Chanzo cha vurugu kuhusu gesi zilizotokea hivi karibuni mkoani Mtwara, kinaelezwa kuwa ni vuguvugu la kisiasa lililowaingia wananchi kiasi cha kujenga chuki kubwa dhidi ya Serikali baada ya kupata mahubiri ya wanasiasa.
Inaelezwa kuwa mzozo huo ulianza rasmi mwaka jana baada ya Serikali kuituma kamati ya kuratibu Maoni ya Sera ya Gesi ambayo ilifika mkoani Mtwara, Novemba 16, mwaka jana kukusanya maoni ya wananchi.
Katika mikutano yake mjini Mtwara, inaelezwa kuwa wananchi wengi hawakukubaliana na wazo la kusafirisha gesi kwenda nje ya Mtwara kwa njia ya bomba.
Hali hiyo ndiyo iliyowafanya viongozi wa vyama vya NCCR-Mageuzi, TLP, UDP, ADC, DP, APPT Maendeleo, Sau na Chauma, kuungana na kuhamasisha wananchi kuhusu suala hilo.
Inaelezwa kuwa hilo lilifanyika Desemba 6, mwaka jana.
Katibu Mkuu wa Muungano huo, Selemani Litope ,alisema mikutano kati ya viongozi wa vyama hivyo na wananchi ilianza Desemba 12. Mikutano hiyo iliyopewa vibali na Jeshi la Polisi ilifanyika Desemba 12, 16, 19 na 22 na Desemba 27 yalifanyika maandamano makubwa.
“Tuliona kuna malalamiko mengi ya wananchi kuhusu suala gesi kusafirishwa kwenda Dar es Salaam, tukaona tuungane ili tufikishe kilio cha wananchi serikalini, kwa sababu tunaamini kwamba, kuisafirisha gesi hiyo ni kuwanyima wananchi fursa ya kufaidika,” alisema Litope.
Alisema katika maandamano yaliyofanyika Desemba 27, Litope alisema walimwandikia Mkuu wa Mkoa huo, Kanali Mstaafu Joseph Simbakalia ombi la kutaka ayapokee lakini akakataa na kuwaita kuwa ni wapuuzi, jambo lililozidisha chuki ya wananchi.
“Kitendo cha mkuu wa mkoa kutuita wapuuzi ,kimeibua chuki kubwa miongoni mwa wananchi, hata hivyo maandamano yetu yalifanikiwa kwa sababu watu wengi walihudhuria na tukafanya mkutano katika Uwanja wa Mashujaa,” alisema.
Hata hivyo, Simbakalia alishaomba radhi kwa kauli yake hiyo Januari mwaka huu kupitia kikao cha majumuisho cha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Nani anayetuma vipeperushi na meseji?
Kabla ya vurugu zilizotokea Mei 22 mwaka huu, kulikuwa na vipeperushi na ujumbe wa simu uliosambazwa mjini Mtwara.
Moja ya waraka uliosambazwa Mei 17, ulisomeka: “Kusini zinduka, tuungane pamoja, maana dhamira ya Serikali haieleweki kwa mikoa ya kusini kama mnavyoona.Wote kwa pamoja saa 3.00 asubuhi ya Mei 17, 2013 tusikilize bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni, ili kujua mustakabali mzima wa gesi yetu na ili kuonyesha kilio/msimamo wetu kwa Serikali wa kutaka maendeleo kwa mikoa ya kusini.
Siku hiyo huduma zote za kijamii zisimamishwe ikiwa na maana ya maduka, masoko, daladala, pikipiki n.k ili iwe ujumbe kwa Serikali, maana JK ameamua kutumia nguvu nasi inabidi tupambane naye,” ulisomeka ujumbe huo.
Wakati Jeshi la Polisi likidai kuwakamata watu wawili wanaohusika kusambaza ujumbe wa simu, chanzo cha habari kimeeleza kuwa vipeperushi hivyo huchapishwa mjini Mtwara kwa siri kubwa.
“Hivi vipeperushi vinatengenezwa hapa hapa kwa siri kubwa ila hilo la ujumbe inategemea, mtu anaweza tu kuandika na kuitupa line ya simu. Lengo ni kuhakikisha kuwa mradi wa gesi unakwama kwa njia yoyote,” kilisema chanzo chetu kwa sharti la kutotajwa jina.
Chanzo hicho kilibainisha kuwepo kwa mkakati wa kuisambaratisha kabisa CCM mkoani Mtwara.
“Kwa sasa kuna kadi zaidi ya 6,000 ambazo zinapangwa kurudishwa CCM, hatukitaki tena chama hiki Mtwara.Tunafikiria chama kingine cha kutuongoza,” kilisema chanzo hicho mjini Mtwara.
Akizungumza kwa njia ya simu, Makamu Mwenyekiti wa umoja wa vyama hivyo, Abdallah Uledi, alisema wanaotuma vipeperushi na meseji ni wananchi wasiokubaliana na mradi huo.
“Siwezi kujua meseji na vipeperushi vinatumwa na nani, lakini najua kuwa kila namba ya simu imesajiliwa, kwa nini Serikali isifuatilie?” alihoji Uledi a kuongeza:
“Tangu mchakato umeanza Serikali imewahoji viongozi wa siasa, viongozi wa dini, vijana na wazee na wote wameonyesha nia ya kupinga gesi. Hili ni suala la wananchi wote wa Mtwara, siyo wanasiasa peke yake.”
Aliilaumu Serikali kwa kutotoa elimu ya kutosha kwa wananchi na kwamba matokeo yake ni vurugu.
Kwa upande wake, Fatma Sinani wa NCCR-Mageuzi, amesema ujumbe huo ni dalili kuwa wananchi wamehamasika na elimu ya uraia waliyoitoa.
“Kabla ya kuanzishwa kwa umoja wetu, Serikali ilituma Kamati ya Nishati na Madini kupata maoni ya wananchi. Kamati hiyo ndiyo ilituelekeza tutoe elimu kwa wananchi na sisi baada ya kulitafakari suala hilo tukashtukia mradi huo. Siyo kwamba tumemwaga sumu kwa wananchi, ila unachokiona sasa ni ukweli uliowaingia wananchi ndiyo maana hawakubali gesi kusafirishwa.”
Umaskini na ubabe wa Jeshi la Polisi
Licha ya nia njema ya Serikali kutuliza vurugu kwa majeshi ya ulinzi na usalama, Jeshi la Polisi limeelezwa kutumia nguvu kubwa kupita kiasi ma hivyo kupoteza imani ya wananchi.
Hali hiyo imejidhihirisha kwa wananchi kuchoma nyumba za polisi na taasisi za Serikali na CCM, ili kuonyesha hisia zao.
Kwa upande mwingine, wengi wamekata tamaa kutokana na umaskini wa muda mrefu.
“Polisi tuliotegemea ndiyo wametutesa, wamechoma nyumba zetu, wameua tunazika mtu aliyepigwa risasi. Tunanyanyaswa ndani ya nchi yetu, twende wapi?” alihoji Abdallah Salum wa Mikindani.
Naye Said Rashid wa Mikindani amelalamikia umaskini: “Hapa hatuna chochote cha kutegemea, samaki tuliokuwa tukivua wametukataza wakisema tunavua kwenye hifadhi ya bahari. Hatuna uwezo wa kununua mitumbwi ya kuvua kina kirefu. Gesi ndiyo hiyo inasafirishwa kwenda Dar es Salaam,” aliongeza.
Serikali inakimbia kivuli chake?
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina, mfanyabiashara wa Soko Kuu la mjini Mtwara, alisema Serikali ndiyo imeasisi vurugu hizo kwa kuruhusu mikutano na maandamano ya wanasiasa.
“Wanasiasa walipoungana na kuanza kufanya mikutano, walipata vibali vya polisi na hata maandamano yalipofanyika, waliruhusiwa.Leo mambo yamevurugika ndiyo wanaanza kutafuta mchawi.Ndiyo maana kabla ya vurugu za sasa hawakuwahi kukamata mtu,” alisema.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa, Joseph Simbakalia alisema kuwa baada ya maandamano ya Desemba 27, waliwahoji makundi ya watu, lakini hakuna aliyeshikiliwa.
“Tangu vurugu hizo zimeanza Desemba, 2012 tuliwahoji watu kadhaa, ila sina uhakika wangapi,” alisema Simbakalia na kuongeza:
“Hizi ni hujuma na wala hazina uhusiano na suala la gesi. Kama tusingekuwa makini, walitaka kuvunja Daraja la Mikindani, wakataka tena kuvunja Daraja la Mpapura, huko Lindi palikuwa giza tupu, baada ya watu hao kutumia misumeno ya umeme na kukata nguzo za umeme. Walitaka hata kuhujumu Hospitali ya Ligula. Hayo yote yana uhusiano gani na gesi?”
Mlolongo wa matukio.
Muungano wa vyama tisa ulipoasisiwa Desemba 6, 2012, umefanya mikutano minne yaani Desemba 12, 16, 19 na 22 kabla ya kufanya maandamano yaliyoishia Uwanja wa Mashujaa, Desemba 27.
Maandamano hayo licha ya kutopokelewa na mkuu wa mkoa huo, yalipata kibali cha polisi na kuhudhuriwa na watu wengi.
Maandamano hayo yalifuatiwa na vurugu zilizotokea wilayani Masasi Januari 26, 2013.
Chanzo cha vurugu za mkoani Mtwara imeelezwa kuwa ni askari wanaozunguka mjini na pikipiki maarufu kwa jina la Tigo, baada ya kumkamata dereva wa pikipiki na kuanza kumpiga.
Madereva wenzake walipoona tukio la mwenzao kupigwa, waliingilia kati mzozo huo na kumtoa mwenzao kwenye kadhia.
Baada ya kumtoa mwenzao, madereva wa bodaboda waliandamana hadi kituo cha polisi wilayani humo ili kueleza hisia zao lakini walipofika, polisi walianza kuwafyatulia mabomu ya kutoa machozi yalioibua hasira za wananchi.
Vurugu hizo zilisababisha majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.
Kutokana na vurugu hizo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alikwenda mkoani Mtwara kutuliza hali ya mambo.
Akizungumza katika mkutano wa majumuisho uliofanyika mjini Mtwara baada ya kusikiliza madai ya wananchi hao kwa siku mbili mfululizo, Pinda alisema hakuna tone la gesi ghafi itakayosafirishwa kwa njia ya bomba na kwamba kiwanda cha kusindika gesi ghafi kitajengwa katika Kijiji cha Madimba, mkoani humo ili mabaki yatokanayo na gesi yatumike kuvutia uwekezaji wa viwanda.
Mbali na Waziri Mkuu, Pinda mawaziri wengine waliokwenda Mtwara ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
Baada ya hapo mikutano ya uhamasishaji ya muungano wa vyama tisa ikasitishwa.
Hata hivyo, viongozi wa muungano huo, wanasema hawakuridhishwa na majumuisho hayo kama anavyoeleza Makamu Mwenyekiti wa Mkoa wa Mtwara wa NCCR-Mageuzi, Mohamed Salim:
“Tulimfuata Waziri Mkuu Pinda huko Dar es Salaam tukiwa na hoja tatu, kwanza turuhusiwe kuendelea na mikutano ili tutoe elimu, pili; Mkuu wa Mkoa, Simbakalia aondolewe na tatu, aje Waziri wa Nishati na Madini ili tuzungumze naye kwa sababu tangu vuguvugu hili lianze hajawahi kufika huku,” alisema Salim.
Hata hivyo, alisema, Waziri Mkuu atalifikisha suala la Mkuu wa Mkoa kwa Rais Jakaya Kikwete na kuhusu mikutano atawasiliana na Waziri Nchimbi na Waziri wa Nishati wa Madini kuhusu kutembelea Mtwara.
“Hayo yote hayajawahi kutekelezwa na ndiyo kiini cha vurugu za sasa, kwani wananchi hawajaridhishwa na ahadi za Serikali,” alisema Salim.
Mwananchi
1 comment:
vyovyote iwavyo hayo ni matokeo ya kushindwa kiuongozi kwa viongozi walio madarakani. siasa maana yake ni busara, viongizi wetu hawana maadili, uadilifu na busara kuweza kuwafahamisha wananchi wao na ndio hata maadui kutoka nje ya nchi yetu wanaweza kwa urahisi kuwarubuni wananchi waharibu nchi. kuna mifano mingi ya sera, mikataba na tabia ya uendeshaji nchi kwa usiri mkubwa kiasi ambacho matokeo yamejionesha ni kwa sababu za ulafi na ubinafsi wa hao walio madarakani waweze kujinufaisha kimapato. kuongoza si kutawala, kwa nini usiweke wazi mambo unaogopa nini kama huna agenda za siri ambazo ndizo zimeifikisha Tanzania hapa ilipo baada ya nusu karne ya uhuru bado ni omba omba tu. nchi haiwezi hata kukusanya mapato yake yenyewe na kugharimia bajeti yake. viongozi wetu tunawapa sifa nyingi kwa kuwa na utaalam wa kuomba wanapokwenda katika mikutano ya kimataifa. safari za nje haziishi na zinamaliza fedha tu. kuna nchi nyingi tu duniani wala huwaoni viongozi wao kusafiri safari na kuimarisha ufakhari na zinajiendesha vizuri tu. unaowaongoza wapo hapa Tanzania tena Europe na US mnakwenda kufanya nini kama si ufakhari usio wa lazima. pengine wako sawa kiongozi wa omba omba lazima avae suti na tai na aendeshe benz ili aonekane wa maana mbele ya mabwana wa kutoa misaada. sisi tulioko huku nje tunawaona viongozi wetu wakija na kile wanachofanya. Tanzania inahitaji mabadiliko makubwa ya culture ya viongozi na uwanasiasa kwani hata kama CCM itashindwa hao wengine nao wakiwa na culture hii hii basi mambo ndo hayo hayo. same horse different saddle.
Post a Comment