
Lakini, unafikiri pesa zake kwako zina faida yoyote zaidi ya kukupenda? Je, kama atakuwa akikupa fedha pale unapohitaji na kukutatulia matatizo yako yote lakini hakujali, hayuko karibu na wewe na anakuumiza kila mara, unadhani anastahili kuwa mpenzi wako?
Sijui wewe unasemaje katika hilo. Najua wapo watakaosema pesa kwanza kisha mambo mengine yatafuata baadaye ila wanaofikiria hivyo niwafahamishe tu kwamba, linapozungumziwa suala la mapenzi ya kweli, pesa inakuwa haina nafasi kubwa.
Ninachotaka kukieleza leo ni kuhusu suala zima la uhongaji katika uhusiano na baadhi ya watu kukubali kuingia kwenye uhusiano kwa kufuata pesa na mali. Kuhonga ni tabia iliyoshamiri sana katika jamii yetu. Kipindi hiki siyo wanaume tu, wapo wanawake pia ambao ni mahodari wa kuhonga.
Tabia hii imekuwa ikiwatia majaribuni walio wengi hali ambayo imesababisha baadhi ya watu wenye tamaa za kijinga kushawishika kufanya ngono na watu ambao katika mazingira ya kawaida wasingeweza kushirikiana nao.
Wapo watu wazima ambao kwa tabia yao ya kuhonga, wamewashawishi hata wale ambao ni kama watoto wao kuwapa penzi, hii inakera sana na kwa kweli ni tabia ambayo inawaudhi wengi!
Lakini sasa linapokuja suala la kuhonga, kuna utata kidogo. Hivi ninapompatia mpenzi wangu fedha kwa ajili ya matumizi nitakuwa nimemhonga? Katika uhalisia neno kuhonga ni kitendo cha mwanaume kutoa fedha ama zawadi kumpa mwanamke hasa pale anapomtongoza ili awe mpenzi wake ama mke wake.
Pia katika kamusi ya kiswahili sanifu neno hilo limetafsiriwa kama malipo ama zawadi itolewayo ili kupata kile unachohitaji au kutaka jambo flani liharakishwe, kwa maana nyingine ni rushwa.
Maana halisi ya kuhonga itapatikana kutokana na nia ya mwanaume hasa pale anapotoa pesa ama kitu kingine kwenda kwa mwanamke. Kwa mfano kama unatoa pesa kwa ajili ya kumsaidia mpenzi wako ama kumkidhia haja mke wako kutokana na tatizo fulani alilonalo, hapo haiwezi ikachukuliwa kwamba umemhonga.
Lakini kama unatoa kitu ama pesa kutaka kulazimisha ama kumshawishi awe rafiki yako, mpenzi wako, mke wako ama kwa kutaka kufanya naye mapenzi, hapo itachukuliwa kwamba umehonga.
Kikubwa unachotakiwa kujua ni kwamba, hakuna uhusiano wowote baina ya mapenzi na pesa. Ndiyo maana mapenzi yanaweza kuwepo hata pale pesa inapokosekana.
Kwa kuthibitisha hilo wengi wanaopata penzi kwa njia ya kuhonga, mapenzi yao hayadumu kutokana na mmoja kati ya wawili hao kushawishika kutengeneza uhusiano kutokana na pesa ama kitu kingine.
Utafiti unaonesha kwamba, kwa wanaume walio wengi kuhonga ni sehemu ya maisha yao licha ya kwamba ni katika viwango tofauti.
Niseme tu kwamba, katika uhusiano wa kweli baina ya wawili waliotokea kupendana, suala la kuhongana hakuna. Usimpe mpenzi wako pesa ili kumlainisha akufanyie jambo fulani kwani ipo siku utakuwa huna pesa na unataka akufanyie.
Msaidie pale atakapohitaji msaada wako, kama nilivyowahi kusema huko nyuma kwamba hustahili kuwa mbahili kwa mwenza wako kwani wewe ni yeye na yeye ni wewe.
GPL
No comments:
Post a Comment