ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 23, 2013

ALIYEMWAPISHA RAIS KENYATTA ATIMULIWA KAZINI

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Kenya, Gladys Shollei amefukuzwa kazi kwa madai ya utovu wa nidhamu na kuwadharau makamishna wa Tume inayosimamia idara hiyo (JSC).

Shollei ndiye aliyemwapisha Rais Uhuru Kenyatta alipoingia madarakani mwaka huu.
Kwenye taarifa ya uamuzi huo iliyosomwa na Jaji Mkuu Willy Mutunga mwishoni mwa wiki, JSC ilitoa sababu tano za kumsimamisha kazi Shollei, ambapo msajili huyo alishutumiwa kwa kukosa maadili.
“Baada ya kusoma madai yote yaliyomkabili msajili mkuu wa mahakama na baada ya kusoma majibu yake, ikizingatiwa kwamba aliamua kujitokeza mbele ya tume, tumeamua kwa pamoja kumsimamisha kazi mara moja,” alisema Jaji Mutunga.
Kwa hatua hiyo, Shollei anakuwa msajili mkuu wa Mahakama wa kwanza kufutwa kazi tangu Idara ya Mahakama ifanyiwe marekebisho ili kuafiki matakwa ya Katiba ya sasa. 

Aidha, ni ofisa wa pili wa ngazi ya juu kwenye idara hiyo kupigwa kalamu, baada ya aliyekuwa Naibu Jaji Mkuu, Nancy Baraza kufutwa mwaka jana.

Akielezea uamuzi huo, Jaji Mutunga alitaja ukosefu wa nidhamu, ukiukaji wa kanuni za kazi za maofisa wa mahakama, ukiukaji wa sura ya sita ya Katiba inayohusu maadili na kukaidi maagizo ya wakubwa wake, kama sababu zilizosababisha JSC kumsimamisha kazi Shollei.

“Kutokana na uzito wa masuala yaliyosababisha kusimishwa kazi kwa Shollei, JSC inaialika Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) ifanye uchunguzi wa kina kuhusu masuala haya,” alisema Jaji Mutunga.

“Madai yaliyotolewa kumhusu Shollei ni mazito sana. Pesa zinazohusishwa katika madai hayo ni Sh2.207 bilioni. Amekubali madai 33 ambapo Sh1.7 bilioni pesa za walipa ushuru ziko katika hatari ya kupotea. Amekataa madai 38 ambayo yanafikia Sh250 milioni ilhali majibu yake kuhusu Sh361 milioni yanakanganya,” alisema.

Jaji Mutunga alisema kuwa JSC imeweka madai yote yanayomkabili Shollei, majibu yake na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na JSC katika tovuti yake.

Mwezi uliopita, Shollei aliiandikia barua JSC akiifahamisha kwamba yuko tayari kufika mbele yake kuanzia Oktoba 15, kujibu madai dhidi yake.
MWANANCHI

No comments: