ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 16, 2013

HAYA NI MAONI YANGU: MAENDELEO NI TABIA

Na Nassoro Basalama
Maendeleo sio halua, kwa kukaa jamvini ukapitishiwa sinia kwa kuchukua pande lako , hapana. Maendeleo hayapatikani kwa kukaa pembeni na kuyaagiza, hapana. Maendeleo kwa kubezana au kunyoosheana kidole, pia sio utaratibu wa kuja kwake .
Msingi wa maendeleo ni ushirikiano wa makusudi na wenye mueleko. Bila shaka panapo patikana ushirikiano katika mazingira yanayokubalika na ushirikiano huu ukadumu, maendeleo hayana budi kuja.
Maendelo ya kifamilia yanaletwa na wanafamilia, maendeleo ya kijamii yanaletwa na wanajamii, vilevile maendeleo ya nchi yanaletwa na wananchi wenyewe. Nikizingatia maendeleo ya nchi, ambayo ndio yamekuwa kero kubwa na la muda mrefu na kwa walio wengi.
Pamoja na kuwa tunaishi katika ulimwengu wa ushirikiano wa kimataifa, ulimwengu ambao ushirikiano unapatikana pia kutoka katika nchi moja na nyingine. Lakini bado ulazimu wa wananchi wenyewe kujenga chachu upo palepale. Wenyenchi wenyewe wasiposhiriki katika usimamizi wa nchi yao, sio jambo la kushangaza kuchelea kukwamuka kimaendeleo. Mifano mingi tumeiona katika Jumuiya zetu za kijamii. Zinapokosa ushirikiano na mwitikio wa kijamii, zinapata mazingira magumu sana ya kujiimarisha.
 Moja katika Kadhia kubwa ambayo tumeiona katika bara zima la Afrika ni maendeleo ya kiuchumi, ikiwemo nchi yetu adhwimu ya Tanzania. Sasa mimi ningependa sana kuzungumzia hapa na watu wake.
Kwa muda mrefu watanzania tumekuwa na tabia ya kukaa pembeni na kulalamika, kukosoa na hata kufundisha. Lakini kwa bahati mbaya, malalamiko haya, makosoo na elimu tunayoitoa, huwa tunaianzisha na kuishimiza humohumo vijiweni. Kwa hakika ustaarabu wa aina hii unakosa wa kumfaidisha. 
Rais Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema: Watanzania wachache wamesoma, lakini wengi sana wanajua. Naamini huu ni msemo wa kubeza, akimaanisha watanzania tuna maneno mengi.
Siku moja nilimuaga rafiki yangu nikamwambia nakwenda sehemu kuna mkusanyiko wa Watanzania, nataka nikafanye uchunguzi wa tabia flani. Nilipofika kwenye kikao hicho, nikaanzisha shutma juu ya Mwalimu Nyerere, juu ya jambo jipya ambalo halijawahi kutokea wala kusikika. Nikasema Mwalimu Nyerere alikuwa na mke wa siri Muisilamu na alizaa naye watoto 7. La kusikitisha ni kwamba katika mkusanyiko ule kila mmoja alichangia kwa upande wake na kusherehesha ufahamu wake wa tukio hilo. Kuna walionikosoa juu ya idadi ya watoto hao, kuna walionitajia mpaka majina ya watoto hao na mengine mengi.
Ninachotaka kusema, maendeleo ni kazi. Kazi ambayo inaanzia kwetu sisi wenyewe, na jambo la mwanzo ni jinsi gani tunavyofikiri na kufanya maamuzi

Wanasema wanafalsafa, unapopenda penda kiasi na unapochukia chukia kiasi. Ukipenda sana utajinyima nafasi ya kuona kasoro na hutoweza kukosoa, na pia ukichukia sana, utajinyima nafasi ya kutambua yaliyo mazuri na hutoweza kushukuru. Inaendele,…….  

2 comments:

Anonymous said...

Sawa kaka mwaga uwazi

Anonymous said...

Bwana Nassoro umeongea sana general. Twambie mtanzania afanye nini hili angalau awe na maendeleo.
Naomba pia uongelee tabia ya kujilimbikizia mali. Hii si kwa vigogo tu bali kwa watanzania wote sababu naamini inachangia kuyumbisha maendeleo.
Kutokuwa waaminifu katika mapenzi? Nayo inachangia kuturudisha nyuma. Ongelea pia rushwa na mchango wake katika maendeleo.
Uvivu...yaani watu kutofanya kazi. Hii iongezee kwenye kujilimbikizia mali na kujituma.
Kutoamini tulichonacho na kuamini vya wageni. Nayo inaturudisha nyuma. Ntafatilia topic yako na kuchangia. Hakika ni nzuri.