ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 3, 2013

Familia ya Mandela wavutana

Pretoria. Wakati Rais wa kwanza mzalendo wa Afrika Kusini, Mzee Nelson Mandela akiendelea kuugua hospitalini, mivutano inaendelea kuigawa familia yake katika kile kinachoonekana kuwa ni “kuwania madaraka”.
  Hali hiyo inatokana na kuwapo kwa taarifa kwamba familia ya kiongozi huyo inakusudia kumvua Utemi (uchifu) wa Kijiji cha Mvezo, mjukuu wa Mandla ambaye ni mjukuu wa Mzee Mandela kwa madai kwamba kwa mujibu wa mila na desturi umri wake haumruhusu kushika nafasi hiyo.
  Ndugu wa kambo wa Mandla, Ndaba alisema viongozi wa kimila wanakusudia kuchukua hatua kwa kumvua madaraka ndugu yake huyo kutokana na kukiuka miiko na mila za jadi pale alipohamisha mabaki ya miili ya wanafamilia hao waliokuwa wamezikwa Qunu na kuyazika upya Mvezo.
  Wakati hayo yakiendelea kwa upande mwingine wanafamilia hao wa Mandela jana waliingia katika siku ya pili ya mapambano mengine katika Mahakama Kuu ya Eastern Cape, Mthatha kuhusu suala la kuhamishwa kwa makaburi.  Binti mkubwa wa Mandela, Makaziwe anaongoza wanafamilia 16 dhidi ya Mandla ugomvi ambao chimbuko lake ni hatua ya mjukuu huyo ambaye pia ni mbunge kuhamisha makaburi ya wanafamilia watatu kutoka eneo la Qunu kwenda Mvezo.
Alifanya hivyo 2011 ikiwa ni hatua ya kutaka babu yake, Mzee Mandela akifa naye azikwe Mvezo ili kuwavutia watalii katika kijiji hicho. Mandela aliwahi kunukuliwa akisema akifa angependa azikwe pembezoni mwa walipozikwa ndugu zake ambako ni Qunu.
Mandela amelazwa katika hospitali ya magonjwa ya moyo, Medclinic iliyopo Pretoria karibu wiki ya nne sasa na hali yake imeendelea kuwa mbaya kiasi kwamba taarifa zinasema anapumua kwa msaada wa mashine.
Mwananchi

No comments: