Mazingira wanayopikia wanafamilia hao.
MAISHA ya familia ya mzee Athumani Mwenda, 80, ni ya mateso makali baada ya nyumba yao kubomolewa ikiwa na vitu ndani.
Watoto wa familia ya mzee Athumani Mwenda wakiwa wamelala nje.
Mzee huyo na familia yake sasa wamekuwa wakiishi nje huku wakikabiliwa na njaa pamoja na maradhi mbalimbali.Tukio la kuvunjiwa nyumba lilitokea Mei 24, mwaka huu katika Kitongoji cha Mvuti, Ilala, Dar na inadaiwa kuwa ubomoaji huo ulifanyika chini ya mtu aliyejitambulisha kwa jina la Boatu Msuya ambaye ni dalali wa mahakama huku akiongozana na polisi sita wenye bunduki aina ya SMG.
Akielezea tukio hilo kwa masikitiko makubwa, mzee Mwenda ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Sangara, Kata ya Msongora alikuwa na haya ya kusema:
“Sina mahala pa kwenda na hawa watoto, nani anaweza kutupa hifadhi, chakula na matibabu? Tunaishi kama wanyama porini.
Baadhi ya wanafamilia hao wakiwa wamejihifadhi katika kibanda hiki.
“Sijatendewa haki hata kidogo, ni bora wangetuua kuliko kutufanyia kitendo hiki kilichosababisha tuishi kwa dhiki. Sidhani kama kuna mahakama inayotoa amri ya kugawa ardhi yangu bila kutembelea eneo la tukio, anayedaiwa kuwa ni dalali amegawa na kuchukua eneo kubwa tofauti na tulivyopatana mahakamani.“Ni zaidi ya nusu ekari na ndiyo maana wamechukua na eneo la nyumba yangu na kuibomoa huku nikiwa nimelala ndani na wajukuu zangu, niliamshwa dakika za mwisho, nikaokolewa na wajukuu zangu, nusura tufunikwe na kifusi.
“Nilipotoka nje nilikuta kundi la vijana na askari, niliwauliza kwa nini wananibomolea nyumba, wakanijibu nikae kimya. Hakuna kiongozi yeyote wa serikali aliyekuja naye wala barua inayonitaka nihame au kubomoa nyumba.
“Ninachokijua ni kwamba tulikubaliana mahakamani kuwa nigawe nusu ekari ya ardhi yangu ninayoishi nimpe tuliyekuwa naye kwenye kesi mahakamani.
”Naamini kungekua na watendaji wa mahakama hapa au kiongozi yeyote wa serikali wa kusimamia zoezi hili haya yote yasingetokea, nimeonewa.
“Kwa sasa tunalala nje, mvua, jua na maradhi ni vyetu, nimeishi hapa tangu mwaka 1980 enzi hizo hapa likiwa pori, leo hii wameona lipo karibu na barabara ya lami wanaamua kujigawia, sikubali hata kidogo,” alisema.
Afisa Mtendaji wa kata hiyo, Omar Ali Khalfan alipoulizwa juu ya sakata hilo, alisema kwamba mzee huyo tayari ameshachukua hatua ya kuandika barua kwenda mahakama kuu na ameshaipitisha na kumgongea muhuri.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment