“Upendo na huruma ni mambo ya lazima. Yakikosekana, ubinadamu hautakuwepo,” alisema Dalai Lama.
Kwa tafsiri iliyonyooka ni kuwa uwepo wa mapenzi ndipo hujenga familia imara. Ukiona nyumba inayumba, migogoro inatawala kati ya wazazi au watoto, hapo hupaswi kuumiza kichwa, zaidi unatakiwa kupigia mstari kwamba upendo haupo.
Hata nchi, vita ya wenyewe kwa wenyewe chanzo chake ni kutokuwepo kwa upendo. Kuna vitu vitu vitatu vinategemeana, ila viwili ndiyo zaidi. Upendo, amani na huruma. Vinahitajika muda wote kwa pamoja lakini kuna kinachoanza na vingine vinafuata.
Viwili vya zaidi ni upendo na amani, halafu huruma hufuata. Palipo na upendo amani huja yenyewe, halafu ieleweke kuwa amani haitakuwepo kama upendo hakuna. Kwa maana hiyo, upendo ndiyo chemchemi ya furaha, faraja na utulivu.
Ukishakubaliana na hoja hii kuwa upendo ndiyo kila kitu, sasa weka mkazo kuhakikisha hapo unapofanya kazi, unapoishi na popote pale ambako huwa unakwenda, kuna upendo. Amua leo na uhakikisha kati yako na mwenzi wako kuna upendo ulioshiba. Huo ni msingi wa kufurahia maisha.
Maisha ya kimapenzi ni kama kioo. Yaani ukiyachekea nayo yatakuchekea, ila ukiyanunia, nayo yatakukunjia sura. Hakuna njia mbadala ya kuyachekea mapenzi zaidi ya kuwekeza upendo pale ambapo unahitaji kupendwa. Ni kichekesho kwa mbaguzi, mwenye chuki kwa wenzake halafu eti anataka apendwe. Ni ngumu.
Tukirejea pointi yetu ya wiki iliyopita ya kupambana kiungwana ni kwamba; mathalan, tabia ya mwenzi wako ya kutembea usiku wa manane imekuwa kero, sasa unaamua kumkabili. Lugha unayotumia ni ya kuudhi. Unamwambia yeye ni kiruka njia, hafai kwenye jamii. Je, kupitia kauli zako, unataka aelekee kwenye mstari sahihi au azidi kupotoka na kukuchukia?
Lugha unayotumia inaweza kuyafanya mapenzi yako kuwa mepesi na matamu. Vilevile, inaweza kusababisha yakawa magumu kupita kiasi ambayo mwisho wake ni kukufanya uishi kwenye mateso makubwa. Sasa kwa nini uteseke? Jenga subira kwa maana yenyewe huzaa hekima.
Ukishakuwa na hekima, utajua kitu cha kufanya kwa wakati sahihi. Utaelewa maneno ya kuzungumza sasa, yale ambayo unaweza kuyaweka akiba mpaka muda wake ukifika, kadhalika yapo ya kuyadharau na kuyatupilia mbali. Ukiwa na uwezo huo, itakuwa rahisi kwako kila siku kuzikabili changamoto za kimapenzi.
Silaha muhimu kwako ni kudhibiti jazba. Ukiwa mwingi wa hasira za haraka, utapoteza pointi kila siku. Utashindwa kujenga hoja zenye mafundisho kwa mwenzi wako, kwa hiyo hutamsaidia, badala yake utazidi kumpotosha. Kama ni mwanamke ndiyo kabisa, maana utamfanya azidi kuwachukia wanaume.
Ikiwa wewe ni mwanamke halafu mwanaume wako ndiye mwenye matatizo, utajisababishia majanga ikiwa utakuwa mwingi wa maneno makali. Anarudi nyumbani, badala ya kuzungumza naye kwa utaratibu, unamkaripia, unamwita malaya na kwamba eti huko alikuwa kwa wanawake.
Unapomfanyia hivyo mwanaume wako, ni sawa na kumpa akili ya ziada. Wengi wao huona hakuna faida za uaminifu wao, kwani wanajitunza lakini wanashutumiwa kwamba siyo waaminifu. Amechelewa kurudi nyumbani kutokana na kubanwa na kazi, wewe unamwambia alikuwa kwa wanawake.
Kwa nafasi yangu, nimeshaona mifano ya wanaume wengi ambao huamua kuwasaliti wenzi wao kwa sababu walipokuwa waaminifu, hawakueleweka na zaidi walituhumiwa isivyofaa. Vilevile kuna wanawake walioanzisha uhusiano wa pembeni kwa vile tu, wanaume wao hawakuwaamini pindi waliposimamia uaminifu wa kweli.
Sasa basi, weka mazingira ya kushinda mapambano yako. Tanguliza busara ambazo ndizo zitakuongoza kupambana kiungwana. Lugha chafu na papara za kuzungumza bila utulivu, vitakupeleka kwenye mateso ya kimapenzi. Mwisho utayachukia mapenzi wakati yenyewe siyo mabaya, isipokuwa ni wewe mwenyewe mapepe yako.
7. USIOGOPE KUONEKANA MNYONGE
Moja ya kasoro ambayo inaweza kukusababishia ukawa kwenye maisha ya mateso kwenye uhusiano wako ni kutaka kuonekana upo juu kila siku. Lazima ukubali kujishusha wakati mwingine kwa lengo la kupata suluhu hasa pale unapoona kwamba makosa yapo upande wako.
Unapogoma kujishusha ilhali kila kitu kipo wazi kwamba wewe ni mkosefu, kwanza utamuumiza mwenzi wako. Hapohapo utamfanya naye siku zijazo aanze kuwa mgumu kukubali makosa yake. Nyakati hizo zitakapowadia, maumivu yatakuwa upande wako. Hebu jikosoe, siyo ujinga kujishusha. Fanya hivyo uone faida zake.
Itaendelea wiki ijayo.
Global Publishers
No comments:
Post a Comment