Thursday, November 21, 2013

JK vunja Baraza la Mawaziri – Ndesamburo

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mkoa wa Kilimanjaro, Philemon Ndesamburo, amesema anaafiki mkakati wa kuwafuta kazi mawaziri wanaokataliwa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kwenda mbali zaidi kwa kumtaka Rais Jakaya Kikwete avunje Baraza zima la Mawaziri.
Ndesamburo, maarufu kama ‘Ndesapesa’ alitoa kauli hiyo jana akiunga mkono kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nauye, aliyetaka Rais Kikwete awatimue baadhi ya mawaziri kwa kushindwa kuwajibika.

Juzi Nape akiwa mjini Songea alimtaka Rais Kikwete kuwafuta kazi Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, Naibu wake, Adamu Malima na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa ambaye ametajwa kuwa sehemu ya matatizo katika kila wizara anayopewa kuiongoza.

Akizungumzia malalamiko ya CCM kulalamikia baadhi ya mawaziri kutowajibika, Ndesamburo alisema kelele hizo huenda zikawa kama mchezo wa kuigiza ili wananchi waone chama hicho kina nia ya kuwawajibisha mawaziri wake.

“Madai ya CCM kutaka Rais Kikwete awafukuze kazi mawaziri wanne wanaotajwa kushindwa kutekeleza majukumu yao ni mazuri, lakini yanaweza kuwa ‘geresha’ dhidi ya umma wa Watanzania.

“Mimi nasema kama CCM inawatakia mema wananchi wake, basi wamtake Rais Kikwete avunje Baraza zima la Mawaziri, kwani wengi wamechoka,” alisema Ndesamburo.

Akitolea mfano Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Ndesamburo alisema ni mzigo kwa taifa kwani haina mpango wa dhati kwa wakulima wanaotegemea jembe la mkono, wakati huo huo wakishinikizwa kuuza mazao yao kwa bei ya chini kwa walanguzi.

Mbunge huyo aliwatahadharisha Watanzania kwamba kauli hiyo ya CCM inaweza kuwa na nia ya kutafuta huruma ili kishinde kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani.

Alisema Rais Kikwete anapaswa asingojee fedheha nyingine itakayotokana na shinikizo la wabunge ama watendaji wakuu wa CCM na kasi ya CHADEMA katika kufanya uamuzi huo.

Alisema ni vema Rais Kikwete angewaondoa mawaziri hao mapema badala ya kusubiri upepo wa wabunge wake na nguvu ya CHADEMA.

No comments: