ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 2, 2013

HAKUNA KAMA OBAMA

Stori:Mwandishi wetu
Ziara ya Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, imetosha kudhihirisha kwamba hakuna kiongozi mwenye mvuto na anayelindwa duniani kote kama yeye.
Inaweza kuonekana pengine ulinzi wake umeimarishwa Afrika tu lakini ripoti zinaonesha kwamba kiongozi huyo hulindwa kwa nguvu kubwa kokote kule aendako.
Ulinzi wa Obama akiwa nchi za Afrika wikiendi iliyopita, unalingana na ule ambao uliwekwa Mei, 2011, alipokwenda Uingereza.
Obama, alitarajiwa kuwasili nchini jana mchana, kadhalika ulinzi wake ulishadumishwa kwa kiwango kikubwa kabla hata ya ujio wake.
Maandalizi pekee ya ziara yake ni kipimo tosha kwamba Obama hana mfano wake duniani kote kwa sasa.
Ukichanganya na ulinzi anaopewa, mvuto wake kijamii ni mkubwa ndiyo maana ziara yake imekuwa ya kipekee duniani kuliko yoyote ile iliyowahi kufanywa na kiongozi mwingine ulimwenguni kote.
DAR YATIKISIKA
Kuelekea ujio wa Obama, Jiji la Dar es Salaam limetikisika kwa kiasi kikubwa na kusababisha ofisi zifungwe na wafanyakazi wengine kujipa likizo bila kufuata utaratibu.
Ugumu wa watu kufika katikati ya Jiji la Dar es Salaam wakati wote wa maandalizi ya ujio wa Obama, ndiyo kichocheo cha wengine kujipa likizo mpaka hapo kiongozi huyo atakapoondoka kurudi nchini kwake.
Baadhi ya ofisi zinazotegemea mauzo ya siku, zimefungwa kwa sababu mzunguko wa kibiashara haukuwa mzuri kuanzia wiki mbili kabla ya ujio wa Obama.
Magari ya abiria, yaani daladala na teksi nyingi zilisitisha kutoa huduma kwa muda kwa sababu ya kukwepa hasara, kutokana na ukweli kwamba abiria walipungua kwa kiasi kikubwa.

WAMACHINGA WALIA
Kishindo cha Obama, kimewagusa mpaka wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama wamachinga ambao wamelia kitendo cha kuondolewa katikati ya jiji.
Mfanyabiashara Maneno Kisala alisema: “Hivi sasa maisha yangu yamekuwa magumu. Kipato ambacho nilikuwa nakipata hapa na kula na familia yangu sasa sikipati.”
Mwingine, Henry Kilado alilalamika: “Tunajua Obama anakuja kwa faida kubwa ya nchi yetu lakini dah, maisha yamekuwa magumu sana. Inabidi serikali ifikirie namna ya kutuacha tufanye biashara, usalama ungedumishwa kwa njia nyingine tu.
“Sisi siyo magaidi, nchi yetu ni salama. Vyombo vya usalama vingetusimamia lakini vingetuacha tufanye kazi zetu vizuri.”
AJA NA NDEGE 20
Obama, anatembea kwa kutumia ndege yake ya Air Force One ambayo ni maalum kwa ajili ya Rais wa Marekani lakini pamoja naye, zipo ndege nyingine 20.
Ndege hizo 20 ndizo ambazo zimekuja nchini na makachero watakaomlinda kiongozi huyo katika kipindi chote atakachokuwepo Tanzania.
Taarifa zinasema katika ndege hizo 20, ya mwisho iliwasili Jumapili iliyopita mchana na timu ya walinzi iliratibu kila kitu kabla ya Obama kutarajiwa kuwasili jana mchana.

MAGARI 150
Meli mbili na manowari kubwa ya kivita, vimewasili nchini kwa ajili ya kudumisha ulinzi wa Obama kipindi chote akiwa nchini.
Magari 150, yamewasili nchini, hayo yalibebwa na ndege kubwa tatu, kila moja ikiwa na uwezo wa kubeba magari 50, siku kadhaa kabla hajawasili nchini.
Uwepo wa magari hayo una maana kuwa msafara wa Obama hautaingiliwa na mengine, vilevile lengo kuu ni kwamba lazima sura ya kiongozi huyo anapotembea ndani ya Marekani, ifanane na akiwa nje.
MAREKANI NI TISHIO KWA TEKNOLOJIA
Zipo helikopta kadhaa ambazo ziliwasili nchini vipandevipande na kuunganishwa hapahapa.
Helikopta hizo, kazi yake ni kufanya doria kipindi chote cha kabla ya Obama hajawasili nchini na muda wote akiwa ndani ya nchi.
Wikiendi iliyopita, makachero wa Marekani walikuwa na kazi nzito ya matayarisho ya mwisho ya ziara ya Rais Obama, ambapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa na kazi ya kuunganisha helikopta za doria.
Makachero hao walikuwa wakiunganisha helikopta sita zilizosafirishwa vipandevipande kutoka Marekani, ambapo meli mbili za kivita na ndege moja pia zimewasili.
Habari zinasema kuwa helikopta hizo sita, ziliunganishwa katika sehemu ya karakana ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

No comments: