ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 9, 2013

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL ASHIRIKI SWALA YA IJUMAA MSIKITI WA MANYEMA TABORA, MGENI RASMI KATIKA BARAZA LA IID KITAIFA MKOA WA TABORA

Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiwasili kwenye Msikiti wa Manyema Mkoani Tabora, kwa ajili ya kuhudhuria Swala ya Ijumaa kabla kuzungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza kuwahutubia wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora leo, baada ya swala ya Iddi na ya Ijumaa. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza kuwahutubia wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu katika Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora leo, baada ya swala ya Iddi na ya Ijumaa. 
 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu katika Msikiti wa Manyema Mkoani Tabora, baada ya kushiriki nao katika Swala ya Ijumaa, leo kabla kuzungumza katika Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora.
  Makamu wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiongozana na Mufti Mkuu wa Tanzania, Shaaban Bin Simba, wakati wakiondoka katika Msikiti wa Manyema mkoani Tabora baada ya kushiriki katika Swala ya Ijumaa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiondoka katika Ukumbi wa Chuo cha Uhaziri, baada ya kuzumza katika Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora leo
  Sehemu ya waumini wa dini ya Kiislamu waliohudhuria Baraza la Iddi lililofanyika Kitaifa Mkoani Tabora leo. Picha na OMR

HOTUBA YA MHE. DKT. MOHAMMED GHARIB BILAL, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE BARAZA LA EID EL FITR, TABORA, TAREHE 9 AGOSTI 2013
 
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania,
Sheikh Issa bin Shaaban Simba;
 
Mheshimiwa Fatma Mwassa
Mkuu wa Mkoa wa Tabora;
 
Viongozi wa Dini na Madhehebu Mbalimbali;
 
Viongozi wa Mkoa wa Tabora na Mikoa jirani;
 
Katibu Mkuu wa BAKWATA;
 
Wajumbe wa Baraza la Ulamaa;
 
Viongozi Mbalimbali wa BAKWATA;
 
Wageni Waalikwa;
 
Ndugu Waumini;
 
Ndugu Wananchi;
 
Eid Mubarak!
 
Awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kutujalia uzima,  afya njema na kutuwezesha kujumuika hapa siku ya leo kuadhimisha tukio hili  muhimu la kumalizika kwa mfungo  wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
 
Napenda nitumie fursa hii, kutoa shukrani zangu    za   dhati   kwako   Mufti   waTanzania, Shekhe Issa bin Shaaban Simba na uongozi mzima wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), kwa heshima mliyonipa, kunialika kuwa mgeni rasmi katika sikukuu hii muhimu.
 
Aidha niwapongeze wale wote waliojaaliwa kukamilisha ibada hii adhimu, ambayo ni moja ya nguzo kuu katika imani ya dini ya Kiislamu. Kwa wale ambao hawakupata bahati hiyo, tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu awajalie uhai na kuwatunuku fursa hiyo siku zijazo. Rai yangu kwa mlioshiriki ibada hii muhimu ni kwamba; endelezeni mema yote mliyofanya na kuonesha   katika  kipindi chote cha mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Matendo mema yawe sehemu ya utamaduni wa maisha yetu ya kila siku katika jamii. Naamini kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunatekeleza kwa vitendo mafundisho ya Mtume wetu Mohammad (S.A.W) na kujiwekea fungu jema duniani na akhera.
 
Ucha Mungu, upole, adabu, upendo, ustahimilivu na mambo yote mema mliyowatendea ndugu, jamaa na majirani zenu katika kipindi chote cha mfungo wa Ramadhani,   yadumu   na   kuwa   kielelezo  na ushahidi wa imani yenu mbele ya wanadamu wenzenu. Kwa mwislamu mwenye imani ya kweli, kuwajali wenye shida, wajane na yatima, ni ibada muhimu kwa maisha yake ya kila siku, hili halikomi baada ya kumalizika kwa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
 
Endeleeni kujitoa kwa ajili ya wenye shida, salini kwa bidii na kuzingatia mafundisho yote ya Mtume wetu Mohammad (S.A.W) mliyoyapata wakati wa mfungo. Kumbukeni kuwa kumcha Mwenyezi Mungu ni msingi wa  mafanikio  yote  hapa  duniani.   Jamii  ya  watu wacha Mungu ni jamii iliyostaarabika, isiyo na chuki, mifarakano wala ugomvi, zaidi ya hayo; inatii sheria na kuheshimu mamlaka zote zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.
 
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;
Ndugu Waumini;
Ndugu Wananchi;
 
Amani katika Taifa au jamii yoyote, ni sharti la kwanza katika mchakato mzima wa kuleta maendeleo. Mara kadhaa kwa nyakati tofauti, nimepata fursa ya kuzungumza na waumini wa dini   na   madhehebu  mbalimbali  hapa  nchini. Kila nipatapo nafasi kama hii, nimekuwa nasisitiza sana suala la kulinda na kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa Taifa letu.
 
Nafanya hivyo kwasababu naamini kwamba dini na viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kusaidia kujenga maadili mema katika taifa letu. Watu wakishiba imani ndani ya nafsi zao, wakaelewa na kuzingatia mafundisho ya dini zao, ni dhahiri maovu ndani ya jamii yatapungua sana kama si kumalizika kabisa. Sisi katika Serikali, tutapa ahueni kubwa kwani badala   ya    kutenga   bajeti   kubwa   kupanua magereza, kugharamia wafungwa na mahabusu na uendeshaji wa mahakama, rasilimali hizo zitaelekezwa katika mipango mingine ya maendeleo kama vile kuimarisha elimu, huduma za afya, kuboresha miundombinu nk.
 
Napenda kutumia nafasi hii kutoa wito kwa viongozi wa dini na madhehebu yote nchini, kuhakikisha wanatumia nafasi zao vyema kuwaandaa na kuwajenga waumini wao kimaadili, ili wawe raia bora watakaosaidia kudumisha na kuendeleza sifa na heshima ya Taifa letu.
                    
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;
Ndugu Waumini;
 
Nchi yetu kwa muda mrefu imekuwa kisiwa cha amani na utulivu. Jambo hili si kwamba linamfurahisha kila mmoja, wapo wanaotutazama kwa jicho la husda na kutuombea mabaya ili tufike mahali tuharibikiwe ili wao wafurahi. Lakini wakumbuke kuwa ‘dua la kuku halimpati mwewe’.
 
Katika siku za hivi karibuni, yameibuka matukio kadhaa yanaoashiria kutaka kuvuruga amani na utulivu wa Taifa letu. Hujuma hizi                                                                                                                             zinafanywa na watu wachache wasiolitakia mema taifa letu kwa maslahi yao binafsi.
 
Napenda niwahakikishie kwamba Serikali yenu ipo madhubuti na itahakikisha inapambana kwa nguvu zote kudhibiti hujuma zote zenye nia mbaya ya kuchafua sifa  njema ya amani na utulivu wa Taifa letu na kuzuia khofu zisizo za lazima miongoni mwa raia wema. Watanzania tumeishi kama ndugu na Taifa moja kwa muda mrefu na kamwe hatutakubali tunu hii njema ivurugwe     kwa     kisingizio     chochote    kile.
 
Napenda niweke bayana kwamba Serikali yenu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kamwe haitakuwa tayari kuona mtanzania yeyote anaishi kwa khofu na mashaka ndani ya nchi yake kutokana na vitendo vya wahuni wachache.  Kila itakapobidi, tutawasaka, tutawakamata na kuwakomesha kwa rungu la mkono wa sheria. Nawakakikishieni kwamba Tanzania yetu itabaki nchi salama ya amani na utulivu na ya kupigiwa mfano daima.
                    
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;
Ndugu Waumini;
Ndugu Wananchi;
 
Uhuru wa kuabudu katika Taifa letu umejengewa misingi yake ndani ya Katiba yetu. Kutokana na ukweli huo, kila mmoja wetu anapaswa kuheshimu imani au dini ya mwenzake pasi kujiona kwamba imani au dini yake ni bora zaidi. Nawakumbusha tena Watanzania kutokubali kamwe kugawanyika kwa misingi ya dini, kabila, rangi, jinsia au mahala  mtu  alipo  au  atokapo.   Tukatae udini kwa nguvu zetu zote na tusimwonee haya mtu yeyote anayetaka   kutugawa   kwa   misingi   ya udini.
 
Ni busara kwa waumini wa dini na madhehebu yote nchini kujenga utamaduni wa kuvumiliana. Zinapotokea khitilafu ndogo ndogo, kaeni pamoja na kutafuta muafaka kwa njia ya majidiliano ya amani na upendo pasipo kutawaliwa na jazba wala chuki. Tukumbuke kauli na angalizo la Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwamba “Vita ya dini haina mshindi.”
 
Mheshimiwa Mufti wa Tanzania;
Wageni Mbalimbali;
Ndugu Waumini;
Ndugu Wananchi;
 
Kabla sijamaliza hotuba yangu, napenda nipongeze juhudi kubwa zinazofanywa na taasisi na mashirika mbalimbali ya dini hapa nchini katika kusaidia kuboresha huduma za jamii hususan suala la elimu. Kupitia BAKWATA napenda kupongeza mchango mkubwa unaotolewa na taasisi mbalimbali za kiislamu katika    kuimarisha    sekta   ya   elimu   nchini.
 
Katika miaka ya karibuni tumeshuhudia mwamko  mkubwa  kwa  taasisi  hizi kuanzisha shule za msingi, vyuo hadi vyuo vikuu jambo ambalo  sisi  katika  Serikali tunaridhishwa nalo na kuhamasisha kasi zaidi ya kuimarisha sekta ya elimu nchini. Nazidi kuwatia shime Waislamu na dini zingine zote nchini kuongeza kasi zaidi katika kuboresha sekta ya elimu. Tukumbuke kwamba uhai wa Taifa hili na lolote lile duniani utategemea ubora wa elimu inayotolewa leo.
 
Baada ya kusema hayo napenda niwashukuruni tena kwa heshima kubwa mliyonipa pamoja na makaribisho mazuri niliyoyapata mimi pamoja na msafara wangu tokea tulipofika Mkoani hapa. Naomba nihitimishe kwa kuwatakia nyote mliofika hapa, na Watanzania wote kwa ujumla;  EID MUBARAK !
  
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.

No comments: