Mchana mnawasiliana na kila mmoja anataka kujua hali ya mwenzake. Jioni tena mnakutana nyumbani baada ya mihangaiko ya siku nzima.
Kila mmoja ana hamu na mwenzake. Mnapokeana kwa shangwe na kila mtu anamsimulia mwenzake siku yake ilivyokuwa. Mnaijulia hali familia. Mnapata chakula cha usiku, kisha mnalala – siku imekwisha!
Inaendelea hivyo kwa wiki kadhaa. Mko makini, mnasikilizana, wepesi kusameheana na kupeana maelekezo ya namna bora ya kuishi. Ni maisha matamu kiasi gani?
Ingawa hapo nimezungumza kwa upande wa wanandoa zaidi lakini hata kwa wale ambao wapo katika urafiki na uchumba, kuishi kwa amani na kushirikiana kwa kila hatua ndiyo furaha ya uhusiano wenyewe.
Hata hivyo, si rahisi kukwepa kuhitilafiana. Ni jambo la kawaida kabisa. Tatizo ni namna gani ya kumaliza ugomvi pindi unapojitokeza. Kama mtakumbuka, wiki iliyopita nilieleza kwamba, ukiachana na namna ya kumaliza mgogoro pia kauli utakazotoa kwa mwenzako mkiwa katika ugomvi zinaweza kusababisha tatizo jingine jipya.
Unaweza kumwambia au kumjibu jibu ambalo utakuwa umelisema kwa hasira tu lakini kumbe unajisababishia matatizo makubwa siku za usoni.
Wiki iliyopita tuliona baadhi ya kauli za hatari, leo tunamalizia mada yetu. Tuendelee na darasa letu marafiki...
KUHUSU FAMILIA
Muunganiko wa ndoa hutokana na familia mbili. Kila mmoja huko alipotoka, ana upendo mkubwa na ndugu zake. Kama kuna kosa kubwa utakapolifanya mkiwa kwenye ugomvi na mwenzako ni kuisema vibaya familia yake.
Wako wasio na busara hufikia hatua ya kusema: “Kwanza ninyi ni maskini tu. Kukuoa wewe ni kuwasadia matatizo. Hamna shukrani kabisa. Kama siyo mimi, baba yako mpaka leo asingekuwa na gari.”
Mwingine anakwenda mbali anasema: “Nimekuoa wewe lakini ni kama nimeoa familia yenu nzima. Nawahudumia kwa kila kitu halafu na wewe unaniletea mambo ya kipuuzi. Najuta kabisa kukutana na wewe.”
Hizi ni baadhi ya kauli mbaya ambazo hutakiwi kabisa kutamka mbele ya mpenzi wako. Kugundua kuwa huwaheshimu ndugu zake, unawasimanga au unawaona hawana maana kutapunguza upendo wa awali na mwisho unampa wakati mgumu wa kuanza kufikiria suluhisho jingine nje ya ndoa.
Unapogombana na mwenzako, jua unakabiliana naye yeye kama yeye si vinginevyo.
KUHUSU MTOTO/WATOTO
Hapa zaidi wanawake ndiyo huwa na tabia ya kuzungumza maneno yasiyofaa na wenzao wakiwa kwenye ugomvi wakiwataja watoto au mtoto wao.
Ugomvi umekolea kwelikweli, wametupiana maneno ya hapa na pale, lakini ghafla mwanamke anasikika akisema: “Kwanza una uhakika gani kama (anataja jina la mtoto) ni wako? Siri ya mtoto anaijua mama bwana!”
Wanawake wanaotamka maneno haya, huamini kuwa ni adhabu tosha kwa mwanaume wake. Kwa bahati mbaya sana huwa wanajidanganya. Kati ya maneno yanayowaumiza wanaume na kuwakosesha amani ni pamoja na kuambiwa kuwa ‘mtoto si wake’.
Ingawa utakuwa umetamka kwa hasira na pengine ulichukulia kama jambo la kawaida tu, lina athari kubwa sana katika uhusiano na mbaya zaidi utakuwa umetengeneza uhusiano mbaya kati ya mwanao na baba yake.
USAHIHI NI UPI?
Kwanza kabisa unatakiwa kufahamu kwamba, hata kama mna ugomvi mkubwa kiasi gani, siyo mwisho wa uhusiano. Pili, acha kabisa kuchanganya mambo.
Mpo kwenye ugomvi wenu unaohusu jambo fulani, usichanganye mambo. Toa maneno yanayoelezea hilo tu, usiingize mambo ambayo si hoja ya ugomvi wenu.
Kuwa na kiasi lakini utambue kuwa mwenzako ni binadamu ambaye ana maumivu ya moyo ikitokea ukakwazwa. Kumbuka tayari mpo kwenye mgogoro hivyo basi acha kabisa kuzalisha tatizo lingine!
DHIBITHI HASIRA ZAKO
Msingi wa yote niliyoeleza katika mada hii ni hasira. Tuliza hasira zako, zidhibiti. Hasira zinaweza kusababisha ukamkosa mpenzi wako au ukasababisha tatizo lingine kubwa siku zijazo.
Ni vyema kutafuta njia za kutatua tatizo lenu kuliko kuanza kuzungumza maneno makali yanayoweza kuwa shubiri kwako. Iwe umekosa au umekosewa, tuliza kichwa wakati ukitafakari namna ya kuendelea na uhusiano wenu mkiwa na amani.
Wiki ijayo nitakuwa hapa katika mada nyingine, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment