ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 4, 2013

Kagame haitahamishwa Darfur - Musonye

Katibu Mkuu wa Shirikisho la
Soka la Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA),
Nicholas Musonye

Wakati serikali ya Tanzania ikisisitiza kwamba usalama ni mdogo katika mji wa Darfur ambako mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) yatafanyika mwaka huu kuanzia Juni 18 hadi Julai 2, waandaaji wa mashindano hayo wamesema jana kuwa michuano hiyo haitahamishwa.

Mabingwa watetezi Yanga na Simba inayoingia kama bingwa wa ligi wa mwaka jana wataiwakilisha Tanzania Bara, wakati Super Falcon itaiwakilisha Zanzibar.

Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Nicholas Musonye, alisisitiza kuwa kwa sasa mji huo ni salama na kwamba kabla ya kukubali mashindano hayo yafanyike Sudan, walipeleka taarifa katika Umoja wa Afrika (AU) kutaka kuthibitisha hali hiyo.


Musonye alisema kwamba CECAFA inapenda amani na kamwe haiwezi kupeleka wachezaji na viongozi sehemu isiyokuwa na usalama na kuendesha mashindano.

"Sudan ni salama, Darfur ni salama, ulinzi ni wa kutosha kwa wageni watakapotua kwenye mashindano," alisema katibu huyo wa CECAFA ambaye anatoka Kenya.

Musonye alisema kwamba anaendelea kuwasiliana na viongozi mbalimbali wa serikali ya Tanzania na Sudan ili kuliweka sawa suala hilo na kuzitaka Simba, Yanga na Super Falcon ziendelee na maandalizi ya kuwania kikombe cha mashindano hayo ya kila mwaka.

Viongozi wa Simba na Yanga kwa nyakati tofauti jana waliliambia gazeti hili kuwa wanasikiliza na watafuata maelekezo kutoka serikalini ingawa wao wanafanya kazi na Shirikisho la Soka Nchini (TFF).

Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako, alisema kuwa wao waliandika barua TFF wiki mbili zilizopita wakitaka kufahamu usalama wa Darfur lakini hawakupewa jibu lolote na sasa watasikiliza tamko litakalotolewa na serikali.

Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kwamba wanaifuata serikali na wanaamini walichokisema kimefanyiwa uchunguzi na ni kwa maslahi ya raia wake.

Katika mashindano hayo, Yanga iliyoko katika kundi C imepangiwa kucheza mechi yake ya kwanza Juni 20 dhidi ya Express ya Uganda wakati Simba iliyo katika kundi B imepangwa kuanza dhidi ya El Merreikh na zote zimepangwa kucheza katika mji wa Darfur Kaskazini.

Kundi A litacheza mechi zake katika mji wa Gordofan Kusini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: