ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 23, 2013

MAISHA NDIVYO YALIVYO: Mke wa ndoa ana mwanaume nje na wazazi wake wanajua…!

Na. Flora Wingia
Mpenzi msomaji, leo ninalo jambo jingine ningependa tulijadili kwa pamoja. Mwishoni nitadokeza kidogo kuhusiana na mada ya wiki iliyopita.
Lipo jambo amenidokeza msomaji wetu mzuri huku akiishia kuomba ushauri utakaosaidia kuepusha balaa. Hebu sikia ujumbe wake kupitia simu yangu ya mkononi wiki hii;

“Dada Flora, leo nina kisa cha mke mwenye bwana nje ya ndoa na wazazi pamoja na nduguze wanafahamu fika.
Huyu mke ana mumewe na watoto, lakini cha kushangaza mama huyu ana mwanaume ambaye mawasiliano yao hufanyikia kwao na mwanaume huyo ndiye anayetoa mahitaji ya kila siku.

Watoto wanamfahamu kama baba wa mtoto wa mama yao mkubwa! Mimi binafsi inaniuma sana. Naomba ushauri ni jinsi gani tumbadilishe mke huyu aache hiyo tabia(Rama wa DSM).
Ujumbe huu umebeba dhana nzito ya uaminifu. Dhana hii pia ilitawala mada ya wiki iliyopita pale jamaa aliporejea na kukuta mkewe akiwa ana mimba ya mwezi mmoja na nusu. Na hii ni baada ya kumpima kabla ya kukutana naye kimwili. Akanyamaza. Mbio akaenda kumchukua mtoto wake aliyezaa na mwanamke mwingine kabla ya kumuoa huyu mwenye mimba.
Kuona mtoto akaanza kumnyanyasa, jamaa akagundua akampeleka kwa mama yake mzazi. Sasa anasubiri mimba hiyo ikue bila hata kumgusa ili ukweli ubainike kuwa mimba ni ya nani. Uaminifu umetoweka ndani ya familia zetu.

Msomaji aliyetuma ujumbe kuhusu kituko hicho cha mimba nilimjibu ifuatavyo; Huyo ameshanaswa mtegoni na kama wana ndoa iko shakani. Kwa sasa kutoa hawezi kwani mume ameshaigundua.

Mume yuko kimya pengine akingojea mama aseme ana mimba. Angejua angetoa, vinginevyo ajiandae kwenda kwa aliyempa mimba hiyo. Kwa kifupi hakuwa mwaminifu wala subira, hivyo mume huyo atamkosa. Naam. Mpenzi msomaji, angalia tena kwenye ujumbe wa hapo juu jinsi ambavyo baadhi ya wanawake wamejikita katika kuwavunjia uaminifu waume zao japo wanaishi mjengo mmoja. Wanalala na kuamkia kitanda kimoja, chumba kimoja lakini wakishatoka milangoni kwenda nje, kila mtu na lwake. Watu wanaponea wapi?

Ati mwanamama ana mwanaume wa nje, ambaye wazazi wake na ndugu wanamfahamu na mawasiliano ya wawili hawa hufanyikia kwa wazazi wa mwanaume. Ni kituko gani hiki? Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo. Nasema hivi kwa sababu usaliti huo umewezekana na ajabu nyingine ni kuwa wahusika wote wanaona ni jambo la kawaida kabisa.

Yapo maswali kama mawili hivi ya kujiuliza hapa; Je, mama huyu aliyejenga mahusiano nje ya ndoa anampenda na kumjali kweli mumewe? Na je, hawa wazazi wanaokubaliana na binti yao kuwa na mahusiano na mwanaume mwingine tena nyumbani kwao kama eneo la kukutania huku angali na mumewe wanatenda haki?

Lakini pamoja na maswali hayo, nikitizama kwa undani nahisi kwamba huenda yule bwana wa nje anamridhisha bibie huyu katika mahitaji yake pamoja na wazazi wake. Na ndiyo maana anawahusisha wazazi wake ambao wao wanaona wanafaidi vinono toka kwa mwanaume huyu wa nje kuliko kwa yule mkwe(mume wa binti yao).

Lakini siku za mwizi ni arobaini. Ipo siku mambo yatafumuka na kuwa hadharani. Na arobaini hiyo haiko mbali . Msomaji aliyenitumia ujumbe huo hapo juu ameweka wazi kuwa roho inamuuma kwa kitendo anachofanya bibie. Akaomba ushauri jinsi bibie atakavyoweza kuachana na tabia hiyo.

Mimi ujumbe huo nilimjibu nikamwambia yafuatayo, “huyo mke mwenye mwanaume nje ya ndoa ni mjanja na kazoea ndiyo maana mawasiliano anafanyia kwa wazazi wake ili wamkingie kifua. Hata bomu likilipuka arudi kwao. Ila mumewe anaweza kumfuatilia kama anazo fununu. Za mwizi ni arobaini atanaswa tu.”

Huyu msomaji wetu aliyeamua kutoa dukuduku hilo kupitia safu hii na kusisitiza inamuuma, anaweza kulizungumzia hilo hata kwa marafiki zake na mwisho wa siku taarifa zikasambaa na kumfikia jamaa mwenye mke anayesaliti ndoa yake.

Tabia hizi za kuwa na wanaume au wanawake wa pembezoni huku wale wa ndani(wenye miji) ama wako gizani hawajui kinachoendelea au wanajua ila wanaumia rohoni, zilemeta misukosuko na mipasuko mingi katika nyingi ya familia zetu.

Hata haya maambukizi ya virusi vya ukimwi katika nyingi ya familia yamesambazwa kwa njia hii ya watu kutoka ovyo nje ya ndoa. Matokeo yake watoto wanabaki yatima baada ya wazazi kupoteza maisha kwa ukimwi.

Kwa mfano, mwanamama huyo anayekutana na mwanaume mwingine kwa wazazi wake anaweza kabisa kuzoa gonjwa hilo huko nje na kumletea mumewe. Ikitokea hivyo atamlaumu nani?

Na mume huyu anayefanyiwa vitimbwi na mkewe, akigundua itatokea nini? Wengine huwa wanagundua nyendo za wake zao, badala ya kuuliza ili kudhibiti tabia hiyo, wao ndiyo kwanza wanafyatuka na kutafuta pa kujiliwaza huko nje.

Matokeo yake ni kwamba mama anatoka kujinafasi anga za mbali na baba naye anatafuta sababu ya roho kwingine. Mwisho wa siku kila mmoja anajiona mshindi kumbe ni maangamizi yasiyokuwa na mshindi. Maisha Ndivyo Yalivyo, lakini kumbuka ile hadithi ya mbayuwayu anakwambia akili ni zako lakini waweza kuzichanganya na za mwenzio ukapata jawabu.

No comments: