ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Waomba ajira vinara wa kugushi vyeti vya Veta

Dar es Salaam. Chuo Cha Mafunzo ya Ufundi (Veta) ni miongoni mwa taasisi za elimu za Serikali zinazoongoza kughushi vyeti kwa wanafunzi wanaoomba kazi kupitia Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira kwa Watumishi wa Umma.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Ofisi ya Sekretarieti hiyo, Kasim Nyaki alisema kuwa, watu 517 waliotumia vyeti vya Veta kuomba ajira kupitia sekretarieti hiyo, watu 304 walitoa vyeti halali, lakini watu 213 walighushi.
“Baadhi ya watu walioomba ajira kupitia sekretarieti yetu ambao wamebainika kutumia vyeti vya Veta ambavyo vimeghushiwa, jambo ambalo limeonyesha wazi kuwa, taasisi hiyo ya elimu inaongoza kwa watu kughushi vyeti vyao,”alisema Nyaki.
Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, zaidi ya watu 13,554 walioomba ajira katika kipindi cha miaka mitatu, watu 816 wamebainika kughushi kwa kutumia vyeti vya taasisi mbalimbali iwe ya elimu, vyeti vya kuzaliwa na vinginevyo.
Alisema kuwa, kutokana na hali hiyo, wananchi wanapaswa kuacha tabia ya kughushi vyeti hivyo kwa sababu vinaweza kuwaletea matatizo katika maisha yao.
Hata hivyo, Nyaki alisema kuwa, wanafunzi wanapaswa kusoma masomo ya sayansi ili waweze kupata uhakika wa ajira kwa sababu nafasi nyingi zinazotokana na masomo hayo.
Alisema kuwa, kutokana na hali hiyo, wanapaswa kujijengea utaratibu wa kupenda kusoma masomo hayo ili waweze kupata uhakika katika soko la ajira, jambo ambalo linaweza kupunguza matatizo ya upatikanaji wa ajira za Serikali.
Mwananchi

No comments: