ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 1, 2013

Wassira, Chikawe, Sophia Simba wang`ang`aniwa


  Wadaiwa kumpotosha Rais
  Maandamano nayo yaiva

Bunge. Vyama hivyo vimeungana kupinga mchakato wa katiba baada ya wabunge wa CCM na Mbunge wa TLP, Augustine Mrema kuupitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya katiba wa mwaka 2013 katika Mkutano wa 12 wa Bunge usisainiwe na  Rais kutokana na baadhi ya vifungu kuingizwa kinyemela na pia umehodhiwa na CCM.

Viongozi wa Kamati ya Ufundi ya Ushirikiano wa Vyama hivyo wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam walisema maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo yatakayofanyika Oktoba 10 mwaka huu, yameanza kufanyika baada ya kuwasiliana na viongozi wa mikoa yote.


Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika, alisema wakati maandalizi kwa ajili ya maandamano hayo, viongozi wakuu wa vyama hivyo, James Mbatia, Profesa Ibrahim Lipumba na Freeman Mbowe wataendelea kukutana na makundi mbalimbali kuwaunga mkono kushinikiza muswada huo usisainiwe.

“Tunatambua haki zilizopo katika katiba kwa wananchi kutotii mambo yasiyofaa, tunataka makundi mengine ya kijamii nayo yatumie njia nyingine kupinga muswada huo, akija mtu kwamba tusiandamane hatutatii, hatuwezi kuwatii watu wanaovunja sheria,” alisema.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Ubungo, alisema katika kipindi hiki vyama hivyo havitakuwa tayari kujadiliana na serikali kwa kuwa viongozi wa vyama hivyo walishafanya hivyo Ikulu na bungeni, lakini bado serikali ikaamua kupeleka muswada usiofaa na kuupitisha kibabe bungeni.

Alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano) na Uratibu, Stephen Wassira; Waziri wa Katiba na Sheria, Mathias Chikawe na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba, waache kumtisha Rais kwamba asiposaini muswada huo ataingia katika mgogoro na Bunge.

Aliongeza kuwa mawaziri hao lazima watambue siyo jambo la ajabu Rais kutosaini muswada kwa sababu katiba ya 1977 inaeleza asiposaini anaurejesha bungeni na kutoa maelezo, hivyo utakaporejeshwa hata wabunge wa CCM watashiriki kuufanyia marekebisho.

“Wassira, Chikawe na Simba kama wana hofu kwamba Bunge litavunjwa iwapo muswada utarejeshwa mara tatu wajiuzulu nyazifa zao ili Rais ateue mawaziri wengine watakaosimamia mchakato wa katiba ili isiitumbukize nchi katika machafuko,” alisema.

Mkurugenzi wa Habari CUF, Abdul Kambaya, alisema kauli za viongozi wa serikali wa Tanzania Bara na Visiwani zimevipa nguvu vyama vya CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi kuendelea na mchakato wa kupinga muswada usisainiwe.

Alisema viongozi hao kwa nyakati tofauti wamenukuliwa wakieleza kuwa kuna mapungufu yaliyopo katika muswada huo, ikiwamo suala la kutoshirikisha wananchi wa Zanzibar katika kutoa maoni.

KAULI YA WASSIRA

Waziri Wassira alipotafutwa kuzungumzia tuhuma za kumtisha Rais Kikwete, alisema maoni ya wapinzani hajayaona isipokuwa atakapoyasoma kwenye vyombo vya habari atawajibu kwa kuwa naye ana mdomo.

WAZIRI CHIKAWE
Waziri Chikawe alipoulizwa kuhusiana na kauli za kutakiwa ajiuzulu, alikataa kuzungumza na kumtaka mwandishi amtafute leo. “Magazeti mpaka sasa hivi (jana saa 1:15 usiku), nitafute kesho ofisini,” alisema.

SOPHIA SIMBA
Naye Sophia Simba alisema kauli za wapinzani hazimtishi kwa kuwa hawezi kukaa kimya huku watu wakipotoshwa kuhusu suala la mchakato wa katiba.

Tangu muswada huo upitishwe, kumekuwapo na shinikizo kubwa kutoka kwa vyama vitatu vya upinzani na makundi ya wanaharakati.

Vyama vya CUF, NCCR-Mageuzi na Chadema vimeshaungana kuupinga muswada huo kwamba utaleta katiba mbaya kutokana na mchakato mzima kuhodhiwa na CCM. Wenyeviti wa vyama hivyo, Profesa Lipumba (CUF), Mbatia (NCCR-Mageuzi) na Mbowe (Chadema) wamekwisha kufanya mikutano miwili ya hadhara jijini Dar es Salaam na Zanzibar kwa lengo la kuwashawishi wananchi waupinge mchakato wa katiba.

Kuvunjwa kwa Tume kabla ya kura ya maoni pia ni moja ya hoja zinazotumiwa na upinzani kupinga mchakato wa katiba kwa maelezo kuwa hatua hiyo itasababisha kutokuwapo na mjumbe halali wa Tume wa kwenda kutoa maelezo katika bunge la katiba ikiwa watahitajika kwa kuwa watakuwa wameshapoteza uhalali wa kuwa wajumbe.

Pia muungano huo unapinga muswada huo kwa kuwa haukuzingatia maoni ya Zanzibar kwa kuwa hawakushirikishwa kabla ya kuwasilishwa bungeni.
CHANZO: NIPASHE

No comments: