
FUNDISHO
Unaruhusiwa kukosea kwenye mapenzi lakini ni dhambi kuendelea kusimama pale ulipokosea. Busara iliyopo upande wako ni kwamba unapaswa kufanya masahihisho kila unapobaini umekwenda mrama. Wewe siyo malaika, kwa hiyo udhaifu wako lazima uukubali, hivyo basi, kujikosoa ni muhimu na lazima.
Romeo aligundua makosa yake, akajisahihisha. Uzuri ni kwamba Mungu alikuwa upande wake, kwa hiyo alimlindia penzi lake kwa Shantale. Hivi sasa anafurahia maisha bora kabisa ya kimapenzi kwa sababu yupo na mwanamke mwenye mapenzi ya dhati. Mwanamke ambaye alimjali akiwa hana kitu na anaendelea kumthamini kwa hali zote.
Mapenzi ni upofu kwa sababu kuna wazee wengi wanachemka licha ya umri wao kuonesha upo alasiri. Wanavuruga nyumba kutokana kudatishwa na penzi la nje, kwa hiyo usiseme Romeo alimsaliti Shantale kwa ujana wake, la hasha! Yana nguvu ya ajabu sana, muhimu ni kuzungumza na moyo wako ili usipotoshwe na tamaa za macho, vilevile unapokosea, jisahihishe haraka ulinde penzi lako.
Mfalme Daud ni mtu wa Mungu, alipomwona Bathsheba (mwana wa kike wa kiapo) ambaye alikuwa mke wa askari wake, Uriah, alimtamani. Hata alipojua kwamba yule ni mke wa mtu, tena mmiliki mwenyewe ni askari wake aliye vitani, aliamuru auawe ili apate nafasi ya kummiliki jumla mrembo huyo (Bathsheba).
Daud aliyaona makosa yake ndiyo maana baadaye alitubu. Hii inamaanisha kwamba kukosea kimapenzi inaweza kumtokea mtu yeyote. Tamaa za macho na upofu wa kutojua mandhari ya kesho yalivyo ni sababu ya wengi wetu kuanguka dhambini na kusaliti. Jisahihishe kama Romeo, maana Romeo ni njia ya Daud.
Kwa Shantale, hivi sasa anafurahia mapenzi yenye ubora wa hali ya juu kabisa. Yale mambo ambayo aliyafanya nyuma kwa ajili ya Romeo, matunda yake anayavuna leo. Uvumilivu wake umemuwezesha kula mbivu ambazo siku za nyuma aliziota. Romeo, anamjali, anamthamini na anamheshimu kuliko mwanamke yeyote chini ya jua.
Kila anachotaka anapewa. Miaka ya nyuma yeye ndiye alikuwa mnunua zawadi lakini hivi sasa ananunuliwa vitu mpaka anajaza makabati na ‘dressing table’. Kwa kifupi, Romeo anampa Shantale matunzo kama malkia. Shantale ni mwenye furaha kwa sababu anafanyiwa mambo hayo na mwanaume anayempenda kuliko kitu chochote.
Elimu tunayoipata hapa ni kwamba wakati mwingine hatutakiwi kuchoka pale wenzi wetu wanapopotoka. Tuwavumilie na tujitahidi kuzungumza nao mpaka watakapobadilika. Kama Shantale asingevumilia, leo hii asingekuwa anafurahia mapenzi bora kutoka kwa Romeo.
SOMO LA JUU KABISA
Siyo kila unayempenda anaweza kuwa mwenzi wako wa maisha. Romeo aliwekeza nguvu nyingi kwa Jannine akijua ni zawadi, unyenyekevu na uhusika wake wa kiungwana, vinaweza kumfanya mwanamke huyo abadilike na kuonesha mapenzi. Haikuwa hivyo, aliteseka mpaka akaamua kuyanawa jumlajumla.
Ona sasa, wakati Romeo anateseka kwenye mapenzi ya Jannine, Shantale naye alikuwa mtu wa kulia, akiwaza jinsi anavyoweza kumfanya Romeo amwelewe ili mapenzi yao yawe na sura inayoeleweka. Kuna kipindi alishajitahidi kuwa na mwanaume mwingine lakini ilishindikana. Moyo wake ulimpenda sana Romeo.
Kitu ambacho Romeo hakuwa akikijua ni kuwa Jannine alishindwa kutulia kwake licha ya kupata mapenzi yenye thamani kubwa kwa sababu naye moyo wake ulikuwa kwa mwanaume mwingine ambaye alikuwa akimtesa. Yule mwanaume hakuhusika ipasavyo kwenye mapenzi na Jannine ndiyo maana mrembo huyo akaona awe na Romeo.
Kutokana na ukweli kwamba aliamua kuwa na Romeo si kwa mapenzi ya dhati, bali kwa kutapatapa baada ya kuteswa na mwenzi wake ambaye alikuwa haeleweki, alishindwa kuonesha mapenzi. Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment