
Vyama vya CCM na Chadema vimekuwa vikituhumiana kuhatarisha amani ya nchi
Dar es Salaam. Siku tatu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuponda mpango wa Chadema kuanzisha kambi kwa ajili ya mafunzo ya ulinzi kuwalinda viongozi na wanachama wake, chama hicho kikuu cha upinzani nchini kimeibuka na kusema kuwa kinaendelea na mpango huo na kambi hizo zitaanza rasmi wiki ijayo.
Kimesema hakitishwi na kauli ya Jeshi la Polisi kukionya juu ya uanzishwaji wa mafunzo hayo, kwamba jeshi hilo linatakiwa kuanza kukizuia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwanza, kwa maelezo kuwa chama hicho tawala pia kina kikundi cha ulinzi ‘Green Guards’ ambacho kinafanya mafunzo ya kijeshi, huku kikitumia silaha za moto.
“CCM ndiyo wataipeleka nchi hii pabaya, wanawafundisha vijana huku wakiwabebesha bunduki, wanajenga taifa la aina gani, bunduki ni silaha ya kivita sasa wanaandaa watu kupigana na nani” alisema Mkurugenzi wa Organaizesheni na Mafunzo wa chama hicho, Benson Kigaira jana wakati akizungumza na wanahabari huku akionyesha picha za mafunzo ya CCM, zinazoonyesha vijana wakiwa wamebeba silaha (hata hivyo ni mbao zilizotengenezwa kwa mfano wa bunduki).
Wakati Chadema wakieleza hayo, CCM kimeshtushwa na taarifa hizo na kueleza kuwa hali hiyo sasa inahatarisha usalama wa nchi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), Martin Shigela alisema ni vyema Chadema kikawaambia wananchi wawalinde, kuliko kuanzisha mafunzo huku akimtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini, John Tendwa kulitizama kwa kina suala hilo.
Akifunga Kongamano la Amani lililoandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), Dar es Salaam Julai 10, mwaka huu, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa pia alikosoa kitendo cha Chadema kususia kongamano hilo alisema, “Sasa hawa kweli wanapenda amani yetu wakati hawapendi tuzungumze wanataka watu wauane, wapigane.”
Mbali na Rais Kikwete, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, SSP Advera Senso juzi alikionya chama hicho kuhusu mpango huo akisema kuwa kitendo cha chama chochote cha siasa kikiwemo Chadema, kuanzisha kikundi cha kujihami ni kinyume na sheria za nchi na endapo watafanya hivyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli ya jana ya Chadema ni mwendelezo wa ile iliyotolewa na Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe Julai 9, mwaka huu, ambapo alisema kimechukua hatua hiyo baada ya Serikali na vyombo vyake vya ulinzi na usalama kushindwa kufanyia kazi malalamiko yao kuhusu mauaji, vitisho na matukio ya kutisha wanayofanyiwa baadhi ya viongozi na wanachama wao.
Katika ufafanuzi wake Kigaila alisema Chadema hakianzishi vikundi vya kijeshi, bali mafunzo ya kuwafundisha walinzi wa chama hicho ‘Red Brigade’, jinsi ya kujilinda.
“Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni haki kwa raia yeyote kujilinda, Chadema ni taasisi ni haki yetu kuilinda taasisi yetu ndiyo maana tumesajili kikundi chetu cha ulinzi, sasa nani anatutisha, tunataka polisi waanze na CCM kwanza ambao katika mafunzo yao wanafundisha hadi kupiga saluti na kutumia silaha,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yataanza rasmi wiki ijayo, huku akisita kutaja siku yatakayoanza, wala mikoa yatakayofanyika na kusisitiza kuwa hayo yatatangazwa wiki ijayo wakati vijana wakienda katika mafunzo.
Tuhuma
Alisema kabla ya uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga mwaka 2011, CCM kilianzisha kambi ya vijana eneo la Ulemo wilayani Iramba katika Jimbo la Iramba Magharibi na kwamba kambi hiyo ilikuwa na vijana 200.
Alifafanua kwamba katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga CCM ilianzisha kambi katika wilayani Nzega, Tabora, Shinyanga na Singida Mjini za kambi hizo zilikuwa na vijana 800.
“Vijana hao walipelekwa katika uchaguzi wa Igunga na kusababisha kifo cha kada wa Chadema, Msafiri Mbwambo ambaye alikuwa wakala wa chama katika uchaguzi huo, awali tuliwaeleza polisi jinsi kambi hizo zilivyowekwa, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka leo,” alisema.
Alisema mwaka jana CCM ilifanya mafunzo ya kitaifa ya vijana wao wa ‘Green Guards’ mkoani Mwanza na baada ya mafunzo hayo walifanya gwaride la kijeshi.
Alisema wakati vijana hao wakihitimisha mafunzo hayo walikaguliwa na Mwenyiki wa Chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Phillip Mangula pamoja na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana, huku wakipigiwa saluti na vijana hao waliokuwa wamebeba ‘matoi’ yaliyotengenezwa kwa mfano wa bunduki.
“CCM wanasema kuwa Green Guards wanafundishwa ujasiriamali, hivi watu wanaofundishwa ujasiriamali huwa wanapigiana saluti, huwa wanabeba ‘matoi’ yenye mfano wa bunduki,” alihoji.
Alisema kambi za CCM zilianza tangu mwaka 2007 wakati wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kiteto, na kufafanua kuwa katika uchaguzi huo baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Zanzibar, Hamad Musa Yusuf walipigwa na Green Guards huku polisi wakishuhudia.
Kauli ya CCM
Uanzishwaji wa mafunzo hayo umeonekana wazi kukitesa CCM ambapo jana Shigela alisema “Chadema kabla ya kuanza kutoa mafunzo hayo kwa vijana hao (Red Brigade) wanatakiwa kuwaeleza wananchi dhamira halisi ya kuanzishwa kwake, kama siyo kuchochea uvunjifu wa amani.”
“Chadema ni chama cha siasa, kinaomba kuwatumikia wananchi wanaowapigia kura wenyewe hivyo kama wanaona hawatendewi haki na polisi wawaambie wananchi wenyewe wawalinde lakini si kuanzisha, kutoa mafunzo hayo kwa vijana.”
Imeandaliwa na Fidelis Butahe, Ibrahim Yamola na Irene Mossi wa Mwananchi
No comments:
Post a Comment