Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo
Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imebatilisha uamuzi wake wa kubadili mfumo wa upangaji wa madaraja ya ufaulu kwa mitihani ya kidato cha nne kama ilivyotolewa awali kwa kurudisha daraja sifuri.
Kutokana na uamuzi huo, sasa daraja la tano lililotangazwa wiki iliyopita kuchukua nafasi ya daraja sifuri sasa limefutwa.
Uamuzi huo umetolewa siku nne baada ya wizara hiyo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Profesa Sifuni Mchome, kutangaza kuwa serikali imeamua kubadilisha mfumo wa kupanga alama na madaraja ya ufaulu.
Uamuzi wa kushusha alama za ufaulu ulipokewa kwa hisia tofauti na wadau wa elimu nchini ambao walikosoa mfumo huo kwa kueleza kuwa unaipeleka kaburini sekta ya elimu ya Tanzania.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo akizungumza na NIPASHE jana kwa njia ya simu kutoka Dodoma, alisema baada ya kutafakari serikali imeamua kuondoa daraja la tano kama ilivyokuwa imetangaza awali na kurejesha daraja sifuri.
“Kwanza niwaombe radhi Watanzania kwa mkanganyiko huo uliojitokeza ambao ni jambo moja tu limewachanganya, lakini walio wengi wanapongeza mfumo huu wa madaraja, tulichokuja kuharibu ni ‘statement’ ya neno division five,” alisema.
Mulugo aliwahakikishia Watanzania kwamba daraja la tano halitakuwapo bali kutakuwa na daraja la kwanza, pili, tatu, nne na sifuri kama ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, alipoulizwa kama watendaji wa wizara hiyo walitoa wapi neno daraja la tano wakati wakitoa taarifa kwa vyombo vya habari, alisema suala hilo hawezi kulieleza, lakini jambo la msingi ni kwamba daraja hilo halitakuwapo.
Kuhusu madai ya wananchi kwamba viwango vya ufaulu vimeshuka, alisema: “Siyo kwamba serikali imeshusha viwango vya ufaulu isipokuwa imepanua wigo wa kufaulu.”
“Mambo ya kitaaluma wananchi wangeacha kwa sababu mfumo huo siyo kwamba unatumika Tanzania peke yake, lakini watu wanakosoa tu utafikiri watu waliopo wizarani wamekaa tu hawajui lolote, ni vizuri wananchi wakatuamini,” alisema.
Wiki iliyopita wizara hiyo ilitangaza mfumo mpya wa usahihishaji wa mitihani kwa kushusha alama za ufaulu. Aidha, mfumo wa upangaji wa madaraja umebadilika kwa kushusha viwango vya alama.
Profesa Sifuni Mchome alisema uamuzi huo umetokana na maoni ya wadau wa elimu kuhusu upangaji wa viwango vya alama katika mitihani kwa kidato cha nne na sita na kwamba utazingatia matumizi ya alama za tathmini ya maendeleo ya mwanafunzi (CA) na kuamua kiwango cha ufaulu wa mwanafunzi.
Awali Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) lilitumia alama A, B, C, D na F huku alama A ikianzia maksi asilimia 81-100, B= 61-80, C=41-60, D= 21-40 na F 0-20. Aidha kulikuwapo na madaraja ya l, ll, lll, lV na 0.
Kwa mujibu wa mabadiliko hayo, alama zitashuka na sasa itakuwa ni alama A itakuwa ni 75-100; B+ 60-74; B 50-59; C 40-49; D 30-39; E 20-29 na F 0-19.
Alama A itahesabika kuwa ni ufaulu uliojipambanua, B+ ufaulu bora sana, B ufaulu mzuri sana, C ufaulu mzuri, D ufaulu hafifu, E ufaulu hafifu sana na F ufaulu usioridhisha.
Alisema kuanzia mwaka huu kiwango cha pointi za kupanga madaraja kimeshushwa. Daraja la kwanza litaanzia pointi 7 hadi 17, daraja la pili 18-24, daraja la tatu 25-31, daraja la nne 32-47 na daraja tano 48-49 sasa itakuwa sifuri.
Muundo wa madaraja wa miaka ya nyuma ulikuwa pointi 7-17 kwa daraja la kwanza, 18-21 daraja la pili, 22-25 daraja la tatu, 26-33 daraja la nne na 34-35 daraja la sifuri.
Alisema kuanzia sasa CA ya mwanafunzi katika masomo yake ya darasani yatatumika kupanga kiwango cha ufaulu katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa sekondari na kwamba yatachangia kwa asilimia 50 kwa Tanzania Bara.
Kwa upande wa Zanzibar CA ni asilimia 40 ya matokeo huku mtihani wa mwisho ikiwa utachangia kwa asilimia 60.
Alisema mkakati huu ni moja ya mikakati katika kuleta tija kwa ‘Matokeo Makubwa Sasa’(BRN), na kwamba muundo wa matokeo kwa shule za sekondari hapo baadaye utatolewa kwa wastani (GPA).
Katika hatua nyingine, serikali imeagizwa kupeleka Bungeni mabadiliko ya viwango vya madaraja ya matokeo ya Kidato cha Nne yaliyotangazwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi hivi karibuni ili kuondoa mkanganyiko uliopo.
3 comments:
hivi hawa watu wanafanya reaseach kabla hawajatangaza mahamuzi yao au wanakurupuka. tuta endelea vipi kama viongozi hawajihamini. hii inaonyesha jinsi gani hawana uwezo wa kutupeleka next step forward. inasikitisha.
Mulugo na Wantanzania wa fikira finyu kama zake wanasisitiza Divion Sifuri kama adhabu ya kumtesa akili na kisaikolojia mtoto mhanga ambaye wanaomsababishia sifuri ni watu hao hao aina ya Mulugo. Mtoto ambaye amehudhuria madarasa yote kila siku katika miaka yake ya sekondari kuna kiasi Fulani cha maarifa ambacho anakuwa amekipata ambacho hakistairi kubatizwa SIFURI. Jina la "Divion V" ndilo muafaka. Basi tu Watanzania tunapenda sana kutumia maneno makali ya kuumiza watu ambao tayari wameumizwa na kupigika kutokana na mfumo wa utawala. Tunashabikia maneno makali kama vile 'wahamiaji haramu' (utamwitaje binadamu mwenzako haramu?), mtoto kaambulia SIFURI (sasa miaka yote minne alikuwa anafanya nini?), nk. Hii inaonesha jinsi worldview yetu inavyotawaliwa na negativity.
Kwa wale wanamichezo, Hii ni sawa na kuongeza ukubwa wa goli ili wachezaji waweze kufunga.
Post a Comment