ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 4, 2013

‘Gharama za simu sasa zimepungua asilimia 57’

Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia, January Makamba(katikati) akibadilishana mawazo na wenzake , Naibu waziri Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck ole Medeye (aliyemgusa) na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Kassim Majaliwa. Kulia ni mbunge wa Viti Maalum (CCM), mkoani Singida Martha Mlata. Picha na Emmanuel Herman.

Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imeliambia Bunge kuwa katika kipindi cha miaka mitano, gharama za kupiga simu zimepungua kwa kiasi kikubwa zaidi.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia January Makamba ambaye alisema kuwa gharama hizo zimepungua kwa simu za ndani na nje ya nchi.
Makamba alikuwa akijibu swali la Mhonga Said Ruhwanya (Viti Maalumu-Chadema) ambaye alihoji kama Serikali itakuwa tayari kutoa mchanganuo wa jinsi gharama za kupiga simu (airtime) kama zimeshuka kama ambavyo Serikali iliahidi huko nyuma.
Mbali na hilo, mbunge huyo alihoji Serikali imefikia hatua gani kwamba taasisi zote za Serikali zinaunganishwa na mkongo wa Taifa ili kuondokana na gharama za mawasiliano na akataka kujua ni lini Mikoa ya Zanzibar itaunganishwa.
Naibu Waziri alisema katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009, gharama za simu zimepungua kutoka Sh 147 kwa dakika na kuwa Sh 62 kwa dakika katika kipindi cha mwaka huu punguzo linalolingana na asilimia 57.
Alisema kuwa gharama za kupiga simu kutoka mtandao mmoja kwenda mtandao mwingine zimepungua kutoka Sh 115 mwaka 2012 kwa dakika hadi kuwa Sh 34.92 iliyoanza kutumika mwaka 2013.
Alisema hadi sasa taasisi 23 za Serikali pamoja na Makao Makuu ya mikoa 24 ya Tanzania Bara zimeunganishwa kwenye mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Kuhusu Mikoa ya Zanzibar alisema Serikali kupitia makubaliano maalumu na Serikali ya watu wa China, imesaini mkataba wa Dola 403 milioni za Marekani kwa ajili ya ujenzi wa mkongo awamu ya tatu ambao utapelekwa huko na kumalizia maeneo yaliyobaki.
Mwananchi

No comments: