Sunday, November 24, 2013

Mwanamke akwaa kamati nyeti TFF

Lina Kessy

Rais wa shirikisho la soka, Jamal Malinzi amemteua mwanamke kuwa mjumbe wa kamati nyeti ya TFF wakati akitangaza kamati mpya jijini jana.

Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika jana, Malinzi alisema mwenyekiti wa chama cha soka cha wanawake Lina Kessy ni mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango.

Lina ambaye chini yake Twiga Stars, timu ya taifa ya wanawake, na soka la wanawake kwa ujumla vimepiga hatua kubwa kimataifa, ni mwanamama pekee katika kamati hiyo ya watu tisa.

Wajumbe wengine wa Kamati ya Fedha na Mipango ni Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia ambaye ni mwenyekiti, Francis Ndulane (makamu mwenyekiti), Omari Walii, Eliud Mvella, Said Muhammed, Geofrey Nyange, Kidao Wilfred, Ayoub Nyenzi na Cyprian Kuhyava.

Aidha, Malinzi alitangaza wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji aliowateua kwa mujibu wa katiba ya shirikisho ambapo amemrudisha TFF mgombea wa nafasi ya makamu aliyeshindwa na makamu wa pili wa awamu iliyopita, Ramadhan Nassib.

Mjumbe mwingine wa kuteuliwa wa Kamati ya Utendaji ni mwanasheria Richard Sinamtwa, alisema Malinzi na kueleza zaidi kuwa Dk. Paul Marealle na Saloum Umande Chama wanaingia moja kwa moja kwenye kamati ya utendaji kutokana na kamati wanazoziongoza.

Dk. Marealle anaongoza Kamati ya Tiba wakati Chama ni mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi.

Mbali na kuwa mjumbe wa Kamati ya Fedha na Mipango, Lina ataongoza Kamati ya Mpira wa Miguu wa Wanawake, alisema Malinzi na kuwataja wajumbe wake kuwa ni Shyrose Bhanji (Makamu Mwenyekiti) na Zena Chande.

Wengine ni Amima Karuma, Dk. Cecilia Makafu, Zafarani Damoder, Beatrice Mgaya, Sofia Tigalyoma, Martin Mung’ong’o na Engrid Kimaro.

Baada ya kuwa mjumbe maalumu wa TFF, Sinaitwa ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji huku Moses Karuwa (Makamu Mwenyekiti), Zacharia Hanspoppe, Hussein Mwamba, Philemon Ntahilaja, Abdul Sauko na Imani Madega ni wajumbe.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: