ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 7, 2013

Mwalusako amkana Mkenya Yanga


Lawrance Mwalusako
Lawrance Mwalusako amekana madai ya uongozi wa Yanga kwamba Mkenya Patrick Naggi ambaye wanachama wa klabu hiyo wamemtimua asionekane Jangwani alifika hapo kwa sababu ni rafiki ya katibu huyo wa zamani, na si kwa sababu ni muajiriwa mpya.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, makamu mwenyekiti wa Yanga Clement Sanga alisema klabu yake haijamuajiri Naggi kuwa katibu mtendaji mpya wala kufanya naye mazungumzo yoyote.

"Huyo mtu bado hajaajiriwa na klabu yetu ila ni mmoja wa watu ambao tumeletewa na kampuni moja tuliyoipa kazi ya kututafutia watu kwa ajili ya kuboresha Sekretalieti yetu," alisema Sanga.


Sanga alikuwa akizungumzia tamko la Baraza la Wazee la kumkataa Naggi kama katibu mtendaji mpya wa Yanga wakati si mwanachama hai kama ambavyo katiba ya klabu hiyo inasema.

Alipoulizwa ni kwa nini alionekana kwenye ofisi za klabu hiyo na zaidi alionekana kuingia kwenye ofisi ya Katibu Mkuu, Sanga alisema Naggi alikuja klabuni hapo kwa ajili ya kuangalia mazingira lakini zaidi kwa sababu anafahamiana na Mwalusako.

"Siwezi kuzungumzia kwa ndani kuja kwake hapa klabuni, lakini alikuja kwa utashi wake mwenyewe na ninavyojua wanafahamiana na Mwalusako," aliongezea kusema Sanga.

Hata hivyo, Mwalusako alionekana kukanusha madai hayo baada ya kutakiwa kuthibitisha madai ya uongozi wa Yanga ambao unaelekea kuelemewa na shutuma za wanachama wake.

Ingawa alishindwa kukubali wala kukataa madai ya Sanga, Mwalusako alisema hataki kuingia kwenye malumbano na mtu au klabu.

"Siwezi kubishana na mtu au klabu. Wewe andika kile ulichoambiwa kwenye huo mkutano, kauli yangu mimi inaweza ikaleta mambo mengine," alisema Mwalusako.

"Wewe andika kilichoongelewa kwenye mkutano watu wataelewa."

Sanga alisema kimsingi wazee wa Yanga wana nafasi na uhuru wa kutoa maoni kwa uongozi lakini hawakutumia njia sahihi ya kutoa maoni yao kwa uongozi huo kwa kuzungumza na vyombo vya habari.

Wakiongozwa na Ibrahim Akilimali, wazee wa Yanga walisema Jumatano kuwa wanajua uongozi wa klabu umemuajiri Naggi lakini wao hawamtambui Mkenya huyo kama katibu wao na aondoke mara moja.

Habari za baadhi ya vyombo vya habari jana zilidai kuwa Naggi alifukuzwa kutoka klabuni, Jangwani, juzi baada ya kuonekana tena hapo licha ya kufuzwa siku iliyotangulia.

Wakati Sanga akidai Naggi si muajiriwa wala mtu ambaye klabu imefanya naye mazungumzo, taarifa za kuaminika ambazo Nipashe imezipata zinasema Mkenya huyo yupo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu hiyo.

Naggi amewahi kuwa mchezaji wa kimataifa wa Kenya, kocha, kiongozi wa klabu ya AFC na katibu wa kamati ya ligi kuu ya Kenya pia.

Yanga inatafuta katibu mpya baada ya mkataba wa mwaka mmoja wa Mwalusako kumalizika na kuamua kutomuongeza.
CHANZO: NIPASHE

No comments: