Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk Charles Tizeba jana alikiri kuwa katika kipindi cha miaka mitatu kumetokea ajali kadhaa katika Mkondo wa Bahari Nungwi.
Hata hivyo alilieleza Bunge kuwa Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha vyombo vyake vinakuwa macho katika kuokoa ajali hizo pindi zinapotokea.
Alikuwa akijibu swali la Yussuf Haji Khamis (Nungwi-CUF) ambaye alitaka kujua Serikali inatoa tamko gani kuhusu ajali mbalimbali ikiwamo kuzama kwa meli na vyombo vingine katika mkondo wa Bahari ya Nungwi.
Mbunge huyo pia aliomba Serikali kutoa tamko ni lini itapeleka ndege katika eneo hilo kwa ajili ya kufuatilia vyombo vya usafiri katika kipindi cha miezi ya Juni na Julai ambapo hali ya bahari huwa ni mbaya.
Naibu Waziri alisema Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatara) imechukua na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha usalama wa usafiri baharini ili kuzuia ajali.
Alitaja baadhi ya hatua hizo ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa vyombo vya usafiri baharini zinakidhi viwango vya kutoa huduma kwa usalama kulingana na sheria, kanuni na taratibu.
“Nyingine ni kuimarisha usimamizi wa meli na vyombo vingine baharini na utoaji huduma kabla na baada ya safari kuanza ikiwamo ufuatiliaji na utunzani wa kumbukumbu,” alisema Tizeba.
Kuhusu suala la kupeleka ndege huko, alisema ni mapema kwa jambo hilo kwani kinachotakiwa ni mawasiliano na kuwa ndiyo ambayo yamekuwa yakitumiwa kuvipasha habari vikosi vya usalama, Polisi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment