Mwanamke anapohisi kumpenda mwanaume, wapo wanaoamua kusema tu kuwa wanawapenda. Ni hisia za ndani na za kweli lakini vipi kuhusu mapokeo? Habari mbaya ni kwamba, wanaume wengi wakiambiwa na wanawake kuwa wanapendwa, hukubali si kwa sababu nao wanawapenda ila kwa kuwaridhisha tu!
Kuna mambo mawili; kuwa nao kwa ajili ya kuwatumia na kuwaacha au kuwakubali ili wasionekane goigoi. Hili haliwezi kufutika vichwani mwa wanaume wengi kwa sababu ndiyo mfumo na kanuni za maisha yetu sisi Waafrika.
Kwa sababu hiyo sasa, ndiyo maana nikaandika makala haya ambayo kama mwanamke atatumia vizuri vipengele vilivyopo ataweza kumvuta mwanaume husika bila kujiingiza kwenye tatizo la kutumika na kuachwa baada ya muda mfupi. Inawezekana kabisa.
Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza maana na namna ya mwanamke kujiweka katika mwonekano wa kuvutia. Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza kabisa. Mwanamke anapaswa kuwa katika mwonekano nadhifu wakati wote. Tuendelee vipengele vingine.
KUMVUTIA MWANAUME
Hapa ni tofauti kidogo na kipengele kilichopita. Kwanza ni lazima uvutie, lakini sasa hapa tunakwenda mbele zaidi. Umeshamwona mwanaume ambaye ni chaguo lako na kwa bahati mbaya hana ‘time’ na wewe. Uteseke moyoni? Hapana!
Vipo vitu ambavyo ukivifuata, utamsogeza mwanaume huyo na mwisho atakuwa wako. Huna sababu ya kubaki na jakamoyo. Silaha ya kwanza kabisa ni kumjua vizuri huyo mwanaume.
Anaishi wapi? Anafanya wapi kazi nk. Inawezekana ikawa vigumu kidogo kujua kila kitu kwa wakati mmoja lakini angalau ukijua kimojawapo itakuwa sawa, usipojua itakuwa imekula kwako!
Mathalani mnafanya naye kazi au huwa anakuja ofisini kwako/kwenu, mnakutana kwenye mikutano au mnaishi mtaa mmoja nk. Hayo ni mambo ya muhimu kuyajua ili uweze kumweka katika mtego wako.
Mvute kwako. Si kwa kumwambia lakini hata kwa vitendo tu. Vaa mavazi mazuri (naomba kusisitiza hapa mavazi ya heshima) ambayo hayatakutafsirisha kama mwanamke asiye na staha.
Wanaume wengi wanapenda kuwa na wanawake wenye staha na wanaotambua heshima yao. Ukijidanganya na kuvaa mavazi ya kujiachia mwili wako, maana yake atakuchukulia kama mwanamke ambaye hujatulia tu.
Wakati unajaribu kumvutia kwako pia chunguza vitu anavyopenda.
Utaweza kujua kwa kumfuatilia hata kwa kidogo tu. Ukigundua hata angalau mtindo mmoja anaoupenda, mtege nao. Tafuta mbunifu ambaye atakuweka katika mtindo ambao anavutika nao.
Kumbuka ni sumu kumfuata mwanaume na kumwambia kuwa unampenda. Kamwe usianzishe uhusiano wewe. Mwache yeye afunguke mwenyewe. Inawezekana kabisa rafiki zangu.
Ningeweza kuendelea zaidi na vipengele vingine lakini nafasi yangu ni ndogo. Kwa leo naishia hapa, wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers, ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
No comments:
Post a Comment