Sunday, November 24, 2013

Majambazi yateka magari 15 na kupora abiria

Kundi la watu wanaosadikiwa kuwa majambazi wakiwa na silaha za kivita limeteka magari zaidi ya 15 yakiwemo ya abiria na kupora mali, wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Tukio hilo lilifanyika jana kwa nyakati tofauti baada ya tukio la kwanza kutekwa magari mawili ikiwemo Toyota Hiace iliyokuwa ikitokea Munzani wilayani Biharamulo kuelekea wilayani Kahama majira ya saa 2:10 asubuhi na jingine likitokea majira ya saa 9 alasiri.
Habari kutoka polisi wilayani Biharamulo, zilidai kuwa zaidi ya magari 15 yakiwemo ya abiria yalitekwa na majambazi hao kwa siku moja kisha kupora mali mbalimbali zikiwemo fedha kabla ya kutokomea kwenye msitu wa hifadhi ya Biharamulo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, Henry Mwaibambe, alisema taarifa alizonazo ni malori matano yaliyotekwa na majambazi waliokuwa na silaha wanaosadikiwa kuwa na idadi ya watu watano ambao hata hivyo hawakujeruhi mtu. 
Kwa mujibu wa Mwaibambe, polisi walifika eneo la tukio na kupambana na majambazi hao kwa kurushiana risasi kwa dakika zipatazo 20 na baada ya kuona yameelemewa yalitokomea msituni na kuacha baadhi ya vifaa vyao.
Alisema baada ya kuyafuatilia msituni humo walifanikiwa kuona michirizi ya damu inayohofiwa kuwa ilitokana na majeraha ya risasi walizoyashambulia mfululizo.
Hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo na polisi inaendelea na msako. 
Mwaibambe alisema katika mapambano hayo, polisi walitupa bomu la mkono lililotoa mshindo mkubwa na kusababisha mshituko kwa dereva wa lori lililokuwa likipanda mlima ambaye alilazimika kurudi nyuma na kusababisha kuanguka mtaroni.
Akizungumza na NIPASHE katika hospitali teule ya wilaya ya Biharamulo, Shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni majeruhi, Gidion Shango, alisema majambazi hayo yalikuwa saba yakiwa na silaha za kivita na wengine wakiwa porini na pinde na mishale. 


CHANZO: NIPASHE

No comments: