ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 15, 2013

Simba, Yanga zatunishiana misuli



Wakati mabingwa wa ligi kuu ya Bara, Yanga jana walitua kisiwani Pemba kwa ajili ya maandalizi ya mechi yao dhidi ya Simba itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa Jumapili, Wekundu wa Msimbazi wakihamisha kambi kutoka Bamba Beach na kwenda Bagamoyo.

Simba walilala 2-0 katika mechi yao iliyopita ya ligi lakini hivi sasa wakiwa na kinara wa kufumania nyavu, Mrundi Amisi Tambwe, hawako tayari kufungwa na kukabidhi uongozi wa ligi kwa Yanga.

Akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kocha msaidizi wa Yanga, Fred Minziro alisema kikosi chake kiliwasili Pemba jana kwa ajili ya kambi hiyo.

Alisema timu hiyo imeamua kupiga kambi visiwani humo ili kukwepa usumbufu, ikiwa ni pamoja na kutaka kuwapa wachezaji nafasi ya kufanya mazoezi kwa uhuru zaidi tofauti wanapokuwa Dar es Salaam.

Alisema timu iliingia Dar juzi ikitokea Kagera ilikoshinda 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na jana asubuhi wakawasili Pemba ambako sasa akili yao iko kwenye pambano hilo la watani wa jadi.

"Timu iko vizuri, wachezaji wote wanaendelea vizuri na mazoezi kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo," alisema na kuongeza kuwa wanatarajia kuwashangaza Simba.
Alisema wachezaji wote sasa wako poa baada ya majeruhi wa muda mrefu Salum Telela naye kurejea mazoezini.

Minziro alisema watakuwa Pemba kwa takribani siku nne kabla ya kurejea Dar kwa ajili ya mechi hiyo.

Hata hivyo, kwa mujibu wa habari za ndani, timu hiyo inapanga kurejea jijini Dar kwa ndege asubuhi ya siku ya mechi hiyo.

Kocha msaidizi wa Simba, Jamhuri Kihwelu 'Julio' alisema jana kuwa Simba ambayo imekuwa kambini Bamba Beach, Kigamboni imehama mahala hapo na kwenda Bagamoyo jana jioni. Julio alisema Yanga watakiona cha moto katika mechi hiyo kwenye Uwanja wa Taifa.

Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo kwa pointi 18 ikifuatiwa na Azam na Mbeya City zenye pointi 17 kila moja. Yanga ni ya nne ikiwa na pointi 15. Hata hivyo, Simba na Yanga zimecheza mechi moja pungufu katika ligi hiyo ambayo imeingia katika raundi ya tisa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: