ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 23, 2013

TUNDU LISSU AKUBALIANA NA TUME

Siku moja baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuomba kuongezewa muda, Mnadhimu wa Chadema, Tundu Lissu (pichani) amesema Tume haijakosea kuomba muda kwani kifungu cha 8 (4) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinaeleza kuwa wanaweza kuomba muda wa miezi miwili zaidi. 
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imeomba kuongezewa mwezi mmoja kukamilisha majukumu yake, ambayo awali ilikuwa yakamilike Novemba Mosi na sasa yatakamilika Desemba Mosi.

Lissu alisema lakini huku akihadharisha kuwa kitendo cha kuongeza muda ni wazi Bunge la Katiba halitakutana Novemba mwaka huu kutokana na mambo ya msingi kutokuwa yamepatiwa ufumbuzi. Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa NCCR- Mageuzi, Samwel Ruhuza alisema hakuna tatizo kwa Tume kuomba kuongezewa muda.

Mkurugenzi wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema hawezi kuzungumza lolote hadi pale atakapolifikisha katika ngazi husika. Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuomba kuongezewa muda, kunaashiria kuna matatizo katika mchakato mzima wa Katiba, licha ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaruhusu tume kuongezewa muda.

No comments: