Moshi. Mambo yamezidi kumwendea vibaya Mwenyekiti mstaafu wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Vicky Swai kutokana na hoteli yake yenye ghorofa moja kuuzwa kwa mnada kwa Sh600 milioni.
Hoteli hiyo iliyopo kiwanja namba 89 eneo la Shanty Town mjini Moshi inayofahamika kama Kibo Executive Lodge, iliuzwa mwishoni mwa wiki ili kufidia deni la Sh350 milioni anazodaiwa na Benki ya CRDB.
Mnada wa kuuza hoteli yake hiyo ulifanyika Jumamosi iliyopita, ukiendeshwa na Kampuni ya Madalali ya Comrade Auction Mart Co Ltd ya jijini Dar es Salaam iliyopewa idhini hiyo na Benki ya CRDB.
Kabla ya kufanyika kwa mnada huo, madalali hao walitoa matangazo katika magazeti ya Daily News na Uhuru ya Mei 17,2013, wakiujulisha umma kuwa baada ya siku 14 wangeiuza hoteli hiyo.
Kampuni ya Charan Singh and Sons Ltd kupitia kwa mwakilishi wake, Agustino Rafael Mrema ndiyo iliyotoa ofa ya juu zaidi ya Sh600 milioni ambayo haikuweza kufikiwa na mnunuzi mwingine yeyote.
Swai amekuwa mwenyekiti wa CCM Mkoa Kilimanjaro kwa vipindi viwili mfululizo (2004-2008 na 2008-2012) na kabla ya hapo,alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Jumuiya ya Wanawake (UWT).
Mwaka jana hakutetea wadhifa wake huo lakini akagombea nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia Wilaya ya Hai Mkoa Kilimanjaro, lakini kamati kuu haikurudisha jina lake.
Mumewe, marehemu Nsilo Swai alikuwa ni miongoni mwa mawaziri sita Waafrika waliounda baraza la mawaziri wakati Tanganyika inapata uhuru wake mwaka 1961 na yeye kuteuliwa Waziri wa Biashara.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment