Moto uliowashwa na baadhi ya watu wakifunga barabara baada ya kutawanywa na Polisi kwa mabomu ya machozi katika viwanja vya SOWETO vilivyopo jijini hapa, barabara Iiliyopo eneo la Kaloleni. (Picha zote na Ferdinand Shayo)
Moto ukiwaka katikati ya barabara wakati wa vurugu zilizotokea katika viwanja vya SOWETO mjini Arusha.
Wanafunzi wa shule wakijiziba na nguo na kunawa uso baada ya kudhuriwa na mabomu ya machozi yaliyopigwa leo na Polisi waliokuwa wakitawanya maelfu ya watu waliokuwa kwenye mkutano katika viwanja vya SOWETO.
Baadhi ya watu wakifunga barabara baada ya kutawanywa na Polisi kwa mabomu ya machozi katika viwanja vya SOWETO vilivyopo jijini hapa, Barabara Kuu inayopitisha magari ya mikoani eneo la Kimahama.
ARUSHA, Tanzania
MBUNGE wa Mbulu kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mustafa Akoonay, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, viongozi wengine wa Chadema na wafuasi kadhaa wa chama hicho wanashikiliwa na Jeshi la Polisi jijini Arusha kwa mahojiano kufuatia vurugu zilizoibuka katika mkutano wa hadhara.
Akizungumza na Habari Mseto Blog kutoka jijini Arusha, Kamanda wa Polisi mkoa huo, Liberatus Sabas alithibitisha kukamatwa kwa viongozi hao waandamizi wa Chadema na wafuasi wa chama hicho muda mfupi baada ya mkutano wa dharura wa chama hicho katika uwanjwa wa Soweto.
Jeshi la Polisi lilivunja mkutano huo kwa kutumia gesi ya machozi yaliyorindima kwa zaidi ya saa mbili kutawanya wafuasi wa chama hicho uwanjani hapo, kutokana viongozi hao kutumia nafasi ya maombolezo kuendesha mkutano hadhara ambao haukuwa na kibali.
Watu kadhaa wanadaiwa kupoteza maisha katika tafrani hiyo, huku wengine wakijeruhiwa na kufikishwa hospitali mbalimbali jijini humo, ikiwemo Hospitali ya Seliani kwa matibabu baada ya kuumizwa na askari, huku wengine wakipata mshtuko iliyosababishwa na mlipuko wa mabomu ya machozi.
Wakiwa ndani ya magari madogo, askari polisi walilipua mabomu hayo maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha hali iliyowalazimu wafanyabiashara jijini humo kufunga biashara zao na kukimbia wakihofia kuvamiwa na wakazi waliokuwa wakikimbia hovyo kunusuru maisha yao.
Hali ya usafiri iligeuka adha nyingine kwa wakazi wa jiji la Arusha, baada ya daladala kushindwa kutoa huduma hiyo, zikihofia mabomu yaliyokuwa yakirushwa na askari, huku barabara zikifungwa baada ya wafuasi wa CHADEMA kuchoma matairi barabarani.
Tafrani hiyo kwa namna moja iliwaathiri hata wanahabari, ambao walijikuta wakipata adha ya ulipuliwaji wa mabomu hayo na kulazimika kujificha katika magofu ya nyumba za AICC zilizoko karibu na uwanja wa Soweto kwa zaidi ya masaa mawili.
Aidha, mapema Waziri Mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda, alikiri kuwa uchunguzi wa haraka umebaini kuwa bomu lililotumika kulipua katika mkutano wa Chadema juzi limetengezwa China, na aina hiyo ya mabomu yanamilikiwa na vyombo vya dola, hasa Jeshi la Wananchi (JWTZ).
No comments:
Post a Comment