ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Viwanja wa soka Tanzania si shwari kwa mashabiki

Dar es Salaam. Imebainika viwanja vyote ninavyotumika kwa mechi za ligi mbalimbali hapa nchini havina vifaa vya kisasa vya usalama, hivyo kuwaweka watazamaji katika hatari ya kukabiliwa na mashambulizi ya kigaidi.
Miongoni mwa vifaa hivyo muhimu vinavyokosekana kwenye viwanja hivyo ni kamera maalumu za kurekodia matukio na mashine maalumu zinazotumika kubaini silaha za hatari.
 Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa muda mrefu umebaini kuwa, mashabiki wamekuwa wakiingia viwanjani pasipo kukaguliwa kama wana vitu vyovyote vya hatari.
 Akizungumzia jambo hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, Wallace Karia alisema, hana wasiwasi na suala la usalama kwenye viwanja hivyo kwa vile wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi na lile la Zimamoto.
 Kususiana na kukosekana kwa vifaa hivyo, Karia alisema, hilo ni jukumu la Polisi, hivyo kamati yake haiwezi kuwapangia nini cha kufanya.
 "Kazi yetu ni kuwakumbusha wasimamizi wa viwanja kuhakikisha vifaa muhimu kama gari la wagonjwa vinakuwapo, lakini suala la kuwakagua mashabiki au kufunga kamera ni suala la polisi hivyo hatuwezi kuwapangia utaratibu,"alisema Karia.
 Hata Hivyo, Kamanda wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonjwa alipotafutwa ili azungumzie suala hilo aliwatupia lawama wamiliki wa viwanja hivyo CCM na TFF kwa madai kwamba ndio wenye jukumu na kuhakikikisha vifaa hivyo vinapatikana.
"Sisi mara nyingi tumewashauri wafunge kamera maalumu (mashine ya kubaini vitu vya hatari), lakini hawatekelezi, si kazi ya polisi kuwafungia ni jukumu lao kutambua umuhimu wa usalama wa mashabiki,"alisema Chagonja na kuongeza:
"Hilo ni jambo la hatari sana na nyinyi waandishi mtusaidie kuwaelimisha, ifike wakati waache kuangalia pesa tu inayoingia waangalie pia usalama wa watu,dunia ya sasa haiko hivyo, tumeshuhudia kilichotokea Kenya hawa watu wanataka mikusanyiko ili madhara yawe makubwa."
Mwananchi

No comments: