ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, June 4, 2013

Rasimu yamiminiwa sifa

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba,
Deus Kibamba

Rasimu ya Katiba mpya iliyozinduliwa jana jijini Dar es Salaam imepokelewa kwa furaha kubwa na viongozi, wanasiasa na wanaharakati ambao wameimiminia sifa kwa kusema maoni yaliyotolewa na wananchi hayakuchakachuliwa badala yake yamechukuliwa kama yalivyotolewa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba, alisema rasimu hiyo iliyosomwa na Jaji Warioba imejibu kiu ya muda mrefu ya Watanzania.

Kibamba alisema maoni yaliyotolewa na Watanzania kwa Tume ya Mbadiliko ya Katiba hayakuchakachuliwa na kwamba alichofanya Warioba ndicho walichotarajia wananchi wengi.

“Kwa kweli nimefurahi sana kuona maoni ya wananchi wengi yamo katika rasimu mpya ya katiba na Warioba amefanya kazi yake vizuri kama tulivyotarajia, ingawa hiyo sio mwisho, lakini ni mwanzo mzuri,'” alisema Kibamba.


Kibamba ambaye amekuwa akikosoa mara kwa mara mchakato mzima wa kupata katiba mpya tofauti na siku zote, jana alionekana kuridhika na kilichotangazwa na Jaji Warioba baada ya kumsikiliza kupitia Luninga na kumpongeza kwa kazi nzuri aliyoifanya na timu yake.

Kibamba aliahidi kuwa ataunda timu ya watalaamu kuchambua rasimu hiyo na kisha kutoa maoni yao zaidi juu ya kilichomo na kuwataka Watanzania waijadili bila jazba, vurugu wala fujo ili mwisho wa siku Tanzania ipate katiba nzuri.

Mhadhiri     Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Benson Bana, alisema rasimu ni nzuri na imekidhi matakwa ya wananchi wengi.

Alitolea mfano pendekezo la kuundwa kwa serikali tatu ambalo alisema Chama Cha Wananchi (CUF) kilikuwa kikilipigia kelele jambo hilo na kuongeza kwamba majibu yamepatikana kwa pande zote.

“Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanazibar, Maalim Seif Sharif Hamad na wenzake wamepata majibu sahihi juu ya kile walichokuwa wanadai kwa muda mrefu katika muundo wa Muungano,” alisema Dk. Bana.

Mbunge wa Lindi Mjini (CUF), Salum Barwany, ambaye ni mwenye ulemavu wa ngozi, alisema rasimu imewatambua na kuwajali walemavu kwa kupendekeza nafasi za rais kuteua wabunge wenye ulemavu.

Alisema hatua hiyo ni nzuri na kuvitaka vyama vya watu wenye ulemavu kuitumia vizuri fursa hiyo katika kupendekeza majina ili kusiwe na mgogoro ambao unaweza kuibuka kugombea nafasi hizo.

Kuhusu mbunge kuwa na ukomo baada ya kushikilia nafasi hiyo kwa vipindi vitatu yaani miaka 15, Barwany alisema ana amini wabunge watakapoijadili wanaweza kupunguza muda huo na kuwa miaka 10.

Alisisitiza kuwa rasimu ni nzuri na imejaribu kugusa makundi yote ya jamii na kwamba wananchi wanatakiwa kuiunga mkono ili ipitishwe.

Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) na Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustino Mrema, alisema anaunga mkono rasimu hiyo kwa sababu imechukua maoni yaliyotolewa na wananchi.

Alisema uamuzi huo utakuwa umepeleka kilio kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa baadhi ya mambo yaliyoelezwa humo yatakifanya kishindwe kuibuka na ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Mwenyekiti wa Chama cha APPT-Maendeleo, Peter Mziray, alisema ni wazi kuwa rasimu hiyo imefurahiwa na Watanzania wengi kwa sababu malalamiko yaliyokuwa yakitolewa kwa muda mrefu sasa yamesikilizwa.

Alisema suala la serikali tatu kuwapo katika rasimu ni muhimu kwa kuwa limejibu maswali mengi yaliyokuwa yakiulizwa na wadau mbalimbali wakiwamo wanasiasa na wananchi wa kawaida.

Mwenyekiti wa Chama Cha Kijamii (CCK), Constantine Akitanda, alisema kuna maeneo ndani ya rasimu ya Katiba mpya yanatakiwa yafanyiwe kazi, likiwamo linalohusu rasimu hiyo kuendelea kumpa Rais mamlaka ya kumteua Jaji Mkuu na Naibu wake.

Alisema jambo lingine linalotakiwa lifanyiwe kazi, linahusu pia rasimu hiyo kumpa Rais mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi, Makamu wake na wajumbe wengine wa tume hiyo.

Alisema badala ya Rais kuachiwa kuteua Jaji Mkuu na Naibu wake, kuwapo na kamati maalum kwenye Mahakama, ambayo itakuwa ikipendekeza kupatika kwa viongozi hao wa Mahakama kama ilivyo kwa jeshi.

Pia alisema haungi mkono Rais kupewa mamlaka ya kuteua Mwenyekiti, Makamu wake na wajumbe wengine wa Tume wa Huru ya Uchaguzi kwa kuwa jambo hilo limeshaonekana kuwa na matatizo huko nyuma.

Naye Kaimu Mwenyekiti Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, alisema rasimu ya Katiba Mpya imegusa maeneo mengi, ambayo ni kero kwa Watanzania wa pande zote mbili za Muungano.

“Tukiunda Katiba mpya bila jazba tunaweza kuleta maendeleo,” alisema Makunga.

Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu Tanzania (Shiviwata), Amon Anastanzia, alisema wamefurahishwa na rasimu hiyo kwa kuwa imempa nafasi Mtanzania mwenye ulemavu kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi na kuondoa hali ya kutengwa kama  kwenye Katiba iliyopo.

Alisema iwapo rasimu hiyo itakuwa Katiba kamili, italeta utu, usawa na haki za kila Mtanzania bila kujali itikadi, dini na hali zao.

Naye, Katibu Mkuu wa National Leaque for Democracy (NLD), Dk. Emmanuel Makaidi, alisema suala la ardhi halijatajwa katika mambo makuu na kwamba ni suala ambalo ni tatizo kubwa kwa sasa na Katiba ingetoa jibu.

Alisema suala la kuwa na wabunge 75 kwenye Bunge la Muungano halijaridhisha kwa kuwa uwakilishi wa wananchi utakuwa mdogo.

Isack Cheyo, Kaimu Katibu Mkuu  wa United Democratic Party (UDP), alisema rasimu hiyo ni nzuri na itawaleta Watanzania pamoja na kuishi kwa misingi ya haki, kuheshimiana na kunufaika na rasilimali za Taifa.

Imeandikwa na Richard Makore,Thobias Mwanakatwe, Muhibu Said na Salome Kitomari.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: