Wapo ambao mpaka sasa hawaijui wala hawafurahii ladha ya faragha na wenzi wao. Nazungumza na wanandoa kwa sababu tayari wameshaingia ndani na hakuna rufaa.
Hapa kwenye Let’s Talk About Love nitaandika kwa kutumia lugha ya kirafiki kabisa - kiutu-uzima zaidi ili tusichafue hali ya hewa. Malalamiko yako kwa mwenzi wako hayatasaidia kitu kama hutakubali kujifunza na kubadilika.
Jenga tabia ya kudadisi, jifunze kwa wengine na kwa hakika utabadilika na kuwa mpya kabisa katika ndoa yako.
Vipengele vifuatavyo ni kati ya vile muhimu zaidi, ambavyo kama ukizingatia basi, hutajutia kuingia kwenye ndoa kwani wewe na mwenzi wako mtakuwa wenye furaha sana kila mnapokutana faragha.
MAZINGIRA YAKOJE?
Wapo ambao watatafsiri zaidi ya nilivyokusudia, lakini haidhuru! Nazungumzia maandalizi kwa maana ya maandalizi ya tendo lenyewe. Fanya maandalizi hayo kwa jinsi ambavyo umeelewa neno hili, lakini mimi pia ninayo maelekezo machache ya jinsi ya kufanya maandalizi hayo.
Mwanamke unapaswa kufahamu kwamba, mapenzi ni usafi hivyo basi ni vyema kama chumba chenu kitakuwa katika hali ya usafi na mazingira yatakuwa bora.
Tandika mashuka mazuri, masafi, pulizia manukato mazuri, lakini yawe mepesi na yasiyo na harufu kali.
Weka kila kitu katika mpangilio wa ‘karibu mgeni’, baada ya kuridhika sasa utakuwa umetimiza angalau moja kati ya taratibu muhimu sana za kufurahia tendo la ndoa.
Jiandae kufurahi lakini wakati huo huo tambua kuwa una kazi kubwa ya kuhakikisha mwenzi wako anafurahia tendo hilo.
NGUVU MBADALA
Baadhi ya watu wamekuwa wakieneza propaganda kwamba ukitumia kilevi utakuwa na nguvu zaidi za kufanya tendo la ndoa! Wakati wanaume wakiamini hivyo, wanawake wanaamini kuwa wakitumia vilevi wanakuwa na hamu zaidi na utundu wao unaongezeka!
Hii siyo kweli. Utafiti usio rasmi unaonyesha kwamba, wanaokutana baada ya kutumia vilevi, huwa wanawahi zaidi kufika mshindo kuliko ambao hukutana wakiwa ‘macho makavu’.
Lakini pia, inaendelea kuelezwa kwamba, wanaotumia vilevi huwa wavivu zaidi na huishia kufika mshindo mmoja au miwili tu, kabla ya kugeuka upande wa pili na kukoroma.
Kilevi siyo suluhisho la kufurahia tendo la ndoa. Wako wanaokwenda mbali zaidi, wakidai kwamba eti vilevi vikali ndiyo vinaongeza zaidi kuwafanya wanaume kuwa na nguvu zaidi ya kufurahia tendo hilo na kuwaacha wenzi wao salama, wakiwa wameridhika vya kutosha, jambo ambalo siyo sahihi.
Pamoja na vilevi, kuna ambao wamekuwa wakitumia dawa za kuongeza nguvu /hamu zaidi ya kufanya tendo hilo, hawa ndiyo wanakosea zaidi. Kuuzoesha mwili na dawa ni sawa na kuulemaza au kupunguza nguvu. Inashauriwa na Wataalam wa Afya ya Mapenzi kuwa, ni bora kuzingatia ulaji sahihi wenye mpangilio mzuri kwa ajili ya kuujenga mwili katika tendo hilo kuliko kutumia dawa za kuongeza nguvu ambazo mara nyingi zimekuwa na madhara.
Bado kuna mengi ya kujifunza, wiki ijayo nitakuwa hapa kwa mwendelezo wake, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers.
No comments:
Post a Comment