ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 29, 2013

Serikali yaruhusu mihadhara kwa masharti

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeruhusu waumini wa dini ya kiislamu na kikristo kufanya mihadhara na mikutano ya injili kwa masharti kuwa isiwe na viashiria vya uvunjifu wa amani na ikibainika hivyo viongozi husika watakamatwa na kufunguliwa mashtaka mahakamani.

Waziri wa wizara hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi, akiwakilishwa na Mkuu wa Kitengo cha Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Kamishina Paul Chagonja, alitoa tamko hilo juzi wakati wa kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Kiislamu na wa Umoja wa Wainjilisti wa Kikristo Tanzania (Uwakita).

Kongamano hilo liliitishwa ili kupata msimamo wa serikali kama imepiga marufuku mihadhara kama ilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari (Siyo NIPASHE) wakati wa mkutano wa viongozi wa dini uliofanyika Mei 8, mwaka huu.


“Waziri hajasimamisha mihadhara, bali alisema mihadhara itakayofanyika yenye viashiria vya uvunjifu wa amani viongozi wanaosimamia mhadhara au mkutano wa injili husika wakamatwe na kufunguliwa mashtaka,,” alisema Chagonja.

Kamishina Chagonja alisema Dk. Nchimbi pia aliagiza Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya wafuatilie mihadhara na mikutano hiyo ya mihadhara ya kidini kuona kama inaendeshwa kwa utaratibu mzuri bila kuleta chuki na asiyetekeleza hilo atawajibishwa.

Alisema viongozi wa dini wanapaswa kuzingatia misingi ya amani wakati wa kueneza dini ili nchi iendelee kuwa na amani kwani kwa sasa inakabiliwa na matishio hatari tisa yanayohatarisha kuvunjika kwa amani.

Aliyataja matishio hayo kuwa misimamo mikali ya kidini, misimamo ya kisiasa, mauaji, ajali za barabarani, vita vya wakulima na wafugaji, wawekezaji dhidi ya wazawa, unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto, rushwa na dawa za kulevya.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: