandikwa gazetini kwa madai kuwa wao siyo wasemaji wa halmashuri, walisema kuwa mpango wa kuyafunga mabanda ya filamu huenda usifanikiwe kwa kuwa kuna baadhi ya madiwani wanamiliki mabanda hayo.
“Wapo baadhi ya waheshimiwa madiwani ambao wamekuwa wakitutishia tunapotaka kwenda kuyafunga mabanda hayo kwa sababu nao wanamiliki mabanda,” kilisema chanjo chetu.
Kamanda Kova ahaidi kuchukua hatua
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema kuwa vitendo vinavyofanywa na wenye mabanda ya kuonyesha filamu ni kosa na havikubaliki, huku akiahidi kuwatafuta, kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika wote.
“Vitendo wanavyofanya havikubaliki, tutawajulisha makamanda wote wachukue hatua haraka,” alisema Kova.
Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Polisi bado mpo nyuma ki-teknolojia. hata mkiwazuia kuangalia porn videos, wataingia online na kuangalia. Bado serikali haijawa na uwezo wa ku-block website mbaya siyo tu maya kwa watoto, bali hata kwa usalama wa taifa. Hamna account ya twitter wala face book ambako watu wanatishiana maisha. Hamuwezi ku-monitor phone conversation za wahalifu kupitia makampuni ya simu ambayo hayalipi kodi inavyotakiwa na mnayaogopa. Polisi inabidi mjipange, teknolojia inawaacha nyuma na wananchi ndiyo wanaoumia.