ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, July 2, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 12

Mpenzi msomaji, baada ya kuelezea vipengele vya awali kuhusiana na makala haya yahusuyo utamu au mateso ya mapenzi hutokana na mtindo wako wa maisha. Hebu tumalizie vilivyosalia, naamini vitakupa darasa la kutosha

WAFURAHIE MARAFIKI ILA USIWAPE TURUFU KWENYE MAPENZI YAKO
Fanyia kazi hili suala kwa umakini wa hali ya juu. Turufu au kwa lugha nyingine kura ya veto katika mapezi yako unayo wewe mwenyewe. Kuna watu hawajui mipaka ya kushirikishwa, wakiombwa ushauri wanaweza kuhisi wanamamlaka kwenye uhusiano wa watu wengine, matokeo yake hutoa maagizo.
Kataa hilo kwenye uhusiano wako. Marafiki wanaweza kuwa au wasiwe muhimu kwenye maisha yako. Itategemea na uhusika wao. Jiwekee jawabu kichwani kwako kwamba hata wawe na umuhimu wa aina gani katika maisha yako lakini hawana ubavu wa kufanya uamuzi wowote katika uhusiano wako na mwenzi wako.
Asili ya binadamu, anapokuwa anaombwa ushauri wa mara kwa mara huhisi ana mamlaka makubwa kwa yule aliyeomba ushauri. Hapo hujenga kiburi na wakati mwingine hujivuna waziwazi kwamba yeye nguzo inayoshikilia uhusiano wako. Je, unaona ni sawasawa mtu mwingine kujigamba hivyo?
Inawezekana isiwe kwa kujisifu, ila ukweli uwepo ndani ya kichwa chako kwamba tabia ya kuwashirikisha marafiki kwenye matatizo yako ya uhusiano, ni sawasawa na kuiamiisha jamii kwamba bila wao, maisha yako ya kimapenzi hayawezi kupiga hatua. Hilo likatae.
Ipo tabia ya watu kuwapa kipaumbele marafiki kuliko wenzi wao. Unakuta mwenzi wako analaumu kwamba muda wake mwingi wa kuwa na wewe, unautumia kweye vikao vya washkaji na kadhalika. Unashindwa kabisa kuzingatia wito wake na kuonesha kujali hisia zake.
Hiyo ni tabia mbaya kwa sababu inamfanya mwenzi wako ajione kuwa hana lolote mbele ya marafiki zako. Kadiri unavyofanya na kumwonesha yeye hana kipaumbele kwako, ndivyo unavyomfunza na yeye asikupe daraja la kwanza. Itakapokugeukia, utaumia sana, kwa hiyo jifunze kwa utulivu.
Kuna sababu gani ya wewe na mwenzi wako mkose amani mpaka mshindwe kupeana faraja na raha zinazohitajika kwa sababu ya marafiki? Hebu litazame hili kwa makini na uelewe kuwa muda mwingine haohao marafiki wanakucheka na kukuona huna maana, kwani wao wanawaheshimu wapenzi wao.
Kila mmoja anao mtindo wake wa maisha. Pengine hao marafiki zako wamewazoesha wapenzi wao kuzurura mpaka usiku wa manane ndipo hurudi nyumbani. Huo ni mtindo wao, wewe achana nao, mheshimu mwenzi wako. Anahitaji kuwa na wewe, mpe nafasi anayoitaka.
Mpe sababu ya kukuona wewe ni mwanaume sahihi katika maisha yake. Haiwezekani ukawa humjali halafu ukawa unawathamini sana marafiki kuliko yeye halafu naye awe anajihesabu kuwa ana mpenzi sahihi. Atakushusha thamani, nawe ukigundua hilo itakuuma. Hata hivyo, utakuwa umeyataka mwenyewe.

CHUNGA ISILE KWAKO
Utamu au mateso ya mapenzi husababishwa na mtindo wako wa maisha. Ukiyachekea, nayo yatakuchekea. Ukiyatazama kwa jicho baya, vilevile yatakuonesha ukatili wake. Mapenzi hupandwa, hustawishwa, yakishastawi ndipo utakapoweza kuvuna penzi lililo bora.
Hivyo hivyo, utakapojielekeza katika kumfanya mwenzi wako awe na furaha, atosheke na wewe, utakuwa unawezesha hatua muhimu sana katika maisha yako. Maana kile unachokipanda kwake na kukistawisha, mavuno utavuna mwenyewe.
Usitafute mchawi wa mateso ambayo wewe unakumbana nayo leo katika uhusiano wako. Suluhu ipo ndani yako, tena usihangaike, maana wewe mwenyewe ndiye dawa. Utazame mtindo wako wa maisha. Unaishije na mwenzi wako? Je, mapenzi unayapokea na kuyatenda kwa sura hasi au chanya?
Utakuja kugundua kuwa mtindo wako wa maisha ndiyo tatizo. Haiwezekai ukawa huwasiliani vizuri na mwenzi wako halafu ukawa na matarajio kuwa uhusiano wenu utakuwa barabara. Jamani, kila siku yanazungumzwa, ukiona vyaelea, ujue vimeundwa.
Tunapofikia tamati ya mada hii, nakuasa uzingatie sana vipegele vyote. Kila kipengele kina ujazo wa uchambuzi mahususi. Utakapoelewa utaweza kujua njia ya kushika na mtindo bora wa maisha utakaokuwezesha kuyaona mapenzi ni matamu, halafu mateso utayasikilizia kwa wengine.
Mapenzi hayana ufundi kujua. Hayahitaji ubabe na sifa nyingine zisizopendeza. Yanataka ujiweke juu pale inapohitajika na ujishushe mpaka chini kabisa kama tu ndivyo yanavyohitaji kwa wakati huo. Kaa mbali na kiburi. Zingatia hisia za mwenzako na utende ayapedayo ili naye akutendee uyapendayo. Usipoyakubali haya, itakula kwako.
Mwisho.

GPL

No comments: