ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 30, 2013

BAN KI MOON ALAANI KUUAWA KWA MLINZI WA AMANI WA TANZANIA DRC

Pichani ni walinzi wa Amani wakiwa katika moja ya doria kwenye mitaa ya mji wa Goma, mwanzoni mwa wiki hii kumetokea mapingano katika eneo la vilima vya Kibati Magharibi ya Kivu ambapo kundi la waasi la M23 lilishambulia walinzi wa amani wa Misheni ya Kutuliza Amani katika DRC ( MONUSCO) waliokuwa katika Operesheni ya kulinda raia wakishirikiana na Majeshi ya Serikali ya DRC. Shambulio hilo limesababisha mwanajeshi Mtanzania kupoteza maisha na wengine 10 wakiwamo wanajeshi wa Afrika ya Kusini wamejeruhiwa. Tukio la kushambuliwa kwa walinzi hao limelaaniwa vikali na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, na Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ban Ki Moon na Baraza Kuu wametuma salamu za rambirambi kwa familia ya marehemu na familia za wale waliojeruhiwa na kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Aidha Baraza Kuu limesisitiza kwamba vitendo vinavyolenga kudhoofisha mamlaka ya MONUSCO havitavumiliwa

Na Mwandishi Maalum
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,  Ban Ki Moon  amelaani kuuawa kwa Mlinzi wa Amani kutoka Tanzania  ambapo  wengine  kadhaa  wamejeruhiwa baada ya kushambuliwa na   kundi la waasi la M23 katika  katika  eneo la  Mashariki ya   Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa   na msemaii wa Katibu Mkuu ,  inaeleza kwamba. “ Katibu Mkuu analaani kwa nguvu zote mauaji  ya mlinzi huyo na  kujeruhiwa kwa walinzi  wengine  10 na anatoa salamu zake za rambirambi kwa familia  za walinzi hao  na  kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Jamhuri ya Afrika ya kusini”.
Mashambulizi dhidi ya walinzi hao wa Amani yametokea   siku ya  jumatano katika  Vilima vya Kibati Magharibi ya Kivu ambako Misheni ya   kutuliza Amani   ya  Umoja wa Mataifa katika DRC ( MONUSCO)  ilikuwa ikisaidiana  na  majeshi ya  serikali ya   DRC kuwalinda raia katika eneo  la Goma ambalo lina idadi kubwa ya watu.
Kwa mujibu wa taarifa  hiyo,  MONUSCO  ilijibu mashambulizi hayo kwa kutumia zana mbalimbali za kivita yakiwamo makombora, mizinga na helkopta za kivita wakati majeshi ya DRC yalitumia askari wa ardhini,  vifaru na helkopta za kivita na kwamba operesheni  hiyo bado inaendelea.

Taarifa   inaeleza zaidi kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuwajibika na kuhakikisha inachukua  hatua zote muhimu kwa kuzingatia Azimio  namba  2094 ( 2013) la Baraza Kuu la Usalama  la Umoja wa Mataifa ambalo linasisitiza  ulinzi wa raia katika eneo hilo la Mashariki  ya Kongo.
Wakati huo huo , wakati mapigano yakiendelea,  Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,  katika kikao chake kilichofanyika siku ya Alhamisi   nalo limetoa tamko la  kulaani  vikali tukio la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania,  na kutoa salamu zako za pole kwa serikali ya  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na familia ya marehemu pamja na wale waliojeruhiwa.
Tamko la Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  limetolewa  taarifa hiyo baada ya  Baraza hilo kupokea  taarifa  rasmi  iliyowasilishwa na Naibu Mkuu wa Idara ya Operesheni za Ulinzi wa  Amani, Bw. Edmond Mulet  kuhusu    kinachoendelea  katika DRC.
 Baraza pia limelaani  kwa nvugu zote dhidi ya kujirudia rudia kwa     matukio yanayofanywa na M23  yanayolenga MONUSCO na  rais yakuwalenga raia na MONUSCO.
Na kwa sababu hiyo Baraza   Kuu la Usalama limetaka mamlaka ya DRC kuchunguza tukio la kuuawa kwa mlinzi huyo wa Amani na kisha kuwafikisha mbele ya sheria watakaobainika kuhusika na tukio hilo.
Aidha Baraza Kuu limerejea tena  tamko lake la kuitaka M23 na makundi mengine yenye silaha katika DRC kuacha aina zote za machafuko na kuweka chini silaha zao. Na kwamba, halitasita kupitisha  vikwazo vya nyongeza kwa yeyeyote yule ambaye atabainika kujihusisha na fujo na machafuko na kwamba vikwazo hivyo vitahusu pia silaha.
Aidha wajumbe 15 wa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa limeipongeza MONUSCO kwa namna ambavyo imekuwa ikitekeleza mamlaka yake na hususani ya kuwalinda raia na  limeitaka na kuihimiza  MONUSCO kuendelea na wajibu wake huo  huku lilikisisitiza kwamba Baraza Kuu la Usalama  halitavumilia kitendo chochote kinacholenga kudhoofisha mamlaka ya MONUSCO.
Vilevile Baraza  limeitaka   Expanded Joint Verification Mechanism ( EJVM) kuchunguza madai ya kuwapo kwa vitendo vya urushwaji wa makombora kuelekea nchi ya jirani ya Rwanda
Katika  hatua nyingine ,  Muwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu  katika DRC. Bw. Martin Koble naye ameelezea kusikitishwa kwake na  tukio hilo  la kuuawa kwa mlinzi wa Amani wa Tanzania.
Akielezea masikitiko  yake,  Bw. Martin Koble anasema, “ mlinzi huyo wa Amani  ameyatoa  muhanga maisha yake  ili kuwalinda wananchi wa Goma. Ninaungana na familia ya  marehemu na walinzi wenzake katika  kombania yake katika kipindi hiki cha majonzi na wakati mgumu”.
Katika mwaka mmoja uliopita, kundi la waasi la M23 pamoja na makundi mengine yenye  silaha mara kwa mara yamekuwa  yakipambana na  Jeshi la Serikali ya  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ( FARD). Ambapo  Mwezi Novemba mwaka  jana kundi hilo la M23 lilichukua kwa muda mji wa  Goma.
Machi  28 mwaka huu , Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa,   lilipitisha azimio la kuanzishwa kwa   Brigedi  Maalum ( FIB)  iliyopewa mamlaka   ya  kuyadhibiti makundi ya waasi yenye silaha yenyewe kama FIB na au kwa kushirikiana na Majeshi ya serikali ya DRC ( FARD).
Kupitia azimio hilo Baraza Kuu la Usalama lilitoa wito kwa kundi la M23 kusitisha  mara moja aina zote za  machafuko ikiwa ni pamoja na kuweka chini silaha zao.

Aidha kwa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa  kuimarisha mamlaka ya MONUSCO pamoja na kuundwa kwa FIB kumelenga katika  kusaidia   utekelezaji wa  malengo ya Mpango Mpana  wa Kisiasa wa Umoja wa Mataifa kuhusu  Amani, usalama na maendeleo katika  DRC na eneo  la Maziwa Makuu.

No comments: