ANGALIA LIVE NEWS

Monday, November 4, 2013

LOWASSA AMPIGA DOGO KIKWETE ASEMA NCHI HAINA VIONGOZI JASIRI BALI WALALAMIKAJI

KIGUGUMIZI cha serikali ya Rais Jakaya Kikwete katika kuchukua uamuzi mgumu kwenye masuala mazito kimemwibua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, akisema nchi inakosa viongozi jasiri wenye kusimamia utekelezaji wa mambo waliyoamua katika sekta mbalimbali.

Alisema nchi ina tatizo kubwa la uswahili mwingi wa kukaa kutekeleza kile kinachotakiwa kufanyika kiasi cha kuwafanya kila mtu kuanza kulalamika.
“Hapa mnaamua bila kutekeleza, watu hawana ujasiri wa kufanya maamuzi magumu, ni lazima awepo mtu mmoja wa kuamua si wote kulalamika lalamika.
“Tukishakubaliana mambo ni lazima yafanyike. Ni lazima tuondokane kuwa nchi ya kulalamika kuanzia kiongozi wa juu mpaka mwananchi,” alisema.

Lowassa aliyasema hayo jana bungeni wakati Bunge lilipokaa kama Kamati ya Mipango ili kujadili Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2014/16.

Lowasa ambaye ni mbunge wa Monduli (CCM) alisema kuwa ni vema serikali ingekuwa na mipango michache yenye kutekelezeka na tija kwa taifa.

Aliongeza kuwa kama angekuwa kiongozi wa serikali angejikita kwenye vipaumbele vitatu ambavyo ni ajira, Reli ya Kati na elimu kuliko kuwa na vipaumbele vingi visivyotekelezeka.

Alibainisha kuwa tatizo kubwa linaloifanya serikali ishindwe kufanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali ni kujiwekea vipaumbele vingi huku rasilimali zake zikiwa chache na wakati mwingine zile zinazopatikana hazitumiwi vizuri.

“Vipaumbele vingi mno utekelezaji wake ni tatizo, tungechagua vichache, tukavisimamia na tuvitekeleze. Tukiwa navyo vingi kwa wakati mmoja hatuwezi kuvitekeleza vyote, tuanze na vichache tukivimaliza tunavifuata vingine.

Ajira

Alisema kama angekuwa kiongozi wa serikali angeanza na kipengele cha ajira ambacho kinakwenda sambamba na mipango.

“Huwezi kupanga bila kuzungumza habari za ajira, tukiri kuna Watanzania wengi wamemaliza kidato nne, sita, chuo kikuu, vyuo, darasa la saba walioko mitaani hawana ajira.

“Tusipowashughulikia, watakula sahani moja na sisi, tusipoangalia yatatufika yale ya wenzetu ya Afrika Kaskazini, si lazima yatufike lakini hawa wasio na ajira watakula sahani moja na sisi,” alisema.

Lowassa aliongeza kuwa wanapaswa kuangalia suala la ajira kwa umakini sana, kwamba inawezekana sana kila mmoja akifanya wajibu wake.

Alibainisha kuwa nchi ya Hispania ilikuwa na tatizo kubwa la ajira mara baada ya kutokea kwa mdororo wa uchumi duniani lakini walikaa chini na kuamua kulitafutia ufumbuzi.

“Wale wenzetu waliamua kila mwekezaji anayekwenda kwao sharti kubwa ni lazima atoe ajira kwa vijana, baada ya miaka miwili walipiga hatua kubwa sana, lazima tuliangalie suala hilo kwa umakini mkubwa sana,” alisema.

Lowassa aliwapongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatuma Mwasa na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Elibariki Kingu kwa kuamua kuangalia suala la ajira kwa vijana.

Alisema viongozi hao wamethubutu kwa kuwachukua vijana waliomaliza chuo kikuu na kuwapa matrekta na kuwatafutia ardhi ya kilimo ambapo hivi sasa wanaendesha shughuli zao vizuri.

Aliongeza kuwa Benki ya CRDB nayo imeanza kutoa mikopo kwa vijana wanaomaliza vyuo vikuu kwa kuchukua vyeti vyao kama dhamana.

“Wizara, watendaji na viongozi mbalimbali kila mtu angetimiza wajibu wake katika hili jambo nina hakika tatizo la ajira lingepungua kwa kiasi kikubwa,” alisema.

Elimu

Alisema mjadala wa elimu usipuuzwe kwa kuwa lipo tatizo la msingi katika elimu ya Tanzania na hatua zinazochukuliwa hazitoshi.

Aliongeza kuwa alitegemea ripoti ya tume iliyoundwa na Waziri Mkuu kuchunguza matatizo ya elimu hapa nchini ingetolewa bungeni na ikajadiliwa ili wabunge wajue matatizo yaliyopo na namna ya kuyatatua.

“Haitoshi kuchukua wanafunzi wengi kumaliza chuo kikuu wakati akienda kwenye soko digrii anayoipata haifai, hawezi kupata kazi kwa kuwa aina ya elimu aliyoipata haimuwezeshi kuajiriwa.

“Wenzetu Ujerumani wanagawa digrii nusu inatokana na ujuzi wa kitu fulani na nusu iliyobakia inatokana na elimu aliyoipata hivyo kila kundi hapa lina uhakika wa ajira,” alisema.

Alisema kelele zinazopigwa na wananchi juu ya matatizo ya elimu zinapaswa zisikilizwe na uitishwe mjadala wa jambo hilo ili Tanzania isiachwe na jumuiya mbalimbali ikiwemo ile ya Afrika Mashariki.

“Tukiacha mambo haya yaendelee kwenye elimu yetu tutakuwa wababaishaji na tutaachwa katika soko la ajira duniani,” alisema.

Reli ya Kati

Alisema kipaumbele chake kingine ni kuboresha reli ya kati ambayo itachangia kupunguza uharibifu wa barabara zinazojengwa kwa gharama kubwa na serikali.

Lowassa alimpongeza Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa barabara ambazo hivi sasa zimekuwa zikiharibika kwa kiwango kikubwa kutokana na magari kupitisha mizigo mikubwa.

“Maroli yaliyopaswa kusafirishwa kwa treni hivi sasa yanasafirishwa kwa magari, hapa ni lazima barabara ziharibike, naomba muangalie kwa haraka sana Reli ya Kati,” alisema.

Lowassa pia alimpongeza Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harisson Mwakyembe, kwa jitihada za kutafuta ufumbuzi wa foleni za jijini Dar es Salaam ambazo zinachangia kuzorotesha ukuaji wa uchumi.

“Foleni Dar es Salaam it’s a nightmare (jinamizi), muda tunaokaa katika foleni ukiujulimsha ni mrefu sana serikali ni lazima mchukue hatua sasa, si suala la kusubiri,” alisema.

Afrika Mashariki

Lowassa aliitaka serikali kuacha kugombana na marais wa Rwanda, Paul Kagame, Uhuru Kenyatta (Kenya), Yoweri Museveni (Uganda) ambao wameamua kushirikiana na Sudan katika masuala mbalimbali.

Asema Tanzania ijielekeze zaidi kuimarisha ushirikiano na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo ambako kuna manufaa makubwa zaidi.

Sumaye kufunguka

Wakati huo huo, Waziri Mkuu mstaafu wa Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, ambaye ni mmoja wa watu wanaotajwa kuutaka urais mwaka 2015, leo anakutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuanika kile kinachoelezwa kuwa ni mchezo mchafu unaofanywa na mahasimu wake.

Hatua ya kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), inafuatia tukio la hivi karibuni akidai kuhujumiwa katika mwaliko aliopewa na vijana wa asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha kuelimisha jamii kuhusu usalama na amani (Public Terrorism Awareness Trust Fund and Human Welfare (PTA-HW).

Asasi hiyo iliandaa tamasha Jumapili iliyopita jijini Dar es Salaam na kumwalika Sumaye kuwa mgeni rasmi lakini katika mazingira ya kutatanisha saa chache kabla ya shughuli hiyo iliyofanyika viwanja vya Mnazi Mmoja kuanza, aliarifiwa kuwa imeahirishwa na kwamba atataarifiwa tarehe nyingine itakayopangwa.

Hata hivyo, katika hali isiyoelezeka muda mfupi baadaye maandamano ya vijana hao yaliwasili katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kupokewa na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Wilaya ya Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi.

Dalili za waziwazi za mgawanyiko miongoni mwa waandaji zilijitokeza baada ya kuwasili kwa Karamagi ambaye hakuwa ametarajiwa na waandaaji pamoja na washiriki wa tamasha hilo.

Kwa muda mrefu sasa Sumaye amekuwa akidai kuhujumiwa na wapinzani wake wanaomhofia katika mbio za urais mwaka 2015 ambapo katika Uchaguzi Mkuu wa CCM mwaka jana alidai kuchezewa rafu ya rushwa.

Tanzania Daima

2 comments:

Unknown said...

Lowasa for change. Yes u can sir. Huyo raisi wa sasa m'babaishaji safari nyingi za nje ya nchi mafanikio zero. Kura yangu na vijana wenzangu inakuhusu muheshimiwa.

TANZANIAN PATRIOT said...

Bw.Lowssa IS NOT a solution kwa matatizo ya Taifa letu. Mifano anayoitoa ya kuilinganisha Tanzania na Spain au Germany haileti maana au akili, kwa maana nchi hizo zimeendelea (developed countries) wakati sisi tupo bado katika developing stage (developing country. Hata naye ni mlalamishi maana anataka tufuate strategies za nchi ambazo kimaendeleo zipo mbali sana. Vile vile, inasikitisha kuona Lowassa akiilaumu nchi yetu ya Tanzania kwa hujuma zinazofanywa na Kenya, Rwanda, na Uganda dhidi yetu katika Jumuiya (EAC). Which side are you Mr. Lowassa? Are you an AGENT for those countries? Wanakulipa ili uwatete kwa yale ambayo wanayoifanyia Tanzania?Wasomi wengi nchini na ughaibuni wamesikitishwa na uhasama wa hao majirani, na wanaomba na kuishauri serikali ili tujitoe na hiyo Jumuiya. Haina faida kwa nchi yetu, simply because in the long run, Tanzania itajikwamua na kuendelea vyema. Tumetoka mbali bila wao na tutasonga mbele bila wao! Ni muhimu tuukuze ushirikiano wetu na nchi marafiki za SADC, na kuwakaribisha DRC na Burundi kwa mikono miwili. Unfortunately, Lowassa has shown his true colors, and his patriotism is questionable. Watanzania tuwe makini, tusiruhusu watu kama Lowassa kugombea Urais 2015, wataiuza nchi yetu. Afterall, nani anataka kusikia RICHMOND scandal part 2?