ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 17, 2013

4,000 wakusanya saini kupinga tozo ya simu

Mtumiaji wa simu akitumia simu yake kuwasimiliana na watu, hivi karibuni Serikali ilitangaza tozo ya kwenye simu kwa kila mwezi jambo linalopigiwa kelele na wananchi kwamba wengi hawataweza kumudu tozo hiyo.

Dar es Salaam. Jukwaa la Change Tanzania, limekusanya saini 4,000 za wananchi mikoa mbalimbali, wanaopinga tozo ya kodi kwenye laini ya simu.
Taarifa ya Mratibu wa Jukwaa hilo, Maria Sarungi, ilisema saini hizo
ni fursa kwa mbunge au wabunge wataokuwa tayari kuitika wito wa wapigakura wao na kupeleka hoja bungeni kwa ajili ya kufuta tozo hiyo.
Ilisema saini hizo zimekusanywa kutoka kwa wananchi Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Morogoro, Manyara, Mwanza, Shinyanga, Singida, Ruvuma pamoja na Zanzibar.
Ilisema wananchi wanataka tozo hiyo iondolewe kwa sababu inamkandamiza mwananchi wa hali ya kawaida na chini.
“Hawa ni asilimia 67 ya wananchi wanaoishi chini ya kipato cha dola 1.25 (Sh2,000) kwa siku. Takwimu zinaonyesha kati ya wamiliki wa laini za simu milioni 22, milioni nane wanatumia chini ya Sh 1,000 kwa mwezi. Huku ni kuwaongezea mzigo wananchi hawa,” ilisema taarifa ya Sarungi.
Pia, Ilisema tozo hiyo itawanyima kabisa wananchi hao, fursa ya kutumia huduma muhimu ya mawasiliano ya simu.
“Lakini kodi hii haifuati misingi ya kulipa kwa kadiri ya matumizi, ni kodi kandamizi inayotozwa kwa wamiliki wa laini za simu wote kwa kiasi kimoja bila kuzingatia kiwango cha matumizi,” ilisisitiza.
Ilisema kodi hiyo ni juu ya ongezeko la kodi mbalimbali kwa huduma za simu za mkononi ikiwamo kuongezeka kwa ushuru kutoka asilimia 12 hadi 14.5.

No comments: