
Dar es Salaam. Hatimaye, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetoa taarifa ya uchaguzi wa wanafunzi wa kuingia kidato cha tano katika sekondari za Serikali na vyuo vya ufundi.
Katika uchaguzi huo, wanafunzi 34,213 kati ya 34,599 waliofaulu kwa daraja la kwanza mpaka la tatu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano, vyuo vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Uteuzi wa wanafunzi hao ambao wanapaswa kuripoti shuleni Julai 29, mwaka huu unamaanisha kwamba kutakuwa na upungufu wa wanafunzi wapatao 10,074 katika shule na vyuo hivyo vya ufundi ambavyo vina uwezo wa kuchukua wanafunzi 43,757.
Upungufu huo unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya wanafunzi hao watajiunga na shule za sekondari za binafsi.
Aidha, kwa mujibu wa matokeo hayo, ni wanafunzi 386 tu waliofaulu katika madaraja hayo ya kwanza mpaka tatu ambao hawakuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano au vyuo vya ufundi. Hao, wanaweza kujiunga na vyuo vya ualimu.
Kwa mujibu wa Kitabu cha Takwimu cha Wizara ya Elimu (Best), mwaka 2012 wanafunzi 17,095 walichaguliwa kujiunga na vyuo mbalimbali vya ualimu nchini.
Kutokana na takwimu hizo, Serikali italazimika kuchukua wanafunzi wengi zaidi waliopata daraja la nne kujiunga na vyuo vya ualimu kujaza pengo hilo.
Wanafunzi waliopata daraja la nne kwenye mtihani wa kidato cha nne mwaka jana ni 124,260.
Mulugo alisema kuwa wanafunzi waliopata daraja la nne pointi 27 watachaguliwa kujiunga na vyuo vya ualimu endapo wataomba.
“Vigezo vya kujiunga na kidato cha tano na vile vya vyuo vya ualimu ni tofauti, kidato cha tano mwisho anatakiwa mtu mwenye pointi 25 na combination yake (uwiano wa masomo) iwe sawa, ualimu ni pointi 27 wanafunzi wanaomba.
“Mwanzoni walikuwa wanakwenda wenye pointi 28 lakini mwaka jana tukasema hapana iwe pointi 27 na tutachukua kuanzia waliomaliza mwaka 2008 kama wataomba, kwa sasa hivi watu wanaendelea kuwachagua,” alisema Mulugo.
Waliochaguliwa
Akitangaza uchaguzi wa wanafunzi hao jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema wanafunzi 33,683 wakiwamo wavulana 23,383 na wasichana 10,300 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano kwenye shule 207 za Serikali.
“Idadi hiyo ni ongezeko la wanafunzi 2,824 sawa na asilimia 9.15 ikilinganishwa na wanafunzi 30,859 waliochaguliwa mwaka 2012. Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali,” alisema Mulugo.
Alisema kati ya wavulana hao 23,383 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, 13,708 sawa na asilimia 58.62 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi huku 9,675 sawa na asilimia 41.38 wakienda kusoma masomo ya sayansi ya jamii.
Alisema kati ya wasichana 10,300 waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano, 5,038 sawa na asilimia 48.91 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na 5,262 sawa na asilimia 51.09 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya jamii.
Vyuo vya ufundi
Waziri Mulugo alisema wanafunzi 530, wavulana wakiwa 416 na wasichana 114 wamechaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi na Taasisi ya Menejimenti ya Maendeleo ya Maji.
Idadi ya wanafunzi wanaojiunga na vyuo ufundi imepungua kutoka 564 mwaka 2012 hadi 530 mwaka huu.
“Idadi ya wasichana waliochaguliwa kujiunga na vyuo vya ufundi imeongezeka kutoka 47 mwaka 2012 na kufikia 114 mwaka huu, hili ni ongezeko la wanafunzi 67 sawa na asilimia 142.55,” alisema.
Upungufu wa wanafunzi 10,000
Mulugo alisema kwa mwaka 2013 nafasi za kujiunga na kidato cha tano zilikuwa ni 43,757 zikiwamo 18,564 za masomo ya sayansi na 25,193 masomo ya sayansi ya jamii, ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 3,757 ikilinganishwa na mwaka jana ambao kulikuwa na nafasi 41,000.
“Nafasi zilizojazwa ni 33,683, nafasi zote za masomo ya sayansi zimepangiwa wanafunzi, katika PCB (Fizikia, Kemia na Biolojia) kulikuwa na wanafunzi 6,188 na waliopangwa ni 6,400, kwa sayansi ya jamii nafasi nyingi zimebaki wazi,” alisema.
Alisema kuwa, kwa mchepuo wa HKL (Historia, Kiswahili na Fasihi ya Kiingereza), kulikuwa na nafasi 5,300 lakini wanafunzi waliokuwa na nafasi za kusoma masomo hayo ni 1,527 tu.
Wadau
Akizungumzia uchaguzi huo jana, mdau wa elimu na Profesa mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Ruth Meena alisema nchi nyingi duniani ambazo zinajua maana ya elimu bora, hupeleka wanafunzi waliofanya vizuri na kuwapeleka vyuo vya ualimu.
“Kwanza mtu wa kidato cha nne hastahili kwenda kufundisha, hata kama ana daraja la kwanza siyo sawa, lazima tubadilike, lengo la taifa ni kuwa na watu wa kuweza kupambana na utandawazi, hawa hawawezi kutufikisha huko,” alisema Profesa Meena.
Alisema kwenye miaka ya 1970, wazo la kuwa watu wa kidato cha nne hawawezi kufundisha lilikuwapo lakini cha kushangaza limeyeyuka.
Alipinga walioshindwa kidato cha nne kusomea ualimu akisema hawataweza kujenga msingi mzuri kwa watoto na kwamba kufanya hivyo kutazidi kuporomosha elimu nchini. Mkuu wa Idara ya Saikolojia ya Elimu na Masomo ya Mitalaa ya Shule Kuu ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo alisema matokeo hayo hayatakuwa na athari kwa vyuo vya ualimu tu, bali hata vyuo vikuu mwaka 2015 ambavyo alisema havitapata wanafunzi wa kutosha. Pia alisema kuna hatari ya vile vya binafsi kufungwa.
“Mwaka 2015, vyuo vikuu vitapambana sana kupata wanafunzi, hata kama vyuo havitapanuka kutakuwa na mahitaji ya wanafunzi 27,000 na takwimu zinaonyesha kuwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita ni nusu tu wanaofaulu,” alisema Dk Mkumbo.
Alisema mwaka huu, Serikali haitakuwa na ujanja, bali kukiuka sera yake inayotaka kila anayejiunga na vyuo vya ualimu kusomea ngazi ya cheti awe na angalau daraja la tatu.
Hivyo alisema kwa kupeleka wanafunzi waliofeli ni kuendelea kuzalisha matokeo mabovu, hivyo kuitaka iache kuangalia wingi wa wanafunzi na shule na badala yake ikazanie ubora wa elimu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment