Friday, November 22, 2013

MAHABA NIUE NI MATOKEO YA KUKOSEA VIPIMO VYA MAPENZI JIPANGE NA UJUE UNACHOKITAKA NDANI YA PENZI HADI NDOA


KATIKA siku za hivi karibuni nimekuwa nikisikia msemo; “mahaba niue.” Kutokana na kazi yangu ya kila siku ya kuandika makala zinazotoa muongozo na ushauri kuhusu uhusiano wa kimapenzi, nikafuatilia kujua tafsiri ya hayo maneno.
Nikajua kwamba kwa mujibu wa inavyozungumzwa, maana yake ni uhusiano unaoundwa na mtu ambaye a naona mapenzi ni kila kitu kwake. Inapotokea hana maelewano mazuri na mwenzi wake, basi atahisi kufakufa. Moyo wake hukosa kichocheo chenye faraja mbadala.
Akiambiwa na mwenzi wake waachane, badala ya kuyapima maneno hayo, yeye anakwenda mbali kwa mawazo. Hupaswi kumuwaza mtu ambaye hakupendi, badala yake unapaswa kuwa umeshampima na kupata majibu kuwa hakufai. Usikubali mahaba yakuue.

Kila siku ninashauri watu wayaheshimu mapenzi. Hii ni kwa sababu yenyewe ndiyo huamua furaha na utulivu wa akili na mwili. Vilevile yanaweza kukupa nguvu ya kutekeleza majukumu yako ya kila siku kwa kiwango cha hali ya juu. Yakiutonesha moyo wako, ni ulemavu mkubwa.

Pamoja na heshima, leo naomba nikushauri kwamba ni lazima ujenge kiburi kwa mtu ambaye unamuona hakupendi. Haeleweki, kila siku anakuingiza kwenye mawazo na maumivu ya moyo. Huyo hupaswi kuumiza moyo kwa ajili yake. Unapaswa ‘kum-scan’ halafu ‘um-delete’ haraka.

Huyo ni kirusi hatari kwenye maisha yako. Angekuwa wako angekujali na kuthamini upendo wako. Unapoona hasikilizi shida zako wala kujali maumivu unayoyapata kutokana na jinsi yeye anavyokutenda, unachotakiwa kufanya ni kumbadili kutoka mpenzi hadi kuwa rafiki mnafiki.

Ila usimgeuze kuwa adui, itakuumiza wewe. Mfanye kuwa rafiki mnafiki kwa maana unamuacha aje, unazungumza naye huku ‘unamuinjoi’. Ikiwezekana unamuonesha tabasamu la kinafiki lakini ndani yako unakuwa umeweka kizuizi cha yeye kukujua kwa undani.

Zingatia kanuni moja kwamba rafiki mnafiki hapaswi kujua maumivu yako. Kinachokutesa, hutakiwi kukiweka wazi kwake. Ukithubutu kufanya hivyo, utakuwa umempa sababu ya yeye kwenda kujisifu kwa watu wa pembeni. Cheka naye kisayansi, mwache akuchunguze lakini hakikisha anaambulia sifuri.

Mwache apate majibu chanya kutoka kwako. Hakikisha siku zote anakuona mtu mwenye furaha na mchangamfu. Anapobaini huna raha, kwake anakuwa ametimiza malengo yake, kwa hiyo atakaa na ‘mabazazi’ wenzake kujisifu kwamba amekeweza.
Itaendelea wiki ijayo.

Hujui huyo anayekutenda malengo yake ni nini. Sasa basi, kama dhamira yake ni kukuumiza na unapomuonesha kwamba kweli umeumia, unakuwa umemfanya ajione amefanikiwa. Hii ndiyo sababu ya mimi kukutaka usikubali kuonesha udhaifu wake kwake. Atakwenda kuwakenulia wenzake.

Hata kama una moyo mdogo mpaka unaingia kwenye kundi la akina “mahaba niue”, hakikisha udhaifu huo rafiki mnafiki hauoani. Lia ndani peke yako, akitokeza jikaushe. Akikuuliza mbona macho mekundu? mjibu ulikuwa umelala kisha tabasamu halafu mwambie, “usijali sweetheart, lete stori nyingine.”

Ni falsafa ya kukuwezesha kupata alama A kwenye mapenzi. Kama ambavyo kanuni inakwambia usimuoneshe adui yako udhaifu ulionao, ndivyo ambavyo na rafiki mnafiki unavyotakiwa kumkabili. Hakupendi, kwa hiyo siyo mtu mwema kwako, anakucheza shere, hana tofauti na adui.

Kwa faida yako, uimara wako kwa mwenzi ambaye haoneshi kukujali, unaweza kumbadili kutoka alipo hadi kuwa mpenzi bora wa maisha yako. Atabadilika pale tu atakapogundua kwamba wewe ni mtu makini na huhitaji kuchezewa.

Atabadilika pale atakapogundua kuwa wewe ni moyo wa chuma. Mwenye malengo ya kukucheza shere halafu akakutana na kisiki cha mpigo, humfanya afikirie mara mbili, fikra hizo humzalishia mawazo, anapokuwaza sana mwisho huumia. Unaona sasa, alitaka kukuumiza lakini kaumia yeye.

Maumivu anayoyapata ndiyo yatakayomfanya ajirudi. Atakuheshimu na mwisho atakuonesha upendo wa dhati. Sasa wewe shika hili, anapoanza kukuonesha upendo, upime kwa makini wake halafu jiridhishe kama kweli ana vigezo vya kumfungulia moyo.

Sikushauri ukimbilie kumuacha mpenzi asiyeeleweka, kwani inawezekana akawa ndiye mpenzi bora ila anusumbuliwa na tu na mapepe. Siku zote usilaumu uhusiano, tambua kwamba mpenzi mzuri atakupa furaha ya maisha na mpenzi mbaya ni changamoto ya kukupa uzoefu.

Zingatia kwamba wewe unaweza kumbadili mpenzi asiyeeleweka mpaka kuwa mpenzi muwajibikaji.

No comments: