Sunday, November 24, 2013

Kampuni yakamatwa kwa wizi wa maji ya milioni 24/-

Kampuni ya RP Construction imekamatwa na Kampuni ya Majisafi na Majitaka (Dawasco), kwa kujiunganishia maji kinyume na sheria huku ikiingiza hasara ya Sh. milioni 24.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Jangwani jijini Dar es Salaam jana, Meneja wa Dawasco Kanda ya Magomeni, Peter Chacha, alisema wameikuta kampuni hiyo ambayo ni moja kati ya makampuni yaliyo na mkataba na Kampuni ya ujenzi ya Strabag inayojenga barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (DART). Alisema kampuni hiyo inajishugulisha na ujenzi wa mabomba.

Chacha alifafanua kuwa Dawasco itatoa taarifa hizo polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni hiyo, ikiwa ni pamoja na kumlipisha fedha hizo.

Meneja Uhusiano wa Dawasco Ever Lyaro alisema kuwa tukio hilo linafuatia operesheni maalum inayoendeshwa na kampuni yake kwa watu wote ambao wamekuwa wakiiiba maji kwa kujiunganishia kinyume cha sheria.

Lyaro aliongeza kuwa waameshangazwa na tukio hilo kwani hawakutegemea kampuni kubwa kama hiyo ingejiunganishia maji kinyume cha sheria, kwani wamezoea kuwaona wananchi wa kawaida wakifanya hivyo.

Lyaro alionyesha wasiwasi wake kuwa kampuni hyo huenda ilikuwa inafanya hivyo toka ilipoanza ujenzi wa barabara hiyo, kwani kwanza walikuwa wananunua maji kutoka kwenye maboila kwa Sh 150,000 lakini baadae wakaacha labda kwa kuona wanaingia gharama kubwa.

Lyaro aliendelea kufafanua kuwa bomba hilo ambalo ambalo kampuni hiyo imekutwa ikiwa imejiunganishia kinyemela ni bomba ambalo linapeleka maji katika maeneo ya katikati ya jiji pamoja na hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).

Meneja Mradi wa Kampuni ya Construction Hans Staubhman alisema kuwa aliamua kujiunganishia maji kinyume cha utaratibu kwa kuwa alikuwa anafanya hivyo kwa majaribio tu lakini siyo kwa lengo la kuiba.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: