NIANZE kwa kumshukuru Mungu kwa yale ambayo amekuwa akinitendea katika kila siku ya maisha yangu. Afya yangu pamoja na familia yangu ni kielelezo tosha kwamba anatupenda na ndiyo maana ametufanya tuwe kati ya wale wanaoendelea kuivuta hewa yake safi hadi leo bila malipo yoyote.
Lakini pia nimshukuru kwa kunijaalia watu nyuma yangu, watu ambao wamekuwa wakinielekeza pale ambapo nimekuwa nikikosea na kunipongeza pale ambapo nimefanya vizuri. Hilo ni jambo jema na nimuombe tu Mwenyezi Mungu anijaalie kila la kheri na aniondoshee kila la shari.
Ndugu zangu, hakuna anayeweza kubisha kwamba mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu. Lakini pia mapenzi hayahaya yamekuwa yakisababisha matatizo makubwa kwa baadhi ya watu. Utakubaliana na mimi kwamba huko mtaani kuna ambao wamekatisha maisha yao kwa sababu ya mapenzi.
Wapo watu huko kwenye maeneo yetu ya kazi na mtaani kwetu ambao wanashindwa kufanya shughuli zao kwa ufanisi na ukiuliza aidha utaambiwa wameachwa na mpenzi wao au wamekataliwa uchumba na watu waliotokea kuwapenda.
Naomba niseme tu kwamba, mapenzi usipoyajulia yanaweza kukutoa uhai au kukufanya ukachanganyikiwa lakini utakuwa ni mtu wa ajabu sana kama utadiriki kunywa sumu au kujinyonga eti kwa sababu tu fulani uliyempenda sana amekuacha.
Nasema hivi kwa sababu, mapenzi yapo na aliyeyafanya yawepo alishapanga kuwa wewe utaingia na nani kwenye maisha ya ndoa. Kwa maana hiyo kama umetokea kumpenda Juma au Janeth na kuamini anaweza kuwa mwenza wako kisha yeye akakukatalia, hutakiwi kuumia na kuona huna sababu ya kuendelea kuishi.
Unatakiwa ujue kwamba, Mungu hakupanga uwe na huyo uliyempenda na huenda amekuandalia mwingine wa kuwa naye katika maisha yako hivyo subira lazima ichukue nafasi yake.
Hata kama umeingia kwenye ndoa kisha baada ya muda mfupi mkeo akaomba talaka, huna sababu ya kuumia na kuamua kukatisha uhai wako. Tambua hiyo ni mipango ya Mungu.
Tusikubali kabisa mapenzi yatupe uchizi hasa katika ulimwengu wa sasa ambao mapenzi yametawaliwa na usanii wa hali ya juu. Wenye mapenzi ya dhati ni wachache sana, wengi wamekuwa ni walaghai, anaonesha kukupenda leo na kukuhakikishia kwamba hatakusaliti na atakuwa na wewe kwenye shida na raha lakini huyohuyo kesho anakutenda.
Ndiyo maana nilishawahi kusema mapenzi ni kama kamari nikimaanisha kwamba, unaweza kula au ukaliwa. Hivyo, kama uko kwenye uhusiano au uko kwenye ndoa, tarajia lolote kutokea.
Usije ukashangaa na kuumia sana pale ambapo huyo uliyenaye atakugeuka na kukuonesha makucha ambayo alikuwa ameyaficha, uwezekano huo upo!
Cha msingi ni kutokubali mapenzi yakutibulie maisha yako. Kama umeachwa, kumbuka wewe siyo wa kwanza kuachwa. Wapo walioachwa na wapenzi wao lakini waliweza kukabiliana na hali hiyo na leo wapo na wapenzi wengine na wanayafurahia maisha.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment