ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 5, 2013

WAHANGA WA OPERESHENI TOKOMEZA WAILILIA SERIKALI, MKUU WA MKOA WA RUKWA AWATAKA KUWA WATULIVU

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa kijiji cha Kilangawani kufuatia malalamiko yao kwa Serikali juu ya Opersheni Tokomeza. Wengi wao walikiri kutegemea hifadhi ya akiba ya Uwanda kulisha mifugo yao. 

Jambo ambalo wafugaji wameiomba Serikali kuwatafutia maeneo mbadala ya ufugaji. Kwa upande wao wakulima wameiomba Serikali kuharakisha kutafuta suluhu ya mifugo inayozagaa vijijini na mashambani baada ya kufukuzwa kwenye hifadhi kabla ya msimu wa mvua unaokaribia kuanza kwa ajili ya kilimo kuepusha migogoro kati yao na wafugaji. 

Wavuvi na Wajasiliamali wa samaki waliokuwa wakifanya shughuli zao katika ziwa Rukwa nao wameiomba Serikali iwape muda wa kuvua angalao wa miezi mitatu ili waweze kurudisha madeni ya mikopo kutoka taasisi za fedha walizokopa na kupata nauli za kurudi makwao kwani wengi wao wametoka maeneo tofauti ya mikoa ya Mbeya, Ruvuma, Njombe na Kilimanjaro. 
Sehemu ya kundi kubwa la Ng'ombe likionekana mitaani kutafuta malisho na maji katika kijiji cha Maleza katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa baada ya kufukuzwa katika hifadhi ya akiba ya Uwanda (Uwanda Game Reserve) ikiwa ni matokeo ya operesheni Tokomeza inayofanywa na Serikali kunusuru mali asili nchini. 

Maeneo yaliyoathirika kutokana na Operesheni Tokomeza yapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga ambapo zoezi la kuwaondoa majangili na wavamizi wa hifadhi za misitu limegusa vijiji saba (7) vya Ilambo, Maleza, Kilangawana, Mkusi, Kilyamatundu, Nankanga na Msila. Pia wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Rukwa ambapo jumla ya kambi 13 za wavuvi zimechomwa moto.

Inakadiriwa kuwa takribani watu 1600 wameathiriwa na zoezi hili. Aidha, yapo makundi makubwa ya mifugo (ng’ombe) ambayo yamezagaa vijijini na kuna uhaba mkubwa wa chakula kwa familia hizo kutokana na nyumba zao na vyakula kuchomwa moto.

Sehemu ya kundi kubwa la Ng'ombe likionekana mitaani kutafuta malisho na maji katika kijiji cha Kilangawani katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa baada ya kufukuzwa katika hifadhi ya akiba ya Uwanda (Uwanda Game Reserve) ikiwa ni matokeo ya operesheni Tokomeza inayofanywa na Serikali kunusuru mali asili nchini.
kwa picha zaidi bofya soma zaidi
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya akizungumza na moja ya familia zilizoathirika na Operesheni Tokomeza katika kijiji cha Kilangawani alipotembelea hivi karibuni kuzungumza na wananchi wa kata za Kipeta na Mtowisa kufuatia malalamiko yao kwa Serikali juu ya Opersheni hiyo. Malalamiko hayo ni pamoja na ukosefu wa makazi, vyakula, maeneo kwa ajili ya wafugaji pamoja na athari nyingine nyingi zilizosababishwa na Operesheni hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Methew Sedoyyeka akizungumza na moja ya familia ya wafugaji iliyoathirika na Operesheni hiyo kwa kuharibiwa makazi na vyakula mbalimbali. Familia hiyo pamoja na nyingine zinazoishi kandokando ya hifadhi ya akiba ya Uwanda zimekua zikitegemea hifadhi hiyo inayopakana na Ziwa Rukwa katika kulisha na kunywesha mifugo yao jambo lililopelekea uharibifu mkubwa wa hifadhi hiyo na ziwa Rukwa kwa ujumla.

Ndugu Funuki Kapahungu mfugaji na muathirika wa operesheni hiyo akielezea operesheni hiyo iliyompitia na kuiomba Serikali kuwatafutia maeneo mbadala kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji. Hata hivyo viongozi wa Mkoa wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhandisi Stella Manyanya waliwashauri wafugaji hao kufuga kisasa ufugaji wenye tija kwa kupunguza idadi ya mifugo na kuuza mingine kuwawezesha kununua maeneo madogo ambayo watayaendeleza kwa kuyachimbia visima vya maji na kupanda nyasi kwa ajili ya mifugo yao. Alisisitizia juu ya uvunaji wa mifugo kwa kuwawezesha wafugaji kuinuka kiuchumi. 
Ndugu Sadiki Hiari mkazi wa Ilambo akitoa kero zake katika Mkutano huo. Baadhi ya wananchi wengi walitoa ushauri kwa Serikali ya Wilaya, Kijiji na wananchi hususani wafugaji kukaa pamoja na kuweka utaratibu maalum wa kupunguza idadi ya mifugo kulingana na uwezo wa maeneo ya ufugaji tofauti na ilivyo sasa ambapo mfugaji mmoja ana uwezo wa kufuga ng'ombe wengi hadi kufikia 10, 000 bila kuwa na utaratibu wa kuwavuna waweze kuwasaidia kuondokana na umaskini. Wengi wa wafugaji wanaona ufahari kuwa na mifugo wengi bila hata kujali faida yake kiuchumi.

Uwanja wa Mkutano. Katika Mkutano huu Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Stella Manyanya alitoa maagizo na maelekezo mbalimbali yakiwemo Wafugaji waone uwezekano wa kuvuna mifugo yao ya ziada na kuwekeza katika vitega uchumi vingine mfano nyumba, mashine n.k. vitakavyowezesha kuendeleza fedha zao. Serikali zote za vijiji ziainishe maeneo ambayo bado hayajatumika ili kuweza kuyatengea matumizi bora kwa ajili ya mifugo na kilimo na Hiyo izingatiwe kwa Mkoa wote wa Rukwa. Wavuvi nao waliambiwa kila mwaka kuanzia Januari – Machi ziwa litafungwa kwa ajili ya kuwezesha samaki kuzaliana na kukua lakini pia wajizatiti kutumia zana bora za uvuvi. (Na Hamza Temba - Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Rukwa @Rukwareview.blogspot.com)

No comments: