ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, June 26, 2013

Sala zetu kwa Mzee Madiba

Johannesburg. Familia ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela imesema haitaruhusu kusitishwa kwa matibabu anayoendelea kuyapata na kwamba itaendelea kufanya juhudi za kurefusha uhai wake hadi Mungu atakapoamua kumchukua.

Kauli hiyo ilitolewa jana na mwanawe mkubwa, Makaziwe Mandela huku kukiwa na taarifa kwamba kiongozi huyo hajitambui na anasaidiwa kuendelea kuishi kwa mashine tangu alipofikishwa hospitalini huko Pretoria wiki mbili zilizopita.

Alisema kwamba familia haiwezi kuacha kumhudumia kwa shinikizo la watu wa pembeni wanaodai kwamba inatakiwa imruhusu akapumzike kwa amani na kwamba kwa mujibu wa mila za Wathembu, watafanya hivyo endapo tu mhusika mwenyewe (Madiba), atakapotamka.Juzi, kwa mara ya kwanza, Rais Jacob Zuma alikiri hadharani kwamba hali ya shujaa huyo wa Afrika Kusini ni mbaya na anahitaji maombezi. Alisema hayo baada ya kumtembelea na kuzungumza na mkewe, Graca Machel-Mandela.

Hata hivyo, taarifa zilieleza kwamba hajaweza kuzungumza tangu alipofikishwa hospitali, bali alifungua macho kwa shida mara kadhaa.

Mandela anayesumbuliwa na maradhi ya homa ya mapafu alifikishwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo ya Medi-Clinic, Pretoria Juni 8 na tangu wakati huo, taarifa zimeeleza kwamba hajaweza kuzungumza lolote.

Taarifa zikieleza kwamba hali yake ilizidi kuwa mbaya Jumapili iliyopita na baadhi ya wanafamilia tayari wameshatangulia kijijini kwake, Qunu.

Gazeti la Mail&Guardian la Afrika Kusini lilieleza jana kwamba wanafamilia hao walifanya kikao maalumu nyumbani kwa Mandela, kisha kutembelea na kufanya ukaguzi katika eneo la makaburi ya familia, sehemu ambayo kiongozi huyo pia anaweza kuzikwa.

Makaburi hayo yako jirani na nyumba ya mdogo wake, Morris na haikuwekwa wazi kuhusu uamuzi wa wanafamilia hao kufika eneo hilo la makaburi, lakini kwa mujibu wa mila na desturi za watu wa Kabila la Xosa, familia hutembelea eneo hilo wanapobaini kwamba mmoja wa wanafamilia yuko mbioni kuungana na waliotangulia mbele za haki, au kuomba sala maalumu kwa ajili ya kupata ridhaa ya kurefusha maisha ya mhusika.

Pamoja na mkutano huo, wanafamilia hao walifanya mazungumzo na machifu wa eneo hilo, wakiongozwa na Chifu Bhovulengwe wa Baraza la Kifalme la Abathembu.

Wanafamilia waliofika na kuhudhuria kikao hicho cha jana ni pamoja na mkewe wa zamani, Winnie Madikizela-Mandela na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala, Lindiwe Sisulu pamoja na Kiongozi wa Chama cha United Democratic Movement, Bantu Holomisa.

Iliarifiwa kwamba kikao hicho kilifanyika kutokana na simu ya dharura iliyopigwa kwa wanandugu na wanawe, Mandla, Thanduxolo, Ndaba na Ndileka Mandela ambao tayari walishawasili kijijini hapo tangu Jumapili na kujumuika na wanafamilia wengine.

Mmoja wa wanafamilia Napilisi Mandela alisema mkutano huo uliitishwa ili kujadili ‘masuala muhimu na magumu’ kuhusiana na afya ya Mandela.

Napilisia amekuwa ndiye kiongozi wa vikao vya familia ya Mandela na ndiye anayeongoza matambiko yote ya kimila.

Wasusa kwenda hospitali
Hadi jana mchana, taarifa zilieleza kwamba hakukuwa na wanafamilia waliokuwa wakifika hospitalini hapo tofauti na siku zilizopita ambapo wakati wote walikuwa wakionekana kwenye maeneo hayo.

Ni siku ya 18 tangu alipolazwa na siku ya nne tangu ilipoelezwa kwamba hali yake imekuwa mbaya zaidi kutokana na kutokuweza si kuzungumza tu, bali hata kufungua macho.

Njiwa weupe
Wafugaji wawili wa Johannesburg walijitokeza na kurusha njiwa weupe 100 nje ya hospitali alikolazwa shujaa huyo ikiwa ni ishara ya kuliombea amani taifa iwapo atafariki dunia.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Thomas Coutts alikaririwa akisema njiwa hao pia ni ishara ya kutambua na kukubali mchango mkubwa wa Mandela kwa taifa hilo.
Mwananchi

No comments: