ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, June 2, 2013

WATATU WAFARIKI KWA KUANGUKIWA NA UKUTA PEMBA

Wananchi wakiuangalia mnara wa tangi la maji ulioanguka na kupoteza maisha ya wananchi watatu leo asubuhi
Askari wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama Kisiwani Pemba, wakiwa katika zoezi la kutoa miili ya marehemu waliopoteza maisha katika ajali ya kuangukiwa na ukuta wa tanki la maji eneo la Machomanne Chake Chake Pemba leo.
Daktari bingwa kutoka Cuba anayefanya kazi zake Kisiwani Pemba, (jina halikufahamika) akimtibu mmoja kati ya majeruhi waliolazwa katika hospitali ya Chake Chake baada ya ajali hiyo.

JUMLA ya watu watatu wamefariki dunia papo hapo na watatu kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta wa mnara wa tanki la maji uliopo Machomanne Chake Chake Pemba, leo saa tatu asubuhi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Suleiman Hassan Suleiman, amesema kuwa, merehemu hao walifikwa na mauti wakiwa katika kazi ya kuteremsha ukuta wa mnara wa tanki la maji ambao walikuwa wameshaukata.
Kamanda alisema kuwa idadi ya mafundi waliokuwepo kazini hapo walikuwa ni 12 ambapo watatu wamepoteza maisha papo hapo na watatu kujeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya Chake Chake na wengine sita walikimbia na jeshi la polisi liko katika utaratibu wa kuwatafuta kwa ajili ya kuelewa hali zao.

Aliwataja marehemu hao kuwa ni Juma Rashid Juma (35) mkazi wa Chanjaani, Suleiman Mohammed Abdiadi 'maarufu kama Golo' (55) mkazi wa Kwale na Salum Muhidini Vuai 'Bandudu' (35) mkazi wa Madungu wote wakazi wa wilaya ya Chake Chake mkoa wa Kusini Pemba.

Na majeruhi katika ajali hiyo ni pamoja na Jackson John (26) mzaliwa wa Iringa na mkazi wa Msingini, Ali Saleh Ali (35) mkazi wa Michakaeni na Yohana Richard (25) mkazi wa Machomanne Chake Chake Pemba.

(Habari/Picha: Abdi Sueliman na Bakari Mussa, Pemba-GPL)

No comments: